BARAZA LA MADIWANI LA HALMASHAURI YA WILAYA YA HANDENI YAPATA MWENYEKITI MPYA.
Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga imefanya mabaraza ya siku mbili, baraza la kawaida la robo ya pili ya mwaka na baraza maalumu ya kupitisha rasimu ya bajeti ya mwaka 2019/2020. Katika baraza la kawaida waheshimiwa madiwani walimchagua mwenyekiti mpya wa Halmashauri baada ya nafasi hiyo kuachwa wazi kwa muda wa takribani miezi mitatu kufuatia mwenyekiti wa awali Mh.Diliwa kujiuzuru kutokana na kukataa kusaini muhtasari uliyokuwa unakipengele kinachosema maamuzi ya baraza ya kipindi hicho yaliyofanyika kuhusu makao makuu ya Halmashauri kujengwa Kabuku hayakuwa sahihi.
Uchaguzi huo ulifanyika jana katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni ambapo diwani wa Kata ya Kwamatuku Mh. Mustafa Beleko wa tiketi ya Chama cha Mapinduzi alishinda kwa kura zote 22 ya idadi ya waheshimiwa madiwani waliohudhuria baraza hilo.
Aidha mwenyekiti huyo alipatikana baada ya katibu wa baraza hilo Bw. William Makufwe kuandika barua kwa vyama viwili vya siasa ikiwepo Chama cha Mapinduzi (CCM) na CHADEMA na kupata majibu ya jina moja kutoka CCM. “Tuliandika barua kwa vyama viwili CCM na CHADEMA lakini mpaka leo tumepata barua moja kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) ambayo imeleta jina la mgombea moja kupitia Chama cha Mapinduzi”. Alisema Makufwe.
Mwenyekiti wa Halmashauri Mh. Mustafa Beleko aliwashukuru viongozi wa Chama cha Mapinduzi Wilaya na Waheshimiwa madiwani kwa kumwamini na kumweka katika nafasi hiyo na kuwaahidi kutowaangusha kwani amepata uzoefu wa kutosha kutoka kwa Mwenyekiti aliyepita.
Katika baraza maalumu la kujadili rasimu ya bajeti ya tarehe 05/02/2019 Baraza hilo lilipitisha kwa pamoja rasimu hiyo ya bajeti ya mwaka 2019/2020 kiasi cha shilingi bilioni 36.5.
Afisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bi. Edina Katalaiya akitoa mchanganuo wa bajeti hiyo alisema rasimu hiyo ya bajeti imefuata kanuni, taratibu na mwongozo wa kuandaa bajeti ya mwaka 2019/2020 kutoka Wizara ya fedha na mipango iliyotolewa mwezi Disemba 2018 na vikao vyote vya maamuzi vya Halmashauri.
Aliongeza kuwa rasimu hiyo pia imefuata mwongozo wa undaaji wa bajeti ya mishahara, ilani ya uchaguzi ya chama tawala (Chama cha Mapinduzi), mpango wa pili wa maendeleo wa miaka mitano, mpango mkakati wa Wilaya na mpango wa uwiano wa mkoa. alisema kuwa bajeti hiyo ya billion 36.5 ni kwaajili ya miradi ya maendeleo, kulipia mishahara na matumizi mengineyo.
Waheshimiwa madiwani wakipiga kura ya kumchagua mwenyekiti katika baraza hilo.
Kura zikihesabiwa na mh.Muya wa kwanza kulia, Afisa Utumishi Bi. Kalovya(katikati)
na mwanasheria Bw.Mangesho(wa kwanza kushoto).
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ambaye pia ni katibu wa baraza
Bw.William Makufwe akimvalisha joho mwenyekiti Mh.Mustafa Beleko baada ya uchaguzi
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Mh. Mustafa Beleko akitoa neno la shukrani
baada ya kushinda kwa kura zote za ndiyo.
Kaimu Afisa Mipango, Takwimu na ufuatiliaji Bi. Edina Katalaiya akisoma rasimu ya bajeti ya
mwaka wa fedha 2019/2020.
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa