Baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Handeni limepitisha kwa pamoja rasimu ya bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021 jumla shilingi bilioni 34.8 .
Rasimu hiyo ilipitishwa jana katika kikao cha baraza la kujadili rasimu ya bajeti kilichofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Mkata.
Akifungua kikao hicho Mwentekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Mh. Mustafa Beleko aliwataka waheshimiwa madiwani kutoa michango yao na kuitafakari kwa kina ili kupitisha kwa usahihi bajeti ambayo itadumu kwa mwaka mzima.
Aidha baada ya kupitisha rasimu hiyo ya bajeti Mh.Mustafa aliwataka viongozi wa Halmashauri kwa kushirikiana na Waheshimiwa madiwani kusimamia ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri ili kufikia malengo yaliyopangwa kwa mwaka wa fedha 2020/2021 na kuahidi kwa Kata zitakayofanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato kupewa zawadi zikiwepo pikipiki.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bw. William Makufwe akijibu hoja za wajumbe wa baraza hilo zikiwepo umaliziaji wa miradi ikiwepo Zahanati ya Msangazi, maabara za sayansi kwa shule za Sekondari na uanzishwaji wa vituo vya Afya kwa kila Kata alisema Halmashauri ina mpango wa kumalizia miradi hiyo kadiri itakavyopata fedha na alisema Kituo cha Afya cha Kwamsisi kazi ya ujenzi imeshaanza kwakuwa wafadhili wa shirika la World vision wamefanya kazi kubwa ya kujenga majengo ya awali na kuhimiza Kata zingine kuanza ujenzi wa vituo hivyo ili Halmashauri itakapopata fedha iweze kuongeza nguvu.
Kwa upande wa Zahanati ya Msangazi Makufwe amesema iko kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2019/2020 hivyo itakamilishwa na kuanza kutoa huduma kwa wananchi, amesma maabara za Sayansi zitakamilishwa kwa awamu pale fedha zitakapopatikana kwa kuwa tayari Halmashauri imekamilisha maabara tatu ikiwepo Kwaluguru Sekondari, Ndolwa Sekondari na Kabuku Sekondari.
Alihitimisha kwa kuwasihi waheshimiwa madiwani kuhakikisha wanasimamia mapato ya Halmashauri vizuri ili fedha za kuanzisha na kukamilisha miradi mbalimbali ya Halmashauri ipatikane.
Akisoma rasimu ya bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021 Afisa mipango,takwimu na ufuatiliaji Bi. Edina Katalaiya alisema rasimu hiyo imepitia katika hatua zote za vikao vinavyotakiwa na kuridhia kupitisha kiasi cha shilingi bilioni 34.8 ambayo ni fedha ya miradi ya maendeleo, mishahara na matumizi mengineyo ambapo fedha ya mishahara ni shilingi bilioni 26.88, fedha za matumizi mengineyo ni shilingi bilioni 1.62, miradi ya maendeleo ni shilingi bilioni 4.15 na mapato ya ndani ni shilingi bilioni 2.22.
Kikao cha baraza la rasimu ya bajeti pia kilihudhuriwa na viongozi wa kamati ya ulinzi na usalama pamoja na viongozi wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Handeni ambapo walipongeza utendajikazi wa Halmashauri lakini pia walishauri Halmashauri kuangalia maeneo ambayo wanafunzi wanatoka umbali mrefu kuanzisha shule ili kupunguza adha hiyo, hoja hiyo ilitolewa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Handeni Mwl. Boniphace Maiga pia waliomba pale wananchi wanapochangia shughuli za maendeleo waungwe mkono ikiwepo ujenzi wa barabara, ushauri huo ulitolewa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Handeni Mh. Athumani Malunda
Baada ya kikao cha rasimu ya bajeti Mkurugenzi aligawa mashine za kukusanya mapato 43 zilizotolewa na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI kwa Watendaji wa Kata pamoja na kutoa zawadi kwa Kata zilizoongoza katika ukusanyaji wa mapato zikiwepo Komkonga, Kwamgwe na Kabuku, aliwapongeza watendaji kwa kazi wanazozifanya na kuendelea kufanya kazi kwa weledi.
MWISHO.
Mwenyekiti wa Halmashauri Mh.Mustafa Beleko akisoma dua kabla ya kikao kuanza.
Mkurugenzi Mtendaji Bw. William Makufwe akijibu hoja za wajumbe
Katibu Tawala Wilaya ya Handeni Mwl.Boniphace Maiga akizungumza
Afisa Mipango, Takwimu na Ufuatiliaji Bi.Edina Katalaiya akisoma rasimu ya bajeti 2020/2021
Katibu wa CCM Wilaya ya Handeni akizungumza
Wajumbe wa baraza wakifuatilia kikao
Wajumbe mbalimbali wakiuliza maswali katika kikao.
Mkurugenzi Mtendaji Bw.William Makufwe akitoa mashine za kukusanyia mapato na zawadi kwa Watendaji wa Kata
Mwonekano wa mashine mpya za kukusanyia mapato zilizotolewa na TAMISEMI
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa