Uongozi wa Wilaya ya Handeni umeungana na wananchi kufanya msaragambo wa kuchimba msingi wa madarasa matano shule ya Sekondari Kwaludege iliyoko Kata ya Kabuku Wilaya ya Handeni Mkoa wa Tanga leo tarehe 29-12-2018 lengo likiwa ni kuhakikisha wanafunzi wote waliofaulu wanaendelea na masomo ya Sekondari bila kukwamishwa na uhaba wa madarasa.
Akizungumza katika amsha ari hiyo kwa wananchi ili kutoa nguvu kazi ya kujenga madarasa hayo Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh. Godwin Gondwe alisema wananchi wawe wazalendo kwa kujitolea kazi za maendeleo ikiwepo kujenga madarasa kwani elimu ni urithi pekee ambao mtu anaweza kumpatia mtoto
Aidha amewaomba wadau wa elimu kutoka maeneo mbalimbali wajitokeze kuchangia ujenzi huu wa madarasa ili kukamilisha madarasa hayo haraka na wanafunzi waweze kupata nafasi ya kusoma hasa wale amabao hawakuchaguliwa awamu ya kwanza.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bw.William Makufwe alisema Halmashauri ya Wilaya ya Handeni inauhaba wa madarasa 49 ambapo itagharimu kiasi cha zaidi ya sh.500,000,000 (million mia tano) kwa mahitaji ya mabati, matofali, saruji, misumari, mbao, nondo, kokoto, chokaa, mchanga hivyo anawaomba wadau wa elimu ndani na nje ya Handeni wachangie chochote kupitia akaunti ya mfuko wa elimu namba 4141200084 benki ya NMB au wanaweza kuchangia kupitia namba zifuatazo 0754832436 au 0712018833 au 0784387557 ili kukamilisha madara hayo mapema na wanafunzi waanze masomo.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Handeni Bw. Athumani Malunda amewataka viongozi wa Kata hiyo kuwajibika ipasavyo kukamilisha kazi hiyo ya ujenzi wa madarasa mapema ili wanafunzi wasipate shida na kwamba wasiruhusu siasa isiingilie masuala ya maendeleo.
Pia amewataka wawekezaji walioko Handeni wahakikishe wanachangia shughuli za maendeleo la sivyo hakuna sababu ya wawekezaji hao kuwepo Handeni kama hawatachangia maendeleo ya Handeni.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Handeni Mwl. Boniphace Maiga aliwapongeza wananchi kujitokeza katika shughuli hiyo ya uchimbaji wa msingi huo na kuwataka wananchi hao kuendelea na moyo huo mpaka madarasa hayo yatakapokamilika na kwamba serikali iko tayari kuungana na wananchi kutatua tatizo la uhaba wa madara.
Aidha ametoa onyo kwa wale ambao wanawapa wanafunzi mimba kuwa serikali itawachukulia hatua kali za kisheria watu hao pamoja na mzazi na mtoto aliyepewa ujauzito(Serikali itawaonyesha namna bora watu hao)alisema.
Wananchi wa Kata ya Kabuku kwa pamoja walipongeza juhudi za viongozi wa Wilaya na wameahidi kujitolea hadi ujenzi huo utakapokamilika na wamesema wao hawako tayari kuona watoto wanabaki nyumbani kutokana na uhaba wa madarasa.
MWISHO.
Mkurugenzi Mtendaji Bw. William Makufwe akichimba msingi
Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh.Godwin Gondwe akichimba msingi.
Katibu Tawala Mwl.Boniphace Maiga akishiriki kikamilifu katika Msaragambo huo
Wadau mbalimbali walijitokeza kuhakikisha misingi ya madarasa matano yamekamilika
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa