Halmashauri ya Wilaya ya Handeni inatarajia kuzindua kampeni maalum ya kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma na kuimarisha uwajibikaji kwa watumishi wa umma. Kampeni hiyo inalenga kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi, sambamba na kuimarisha ushirikiano kati ya wananchi na Halmashauri katika kushughulikia kero mbalimbali za kijamii na kiutawala.
Akizungumza leo Januari 21, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Ndg. Saitoti Stephen, amesema kampeni hiyo itajulikana kwa jina la “TATUA FASTA”, ambapo changamoto zitapokelewa, kuchambuliwa na kutatuliwa kwa haraka na ufanisi ndani ya masaa 24. Ameeleza kuwa mpango huo umebuniwa ili kuongeza kasi ya maamuzi, kupunguza urasimu usio wa lazima na kuhakikisha wananchi wanapata majibu kwa wakati.
Amefafanua kuwa kampeni hiyo itawahusisha kwa kiasi kikubwa watumishi wote wa Halmashauri, ambao watatakiwa kushuka hadi ngazi ya kata, vijiji na mitaa kwa kuwatembelea wananchi moja kwa moja, kusikiliza kero zao na kuchukua hatua stahiki kulingana na mamlaka na majukumu yao. Aidha, watumishi watawajibika kufuatilia utekelezaji wa maamuzi na kutoa mrejesho kwa wananchi kwa uwazi.
Ndg. Saitot amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika kampeni ya TATUA FASTA kwa kutoa taarifa sahihi za changamoto zinazowakabili na kushirikiana na watumishi wa Halmashauri wakati wa utekelezaji. Amesisitiza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni imejipanga kuhakikisha hakuna changamoto inayopuuzwa na kwamba sauti ya mwananchi inasikilizwa na kufanyiwa kazi kwa vitendo.
Handeni
Postal Address: 355 Handeni
Telephone: 0272977402
Mobile:
Email: ded@handenidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa