Mkuu wa wilaya ya Handeni Mh Godwin Gondwe amewataka wananchi wilayani Handeni mkoani Tanga kujiunga na mfuko wa bima ya matibabu (CHF) iyoboreshwa ambapo kwa shilingi elfu 30, jumla ya watu 6 kutoka kwenye familia moja watapatiwa matibabu kwa kipindi cha mwaka mmoja katika zahanati, hospitalina vituo vya afya vyote ndani ya mkoa wa Tanga.
Akiongea wakati wa kufungua Kampeni maalumu ijulikanayo kama *BUKU TANO,TIBA MWAKA MZIMA* iliyofanyika katika viwanja vya shule ya Msingi Kabuku nje, DC Gondwe amesema kuwa gharama ya shilingi elfu 30 kwa watu sita ni sawa na kila mmoja kulipia shilingi 5000 na kupatiwa matibabu mwaka mzima.
Aidha Mh. Gondwe amewataka watumishi wa zahanati, vituo vya afya pamoja na Hospitali ya wilaya kutoa kipaumbele kwa wananchi wenye bima za afya pindiwanapokwenda kupata huduma hizo za afya.
Pia katika ufunguzi wa kampeni hiyo Mh.Gondwe aligawa simu janja 43 kwa Watendaji wa Vijiji kwa ajili ya kusajili wanachama wa bima ya matibabu (CHF) iliyoboreshwa ambapo wakishasajiliwa taarifa zao zitasoma moja kwa moja kwenye mfumo wa CHF iliyoborehwa
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Handeni Bw. William Makufwe amefafanua kwa kusema kuwa, Serikali ilifikia maamuzi ya kupanua wigo mpana wa bima ya matibabu (CHF) ili kutoa fursa kwa wananchi kutibiwa mahali popote ndani ya mkoa wa Tanga huku akimshukuru Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dk John Pombe Magufuli kwa kuwezesha wananchi kupata
huduma bora za afya kwa muhstakabali wa maisha yao.
Nao baadhi ya wananchi ambao wamejiunga na bima hiyo ya matibabu (CHF) iliyoboreshwa wameeleza namna ambavyo bima hiyo imewasaidia ambapo wamesema kuwa wamekuwa wakipatiwa huduma bora za afya na hivyo kutoa wito kwa wengine kujiunga na bima ya matibabu (CHF) iliyoboreshwa."Ugonjwa haupigi hodi na kama unamiliki kadi ya bima hauta kuwa na wasiwasi", alisema mnufaika Mwanahamis Salum.
Awali akisoma taarifa ya maendeleo ya bima ya matibabu (CHF) iliyoboreshwa Mganga mkuu wa wilaya ya Handeni Dk Credianus Mgimba amesema kuwa Mpaka sasa tayari kaya 130 zenye jumla ya wanufaika wa bima ya matibabu (CHF) iliyoboreshwa 772 wameshajiunga huku lengo likiwa ni kupata kaya 52303.
MWISHO
Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh. Gondwe akimpatia simu janja moja ya watendaji kwaajili ya kusajili wanachama wa CHF
Mkurugenzi wa Handeni Bw. William Makufwe akimptia simu janja moja ya watendaji kwaajili ya usajili wa wanachama wa CHF
Viongozi mbalimbali walitoa simu kwa watendaji kwaajili usajili wa wanachama wa bima ya matibabu (CHF).
Mnufaika wa bima ya CHF akiwa kwenye picha ya pamoja na Mh.Gondwe
Mganga Mkuu Wilaya ya Handeni Dr.Credianus Mgimba kushoto akiwa kwenye picha ya pamoja na Mh.Diwani wa Kata ya Kabuku nje Amina Mnegelo
Mkuu wa Idara ya Utumishi na Utawala wa kulia Bi.Fatuma Kalovya akiwa kwenye picha ya pamoja na Mh. Gondwe
Mkuu wa Idara ya Mipango Bi. Edina Katalaiya kulia akiwa kwenye picha ya pamoja na Mh.Gondwe
Wadau mbalimbali walishiriki katika ufunguzi wa kampeni ya Buku Tano, Tiba mwaka mzima.
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa