Vifaa hivyo vyenye thamani ya zaidi ya milioni nne vilitolewa jana Kituo cha afya cha Mkata vikiwepo taulo za kike, mzani ya kupimia uzito wa mtoto aliyezaliwa, kanga, vifaa vya kumsaidia mama wakati wa kujifungua, mipira ya vitanda vya kina mama kujifungulia na mashuka lengo likiwa ni kuwasaidia vijana wa kike walioko shuleni na akina mama wanaopitia katika changamoto hasa wakati wa kujifungua.
Akizungumza katika mapokezi ya vifaa hivyo mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Handeni Bi Upendo Magashi alitoa shukrani kwa Asasi hiyo kwa kuunga mkono kampeni ya Makamu wa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha mtoto wa kike anafikia ndoto zake na amesema tangu asasi hiyo imeanza kufanya kazi Handeni imetoa elimu kwa wanafunzi wa kike ambayo imeleta matokeo chanya. Kwa upende wa Kituo cha Afya amesema Serikali imetoa zaidi ya Milioni mia nne kwa ajili ya upanuzi wa majengo ya vituo vya afya pamoja na vifaa tiba hivyo amewashukuru kuunga mkono juhudi hiyo pia.
Bi.Upendo pia alitumia nafasi hiyo kutoa rai kwa wananchi kushirikiana ili kuhahakikisha mtoto wa kike anafikia ndoto zake lakini pia aliwataka Maafisa elimu kuhakikisha wanachagua walimu ambao wanafunzi wanaweza kupeleka matatizo yao na kwamba majina ya walimu hao yapelekwe Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ili waweze kufanya ufuatiliaji.
Alihitimisha kwa kumtaka Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni kuhakikisha vifaa hivyo vinatunzwa ili viweze kudumu kwa muda mrefu na wananchi wa Handeni kufaidika navyo.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bi.Fatuma Kalovya amesema Asasi hiyo ilianza kufanya kazi Handeni tangu mwezi septemba katika Kata nne ikiwepo Sindeni, Kwamatuku, Kwankonje na Kwaluguru na imewasidia sana vijana kwa kike kujielewa na kuwajengea ujasiri wa kujieleza bila woga.
Pia amewashukuru kwa kuchagua Wilaya ya Handeni na amewasihi kuendelea kutoa mchango wao kwa jamii ya Handeni na amesema vituo vya Afya hasa vilivyoko barabara kuu ikiwepo Mkata na Kabuku vimekuwa na mahitaji makubwa kwani wagonjwa ni wengi kutokana na mwingiliano mkubwa wa watu pamoja na ajali za mara kwa mara
Kiongozi wa Asasi ya HOPE FOR YOUNG GIRLS Bi Salama Kikundo amesema tangu wameanza kufanya kazi Halmashauri ya Wilaya ya Handeni mwezi septemba walifanikiwa kutoa elimu kwa wanafunzi wa kike katika shule saba ikiwepo shule za Sekondari tatu na Msingi nne na wamefurahi sana sehemu zote walizopita walipewa ushirikiano.
Akitoa takwimu ya vitu walivyotoa Bi Salama amesema wanatoa taulo za kike boksi 50, mashuka 200, mzani wa kupimia mtoto baada ya kuzaliwa 1, mashine za kupimia presha 3,mashine za kupima Kisukari 3, mipira ya vitanda vya kuzalia kina mama boksi 2, vifaa vya kumsaidia mama kujifungua 2 na kanga doti 50 ambazo zinathamani ya zaidi ya milioni 4.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Dr. Ipyana Mwiluko ameishukuru Taasisi hiyo kwa msaada wao kwa kuwa wamesaidia kupunguza changamoto kubwa hasa vifaa vya kina mama wakati wa kujifungua na watoto wachanga. Aidha amesema vituo vya Afya vya Kabuku na Mkata vinatibu wagonjwa zaidi ya mia moja kwa siku.
MWISHO.
Imeandaliwa na;
Paulina John
Kitengo cha Habari na mawasiliano Handeni DC
Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Handeni Bi.Upendo Magashi wa tatu kulia akipokea vifaa kutoka kwa kiongozi wa asasi hiyo Bi Salama Kikungo
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bi.Fatuma Kalovya wa kulia akipokea vifaa kutoka mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Handeni
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Dkt. Ipyana Mwiluko wa pili kulia akibeba moja ya vifaa alivyokabidhiwa na kuahidi kuvitunza
Picha ya pamoja baada ya kupokea vifaa
Afisa maendeleo ya jamii Bi.Rachel Mbelwa akitoa shukrani kwa shirika kwa kuja Handeni na kutoa vifaa hivyo
Baada ya kukabidhi vifaa wlitembelea wodi ya wazazi na kuwagawia kanga
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa