Benki ya NMB kanda ya kaskazini imetoa viti na meza 50 leo kwa shule ya Sekondari Kisaza iliyoko Kata ya Komkonga, Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga.
Akitoa shukrani kwa wadau hao wa elimu Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh. Godwin Gondwe amesema benki ya NMB imekuwa mstari wa mbele kurudisha fadhila kwa jamii kwa kusaidia sekta mbalimbali ikiwepo elimu na Afya katika Wilaya ya Handeni hivyo amewashukuru na kuwapongeza kwa kuona umuhimu wa kuchangia juhudi za Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. John Pombe Magufuli.
Mh.Gondwe pia amewapongeza wazazi kwa kuchangia nguvukazi katika ujenzi wa madarasa ambapo amesema hawakusita wakati wowote walipohitajika kuongeza nguvukazi hasa katika kazi za misaragambo ya kuchimba misingi ya madarasa na kusomba mawe.
Alihitimisha kwa kuwasihi wazazi kuwalinda na kufuatilia mienendo ya watoto wao ili waweze kufikia malengo yao na amesema kwa pamoja wanaweza kutokomeza mimba za utoro wa rejareja kwa wanafunzi, pia amewataka wakuu wa shule kuhakikisha wanayatunza viti na meza hizo ili viweze kutumika muda mrefu,
Meneja wa NMB kanda ya kaskazini Bi Acencia Muro amesema viti na meza 50 vilivyotolewa vimegharimu kiasi cha shilingi milioni 5 ambapo ni sehemu ya ushiriki wa benki ya NMB kwa jamii ambayo ushiriki huo hufanyika kila mwaka ili kushirikiana na serikali kwenye sekta muhimu hasa elimu na afya ili kutatua changamoto za jamii inayowazunguka.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bw.William Makufwe amesema lengo la kuleta viti na meza hivyo katika shule ya Sekondari Kisaza ni kwa sababu ni shule iliyoanzisha kidato cha tano na sita hivyo vitasaidia sana kupunguza uhaba mkubwa uliopo kwa madarasa hayo na amesema madawati ni nyenzo muhimu sana kwa wanafunzi kujifunza.
Aidha amesema wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka 2020 ni 4,636 hivyo amewaomba wananchi kuwa wasichoke kuchangia ujenzi wa madarasa ili wanafunzi hao waweze kupata madarasa ya kutosha ya kujisomea huku akiwahimiza wazazi kuwapeleka wanafunzi ambao hawakupata nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza katika vyuo vya ufundi ili waweze kujifunza fani mbalimbali kuliko kukaa manyumbani.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Kisaza Bw.Leornard Mshana amesema anaishukuru sana Benki ya NMB kwa kuwapatia viti na meza hamsini ambapo alisema wanafunzi wa kidato cha tano waliopokelewa mwezi septemba wako 50 mchepuo wa CBG 25 na HGK 25 hivyo madawati hayo yatagawiwa katika vyumba viwili madarasa ya michepuo hiyo.
MWISHO.
Imeandaliwa na;
Paulina John
Kitengo cha Habari na mawasiliano Handeni DC
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa