Baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Handeni limepongeza utekelezaji wa mradi wa ajira za muda mfupi za uchimbaji wa marambo ya maji wa TASAF, mradi ambao umechimwa na wanufaika wa mfuko wa kunusuru kaya masikini (TASAF) kuvuna maji katika kipindi cha mvua.
Pongezi hizo zilitolewa mwishoni mwa wiki kwenye Baraza la madiwani lililofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni.
Akizungumza , Mwenyekiti wa Halmashauri BW. Ramadhani Diliwa alisema kuwa wamepitia miradi ya marambo yote na kuona namna ambavyo wananchi wamejitoa kuchimba kwa ufanisi mkubwa marambo hayo mbali na kwamba, kipindi cha utekelezaji kulikua na changamoto ya jua kali na uhaba wa chakula.
“marambo yamechimbwa kwa mikono na walengwa lakini ukiyaangalia utadhani ni mashine ndio imechimba, Hongereni sana” alisema Mwenyekiti.
Aliongeza kuwa kutokana na changamoto ya kuwepo na maji ya uhakika,wananchi watakuwa na uhakika wa maji kutokana na marambo hayo na hivyo kuwataka kuhakikisha wanayatunza ili yawasaidie hasa katika kipindi ambacho mvua itakuwa imekata.
Aidha, alieleza kuwa kuhusiana na changamoto ya malipo kwa walengwa waliofanya kazi hizo kuwa wavumilivu kwa kipindi hiki ambacho fedha zao zinashughulikiwa na mara fedha zitakapowasilishwa Halmashauri itahakikisha inawalipa kwa wakati.
Jumla ya marambo 63 yamechimbwa ambapo vijiji 45 vinatarajiwa kunufaika na mradi wa marambo hayo katika kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa maji ya uhakika.Mradi wa kunusuru kaya masikini TASAF umeibua miradi ya barabara 4, visima 17 na marambo 63 ambapo miradi yote imegharimu jumla ya Tsh. 661,622,600/=.
Rambo la kijiji cha Kwadoya
Rambo lililopo Mailikumi
Rambo la kijiji cha Mandela
Wanakamati na baadhi ya wanufaika wa mradi wakikagua rambo la mandela
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa