Uongozi wa Halmashauri ya Wilayaya Handeni umekabidhiwa rasmi mradi wa choo cha matundu sita kilichojengwa na shirika lisilo la Kiserikali CDMT(Community Development Mission of Tanzania) lenye thamani ya Milioni 19 za Kitanzania kwa lengo la kuboresha huduma ya vyoo kwa wanafunzi wa shule za Msingi.
Akipokea mradi huo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Bw. Aweso Bakari ( Afisa Tarafa Mkumburu) alisema kuwa anashukuru sana CDMT kwa kuona uhitaji wa Shule ya Masatu na kuamua kusaidia ujenzi wa choo chenye matundu 6 yatakayosaidia kupunguza changamoto ya vyoo shuleni hapo.
Kaimu Mkurugenzi alisema kuwa,Shule ya Masatu kwa mujibu wa ripoti ya Mwalimu Mkuu ilikuwa na upungufu wa matundu 29 ya vyoo, Hivyo kwa mradi wa matundu 6 yaliyojengwa na Shirika la CDMT umepunguza na kufikia matundu 23, hivyo anashukuru Shirika hilo kwa jitihada za kuunga Mkono Serikali katika ujenzi wa miundombinu.
Aidha aliwataka viongozi wa shule na Kijiji kuhakikisha wanatunza mradi huo kwa kuzingatia usafi wa mazingira ili hata waliofadhili mradi huo wakija kuutazama wafarijike na waweze kuisaidia Serikali kutatua changamoto nyingine ambazo bado zinaikabili shule hiyo.
“Naishukuru sana CDMT , Viongozi wa shule na Kijiji msimamie mradi huu vizuri kuhakikisha hauharibiwi kwa michoro ya ajabu na usafi uzingatiwe ili hata wafadhili wakija kutembelea waone thamani yake” alisema Aweso
Kwaupande wake Diwani wa Kata ya Segera Mh. Yassin Mtamike alisema kuwa, anaishukuru CDMT na yeye kama Diwani atahakikisha mradi huo unatunzwa na kulindwa ili kuwapa nafasi wafadhili waweze kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutatua changamoto mbalimbali za miundombinu.
Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali CDMT(Community Development Mission of Tanzania) na Afisa Ushirika wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bw. Emile Philipo alisema kuwa baada ya kufika Handeni aligundua changamoto ya vyoo bora kwa Shule za Msingi na kuamua kuandika andiko la kuomba msaada kwa Serikali ya Marekani yenye fungu la fedha la Rais wa Marekani linalosaidia Afrika kwa lengo la kupunguza changamoto ya vyoo.
Aliongeza kuwa kwa tafiti zake za awali aliamua kusaidia shule tatu za msingi ambapo shule 2 za Msomera na Masatu zipo Hamashauri ya Wilaya ya Handeni na shule moja 1 ya Seuta Halmashauri ya Mji Handeni.
Miradi yote imekamilika kwa jumla ya Milioni 58 za Kitanzania ambapo kila shule imejengewa matundu 6 ikiwa matundu 3 kwa wanafunzi wa kike na 3 kwa wanafunzi wa kiume.
Muonekano wa jengo la choo kwambele.
Muonekano wa jengo la choo kwa nyuma
ukaguzi wa mradi ukiendelea kabla ya makabidhiano.
Viongozi wakikagua mradi kabla ya makabidhiano
Diwani wa Kata ya Segera Mh.Yassin Matamike kulia akimshukuru Mkurugenzi wa CDMT Bw. Emile Philipo kwa kupena mikono wakati wa makabidhiano ya mradi huo.
Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Masatu Bw. Daniel Daniel akishukuru kukabidhiwa kwa mradi vyoo vya wananfunzi shuleni kwake na Mkurugenzi wa CDMT na Afisa Ushirika Wilaya Bw.Emile Philipo.
Mtendaji wa Kata ya Segera Kulia Bi.Rukia Aweso akipeana mkono wa Shukurani na Mkurugenzi wa CDMT kushoto Bw. Emile Philipo.
Picha ya pamoja baina ya Viongozi, Mkurugenzi wa CDMT na uongozi wa Halmashauri ya Kijiji cha Masatu mara baada ya kukabidhiwa rasmi jengo la vyoo.
muonekano wa choo kwa ndani.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Bw.Aweso Bakari aliyenyoosha mkono akitoa shukurani kwa ujenzi wa jengo la choo hicho.
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa