Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Handeni limeridhia kwa pamoja kuacha rasmi matumizi ya vitabu vilivyokuwa vinatumika kukusanyia mapato kwenye baadhi ya Kata, na kutumia mashine za kielekroniki (POS) kuanzia tarehe 1 septemba 2017.
Makubaliano hayo yamefikiwa leo kwenye Mkutano wa Baraza la Madiwani lililofanyika kwenye ukumbi wa Halmashuri, kufuatia Halmashauri kuongeza mashine zingine 50 na kufanya jumla ya mashine 80 ambazo zimesambazwa katika kata zote 21. Mashine hizo zitatumika kukusanyia mapato ambapo kwenye maeneo ambayo yatabainika kuwa na upungufu Halmashauri itaendelea kuongeza mashine.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Mh. Ramadhani Diliwa amewaeleza Madiwani kwamba, jukumu la kukusanya mapato ni la wote na kila mmoja aone anawajibu wa kushiriki kuhakikisha anasimamia vyema ukusanyaji wa mapato kwa maendeleo ya Halmashauri.
Aliongeza kuwa ukusanyaji wa mapato haujalishi ukubwa au udogo wa Kata, kila Diwani anao wajibu kuhakikisha vyanzo vya mapato vilivyopo katika eneo lake anavisimamia ili hata kidogo kilichopo kiweze kupatikana kwa uaminifu wake. Kata zibadilishane mbinu za ukusanyaji wa mapato ili zile zinaoonekana kufanya vyema zisaidie Kata zinazofanya vibaya.
Aidha Mwenyekiti alimtaka Mkurugenzi Mtendaji kuhakikisha anafatilia mienendo ya Watendaji kwa namna wanavyowajibika katika suala la kukusanya mapato ya Halmashauri na kuboresha pale inapobidi. Watendaji watakaoonekana kwenda kinyume na taratibu hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi yao kwa wakati ili iwe fundisho kwa Watendaji wengine.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Bw. William Makufwe amewaeleza Madiwani kuwa mashine zimeongezwa ili kuondoa mianya ya ubadhilifu wa mapato ya Halmashuri na kwamba kwa kushirikiana na wataalamu wa mapato watahakikisha mashine zilizotolewa zinatumiwa kwa malengo yaliyokusudiwa.
Aidha amewaeleza madiwani kuwa , wataalamu wa mapato na Afisa TEHAMA wataendelea kutoa mafunzo kwa Waheshimiwa Madiwani kila Kata juu ya matumizi ya mashine hizo ili iwe rahisi kwao kuweza kusimamia vyema ukusanyaji wa mapato kwenye maeneo yao.
Halmashauriya Wilaya ya Handeni ilianza rasmi kutumia Watendaji wa Kata kukusanya mapato ya ndani kuanzia Septemba 1 mwaka 2016 hadi sasa.
Baraza la Madiwani likiendelea kwenye ukumbi wa Halmashauri.
Mwenyekiti wa kamati ya Fedha,Uongozi na Mipango Mh. Mustafa Beleko akiwasilisha Taarifa
Mh. Amina Mnegelo wa Kata ya Kabuku akiwasilisha taarifa ya Tarafa ya Mzundu
Mwenyekiti wa Kamati ya Ukimwi Mh. Abdalla Pendeza akiwasilisha taarifa wakati wa baraza.
Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii Mh. Joel Mabula akitoa taarifa kwenye kikao cha Baraza .
Mkurugenzi Mtendaji Bw. William Makufwe akizungumza kwenye baraza lililofanyika leo.
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa