Taasisi isiyo ya kiserikali inayosimamia maswala ya utawala bora vijijini inayoitwa Civil Education Teachers Association (CETA) imefanya kikao cha tahmini ya kamati zake za vijiji leo katika Ukumbi wa Neema ulioko katika Kata ya Mkata ambapo tahmini hiyo hufanyika kila mwisho wa mwaka ili kuona utekelezaji wa kazi walizofanya, mafanikio na Changamoto .
Akifungua kikao hicho kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bi.Fatuma Kalovya aliwaeleza wajumbe kuwa serikali inaipongeza shirika la CETA kwa mchango mkubwa wanaoutoa katika kuleta maendeleo katika jamii na pia kuipa mafunzo kamati zilizochaguliwa kwenye vjiji mbalimbali ili kufanya ufuatiliaji wa maswala ya utwala bora kwa ufanisi.
Aidha alishukuru kamati hizo kwa kufuatilia miradi mbalimbali inayoendelea na kutoa taarifa na kwamba kupitia taarifa hizo, mambo maovu yanayoendelea vijijini yamekuwa yakichukuliwa hatua. Pia aliwaambia wasijikite kwenye shughuli za maendeleo tu lakini waangalie na mienendo ya kazi za watumishi wa serikali na pale inapotokea baadhi ya watumishi hawatimizi majukumu yao ipasavyo wasisite kutoa taarifa.
Aliongeza kwa kuwaambia wanakamati hao kuwa kazi wanayofanya ipo kwa mujibu wa kanuni, taratibu na sheria hivyo waifanye kwa ujasiri na kwa kujiamini kwani serikali inathamini kazi yao na inawaahidi kuwalinda na kwamba kamati yoyote ikipata usumbufu ipeleke malalamiko yake Idara ya maendeleo ya jamii kitengo cha dawati la malalamiko madai hayo yatashughulikiwa kwa wakati.
Pia amewasihi wanakamati hao kuendelea kutoa elimu kwa wananchi na viongozi kupitia mafunzo waliyofanyiwa kwani suala la utawala bora bado ni changamoto katika ngazi za vijiji kwasababu mikutano ya vijiji havifanyiki kwa wakati na maeneo mengine havifanyiki kabisa kitu kinachofanya maendeleo yarudi nyuma hivyo watoe elimu ili vikao hivyo vifanyike kwa wakati na kwa mujibu wa ratiba iliyowekwa.
Kalovya aliwaeleza pia kamati hizo kutumia maafisa maendeleo ya jamii ili waweza kuwasaidia katika suala la uhamasishaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo na kuhamasisha vikao kwani bila vikao wananchi hawawezi kuchangia shughuli za maendeleo lakini pia wananchi hawataweza kupata mrejesho wa michango yao waliyotoa hivyo wanakosa imani na viongozi wao hata kama hakuna lolote baya limefanyika “bila vikao vya mapato na matumizi wataona wanaibiwa hata kama hakuna kitu”alisema.
Alihitimisha kwa kuwataka kushiriki kwa pamoja kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika kwa manufaa ya umma hasa masuala ya uuzwaji holela wa ardhi bila kufuata sheria hivyo wasisite kutoa taarifa kwani ofisi ziko wazi, Pia aliomba uongozi wa CETA kupatia mafunzo kamati za vijiji vilivyobaki kwakuwa mpaka sasa wamewapatia mafunzo wanakamati wa vijiji 44 kati ya vijiji 91.
Mkurugenzi wa CETA Bw. Safari Minja alisema shirika hilo limenza kufanya kazi Tanzania tangu mwaka 2003 lakini kwa Handeni ilianza kufanyakazi mwaka 2012 ambapo ilianza na mafunzo ya wanakamati katika vijiji 9 na kadiri muda unavoenda walizidi kuwaongeza hadi kufikia vijiji 44 mwaka huu na kwamba lengo lao ni kufikia vijiji vyote 91 vya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni ifikapo mwaka 2020.
Alisema baada ya kamati hizi kufanyiwa mafunzo ya wajibu na majukumu ya serikali za vijiji na kuanza kufanya ufuatiliaji ubadhirifu wa fedha za serikali umepungua kwani wamekuwa wakitoa taarifa na hatua mbalimbali zilichukuliwa lakini pia miradi iliyosimama ilitekelezwa na kutumika na jamii kwa matumizi yaliyokusudiwa, taratibu za matumizi ya fedha zimetumika na kwa wale viongozi wanaokusanya fedha bila risiti pia wamedhibitiwa na sasa fedha zinakusanywa na risiti halali za Halmashauri zinatolewa.
Moja wa wanakamati ya kufuatilia maswala ya utwala bora vijijini Bw.Hassani Selemani alisema kupitia shirika hili tumepata elimu juu ya utawala bora kwani mwanzo tulikuwa hatuelewi na sasa tunauelewa mkubwa na pia tunafuatilia na kulinda ya rasilimali za serikali ili zitumike kwa maslahi ya umma lakini pia vitumike vizuri.
Aidha alisema changamoto wanazokutana nazo ni baadhi viongozi kutokuwa wawazi kwao pale wanahitaji maelezo kuhusu jambo na pia hawataki kukaguliwa au kuwazungusha pale wanapohitaji taarifa.
Baada ya kikao hicho kamati za vijiji vilivyofanya vizuri walipewa zawadi ya baiskeli kwa kila kijiji kama ambavyo wao wenyewe waliomba kupewa hizo baiskeli ambapo vijiji hivyo vilikuwa 6 ikiwepo kijiji cha Kitumbi, Manga, Magamba, Kwamatuku, Kibindu na Mazingara lakini pia Mwenyekiti wa wanakamati Halmashauri ya Wilaya alipewa simu janja(smart phone).
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Bi.Fatuma Kalovya akizungumza
Wajumbe wakisikiliza maelekezo
Wanakamati wakiwa kwenye picha ya pamoja na Kaimu Mkurugenzi baada ya kukabidhiwa baiskeli na mwenyekiti wa wanakamati Wilaya alipewa simu janja
Timu ya viongozi kutoka Halmashauri wakiwa kwenye picha ya pamoja
Kamati pia zilisoma majukumu waliyotekeleza kwa Mkurugenzi kipindi cha mwaka mzima.
Mkurugenzi wa CETA Bw.Safari Minja akizungumza katika kikao hicho.
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa