HOTUBA YA MHESHIMIWA MKUU WA WILAYA YA HANDENI KWENYE UZINDUZI WA MKUTANO WA UANZISHWAJI WA JUKWAA LA UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI KWA WANAWAKE HALMASHAURI YA WILAYA YA HANDENI TAREHE 20/04/2017 KABUKU.
Waheshimiwa Viongozi mliopo katika uzinduzi wa Jukwaa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi la Wanawake, wananchi wote mliohudhuria katika uzinduzi huu, mabibi na mabwana.
Awali ya yote napenda tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutukunisha wote ili kuweza kuzindua Jukwaa la Uwezeshaji wa Wanawake Kiuchumi la Halmashauri ya Wilaya ya Handeni hii leo. Kauli mbiu ya siku hii ni “WEZESHA WANAWAKE KIUCHUMI ILI KUJENGA UCHUMI WA KATI NA TANZANIA YA VIWANDA”.
Ndugu wananchi,
Uanzishwaji wa Majukwaa ya Kuwezesha Wanawake Kiuchumi ni agizo la Mh.Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan, ambaye aliteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuwa mjumbe mmojawapo wa timu ya viongozi na wataalam ambao watafanya kazi kama chombo cha juu katika kupunguza na kuondoa pengo kubwa ambalo limejengeka Duniani na kuongeza ushiriki wa wanawake katika uchumi duniani kote. Lengo ni kufikia maendeleo endelevu ambayo pia yamesisitiza uwezeshaji wa wanawake kiuchumi.
Ndugu wananchi
Mheshimiwa Makamu wa Rais ameelekeza kuwepo na majukwaa ya uwezeshaji wa Wanawake kiuchumi katika Mikoa yote ikiwa ni pamoja na Halmashauri zake zote za Tanzania. Majukwaa haya yatasaidia kuongeza uelewa wa wanawake katika uchumi, biashara, upatikanaji wa mitaji, sheria za nchi katika masuala ya uchumi na jinsi ya kujitegemea kiuchumi.
Halmashauri zote zimeelekezwa kuunda majukwaa kwa ajili ya kuwakutanisha wanawake ili waweze kujadili masuala yao. Sekretarieti ya Mkoa wa Tanga itaratibu shughuli zote za uchumi kwenye Wilaya zote ndani ya Mkoa na kuhakikisha kunakuwa na majukwaa ya Wilaya/Halmashauri zote ambayo yatafanya vikao vyake kila baada ya miezi sita (6).
Ndugu wanachi,
Lengo la jukwaa litakaloundwa ni kukutana pamoja na kujadili fursa, changamoto na jinsi ya kushiriki kikamilifu katika biashara na shughuli nyingine za kiuchumi katika Halmashauri yetu. Vilevile kuongeza uelewa wa wanawake katika upatikanaji wa mitaji, sheria za nchi katika masuala ya uchumi na jinsi ya kujitegemea kiuchumi.
Wanawake wamekuwa hawapati fursa za kutosha za kiuchumi hapa Tanzania na hata duniani kote. Hii inatokana na kutokuwa na usawa katika fursa, uwezo wa kupata mitaji na ajira.
Pia jukwaa litasaidia kuondoa matabaka na sheria ambazo zitasaidia kupunguza ubaguzi wa kiuchumi kwa wanawake, ambalo ni jambo la muhimu sana katika kuleta maendeleo ya usawa katika pato la Taifa, jamii na familia.
Ndugu wananchi,
Nitajisikia fahari sana ndani ya kipindi hiki nikiwa Mkuu wa Wilaya hii ikiwa wataibuka wajasiriamali wakubwa wanawake miongoni mwenu, nami naahidi kushirikiana nanyi bega kwa bega.
Nimefahamishwa kuwa mtachagua Mwenyekiti wenu wa kwanza kutoka katika mkutano huu wa mwanzo, atakaye simamia malengo yenu hapa Halmashauri, halikadhalika mtaunda pia Sekretarieti itakayohakikisha kuwa viongozi wa jukwaa wanatimiza wajibu wao kwa wakati na kwa haki kwa kufuata sheria zilizopo.
Kazi ya jukwaa mtakaloliunda itakuwa ni kutoa mwongozo wa kimkakati, kuangalia mafanikio ya jukwaa, upashaji habari za kuboresha biashara, kutoa elimu ya kiufundi na mwelekeo kuhusu mitaji na kuweka vipaumbele kuhusu program, fursa za biashara na bidhaa mbalimbali.
Ndugu wananchi,
Napenda pia kuchukua fursa hii adimu kuwasihi wanawake wote wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni kushiriki kikamilifu katika vita iliyopo mbele yetu dhidi ya madawa ya kulevya, ukizingatia Halmashauri yetu imepitiwa na barabara kuu ambayo hupitisha mizigo ya aina mbali mbali kutoka katika sehemu mbalimbali za nchi ikiwa ni ndani na nje ya nchi yetu. Natoa rai muwabaini wote wanaojihusisha na biashara hii haramu wakiwemo wauzaji, watumiaji na wasafirishaji kwa kutoa taarifa kwenye vyombo vyetu vya usalama.
Najua kuna Baraza la Taifa la Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi kikiwa ni chombo cha juu cha serikali ambacho kilianzishwa ili kuratibu na kuongoza shughuli zote za uwezeshaji wananchi kiuchumi zinazoendeshwa na sekta ya umma na binafsi. Baraza pia linasimamia utekelezaji wa será ya Taifa ya uwezeshaji wa wananchi kiuchumi kwa kuongoza Watanzania kwenye uchumi imara na kuhakikisha mazingira mazuri ya biashara na uchumi shirikishi yanakuwepo.
Mwisho natangaza kuwa leo tarehe 20/04/2017, Halmashauri ya Wilaya ya Handeni imezindua rasmi jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi.
Asanteni kwa kunisikiliza.
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa