Katika kuhitimisha juma la sheria muwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Handeni Bi. Upendo Magashi (Afisa Tawala Wilaya) amewaasa wanasheraia na watumishi wa mahakama kuendelea kuelimisha wananchi mambo mbalimbali yanayohusu sheria ili kurahisisha upatikanaji wa haki.
Rai hiyo imetolewa leo alipokuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Mh. Gowin Gondwe kwenye maadhimisho ya kilele cha juma la sheria yaliyofanyika kwenye viwanja vya Mahakama ya Wilaya. Alisema wananchi wengi wakishindwa kesi wanaenda kulalamikkia kwenye maeneo yasiyostahili wakijaribu kutafuta msaada.
Afisa Tawala amesema ni vyema wananchi wakajua taratibu na kanuni za kufuata tangu kesi inapoanza hadi tamati ili kuwasaidia kuweza kupata haki zao na kuepuka malalamiko yanayoweza kuzuilika.
“ Ni imani yangu kwamba kila muhimili ukifanya kazi kwa weledi , malalamiko yatapungua na wananchi wataweza kujishughulisha na shughuli nyingine za maendeleo. Matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano yanalenga kuboresha utoaji wa huduma hivyo tutumie ipasavyo” alisema Afisa Tawala
Ameongeza kuwa katika kipindi ambacho Teknolojia inakua mazingira ya kazi na vitendeakazi lazima vibadilike kulingana na wakati ili kuweza kukidhi mahitaji ya wananchi, Na kuendelea kuzingatia maadili na weledi ili kila mmoja aweze kupata haki kwa wakati.
“Mbali na changamoto zilizopo Serikali inaendelea kuziba mapengo yaliyopo na kuhakikisha upatikanaji wa vitendea kazi vitakavyosaidia usikilizaji wa kesi na utoaji wa nakala za hukumu kwa wakati, Hivyo Watumishi wa Mahakama wanapohitaji kwenda kupata mafunzo mafupi waruhusiwe ili waweze kwendana na kasi ya matumizi ya TEHAMA” amesema Afisa Tawala.
Aidha aliwataka waendesha mashitaka na wapelelezi kuhakikisha wanawapa wafungwa muendelezo wa kesi zao badala ya kuwaacha wakiwa hawajui hatma ya kesi zao.
Naye muwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Kilindi Dk.Philis Nyimbi (Katibu Tawala Kilindi) amesema uwepo wa muhimili wa Mahakama umewezesha viongozi kuweza kufanya kazi kwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa, Hivyo kwa kutumia TEHAMA kutawezesha kupata taarifa sahihi za washtakiwa kwa wakati na kutoka mahakama moja kwenda nyingine.
Mh. Hakimu Mkazi Mfawidhi Wilaya ya Handeni na Kilindi Bw.Anorld Kileo amesema kuwa maadhimisho ya juma la sheria huashiria mwaka mpya wa Mahakama, ambapo inapata nafasi ya kujitathmini kiutendaji na kuweka malengo na mikakati inayotekelezeka kwa mwaka mwingine.
Ameongeza kuwa Mahakama inalenga kutoa elimu pana kwa jamii na, kwakutumia TEHAMA Mahakama itaweza kutekeleza kwa weredi jukumu la msingi la utoaji haki, kuimarisha uwazi na uwajibikaji, kusikiliza na kutatua kero za wananchi ili kuhakikisha inakua sehemu pekee ya watu kupata haki.
Maadhimisho ya siku ya sheria Nchini hufanyika kila mwaka wiki ya kwanza ya mwezi wa pili. Maadhimisho hayo yalijumuisha wadau mbalimbali kutoka Wilaya ya Handeni na Kilindi , wakiwemo Wanasheria, Mawakili, Idara ya Uhamiaji, Magereza, TAKUKURU na Polisi, yenye kauli mbiu ya “Matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa haki kwa wakati na kwa kuzingatia maadili”.
Muwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Handeni Bi. Upendo Magashi (Afisa Tawala Wilaya) akihutubia wananchi kwenye kilele cha juma la sheria.
Dk Philis Nyimbi muwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Kilindi Mh. Sauda Mtondoo akizungumza kwenye kilele cha juma la Sheria.
Mh. Anorld Kileo Hakimu Mkazi Mfawidhi Wilaya ya Handeni na Kilindi akizungumza na wageni waalikwa na wanachi kwenye kilele cha juma la Sheria
Mwanasheria wa Halmashauri ya wilaya ya Handeni Bw.Amani mangesho akitoa maada kwenye kilele cha juma la Sheria.
Meza kuu
Mwanasheria wa Halmashauri ya Mji Handeni Mwanaamina Mruma akizungumza na wanachi kwenye maadhimisho ya kilele cha juma la Sheria
Baadhi ya wananchi
Mkuu wa Takukuru Wilaya ya Handeni Bi. Esta Mulima akisisitiza kuzingatia maadili ili kuepusha vitendo vinavyoweza kusababisha lengo la kutoa haki kwa wakati lisitimie Kama ilivyokusudiwa.
Baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya Handeni
Habib Rashid (moja kwa moja) kutoka Ithnasharia Community akiomba wananchi wafahamishwe juu ya sheria na taratibu za kufuata pale ambapo hawajaridhia na hukumu iliyotolewa.
Picha ya pamoja Mara baada ya maadhimisho
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa