Baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Handeni limefanya kikao chake cha robo ya kwanza cha mwaka wa fedha wa 2021/2022 kwenye ukumbi wa Halmashauri.
Mwenyekiti wa baraza hilo Mhe. Mussa Ibrahim Mwanyumbu ameongoza kikao hicho kwa ajili ya kujadili maswala mbalimbali ya maendeleo ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni.
Pia kwenye kikao cha baraza la Halmashauri ya Handeni madiwani walipatiwa semina elekezi ya namna ya kujua majukumu yao kwenye utendaji wao wa kazi. Akitoa semina hiyo Bw. Noel Kazimoto amesema madiwani wanawajibu wa kusimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye maeneo yao, kusimamia ukusanyaji wa mapato, maswala ya elimu, afya, utamaduni na michezo.
Aidha katika baraza hilo lilitoka azimio kuwa kutokana na muundo wa Serikali za mitaa wenyeviti wa vitongoji hawaruhusiwi kumiliki mihuri yeyote kwakuwa hawana mamlaka yoyote ya kupitisha nyaraka zozote kwaniaba ya serikali za vijiji na kwamba Serikali ya kijiji ndiyo ngazi ya pekee ya awali inayoruhusiwa kupitisha nyaraka za serikali.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mhe.Siriel Mchembe kwenye Baraza hilo alimuagiza meneja wa Mamlaka ya maji vijijini na mijini (RUWASA) kuwa kwenye baraza lijalo watoe taarifa za uchimbaji wa visima vilivyochimbwa na idadi ya visima vinavyotoa maji.
Pia Mhe. Mchembe amesema jumuiaya za watumia maji zina changamoto hivyo madiwani wanantakiwa kutambua nafasi zao kwenye jumuiya hizo na kufahamu matumizi ya fedha zinazipatikana kwa jamii.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bw. Saitoti Zelothe Stephen kupitia baraza hilo ametoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuleta jumla ya Tsh.1,820,000,000 za UVICO 19 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi wa madarasa katika Shule za Sekondari na Shule Shikizi za Msingi na alisema Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni wanayo furaha na heshima kubwa kwa kuwaletewa fedha nyingi ambazo haizjawahi kutokea kuletwa kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa wakati mmoja.
Pia amesema Mapokezi ya fedha hizi zimeleta faraja kubwa sana kwa Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni kwani zitasaidia kuleta mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia wanafunzi, kupunguza mrundikano wa wanafunzi darasani, kutia hamasa wanafunzi kwenda shule na kupunguza utoro wa jumla na rejareja, kusaidia wanafunzi wa kidato cha kwanza kuanza masomo kwa wakati na vile vile kuwapunguzia mzigo Wananchi katika kuchangia fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa madarasa pindi wanafunzi wanapochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza na hivyo kuwasaidia wazazi kujikita zaidi katika maandalizi ya mahitaji ya wanafunzi kwa ajili ya kwenda shule hasa katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka.
Afisa Mipango, takwimu na Ufuatiliaji Bi. Amina amesema kuwa utekelezaji wa miradi hiyo unakwenda kama ulivyokusudiwa ili kuhakikisha miradi inakamilikia kwa wakati, na kuipa jina la “Kazi iendelee Programme”
Mwisho.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Mhe. Mussa Ibrahim Mwanyumbu, akiongoza kikao cha Baraza hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mhe. Siriel Mchembe akiongea kwenye kikao cha baraza hilo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bw. Saitoti Zelote Stephen, akiwasikiliza madiwani kwenye kikao cha madiwani.
Wataalam wa Halmashauri ya Handeni wakiwa kwenye kikao cha baraza la madiwani.
Maafisa tarafa wakiwa kwenye kikao.
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa