Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh.Godwin Gondwe amekutana na wawekezaji wa madini ya DOLMITE kutoka India lengo likiwa ni kutembelea maeneo yenye madini hayo ili kuona wingi na ubora ambapo walitembelea moja ya maeneo hayo katika kijiji cha Chanika Kofi Kata ya Ndolwa.
Akizungumza na wawekezaji hao jana Mh. Godwin Gondwe aliwapongeza na kuwashukuru kuja kuwekeza Handeni na pia aliwahakikishia kuwa madini ya DOLMITE yapo ya kutosha Handeni kwa kuwa kuna hekta nyingi za maeneo mbalimbali yenye madini hayo hivyo watapata malighafi ya kutosha na yenye ubora kulingana na mahitaji ya kitu wanachohitaji kutengeneza na kwamba kuwekeza kwao Handeni ni moja ya kutimiza ndoto ya Mh.raisi ya Tanzania ya viwanda.
Aliongeza kwa kusema kuwa sera ya serikali ya Tanzania inawaunga mkono wawekezaji hivyo kwa msaada wowote watakaouhitaji yeye yuko tayari kuwasaidia na pia kwa kuwa malighafi mengi yanapatikana Handeni hivyo kiwanda pia kitajengwa Handeni ni kiasi cha kuchagua sehemu bora ambayo itakidhi mahitaji ya kuendesha kiwanda hicho.
Amehitimisha kwa kuwataka wananchi kuwapokea wawekezaji hao na kuwapa mazingira bora ya kuwekeza na kwamba Handeni ajira za kudumu na muda zitapatikana kupitia wawekezaji hao hivyo maafisa biashara na idara ya maendeleo ya jamii kuhakikisha wawekezaji wakija wanahudumiwa haraka ili wawekeze haraka, serikali ipate kipato chake na wao kama wawekezaji waweze kunufaika na uwekezaji wao katika nchi yetu ya Tanzania.
Aidha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmasahuri ya Wilaya ya Handeni Bw.William Makufwe amewashukuru wawekezaji hao kuonyesha nia ya kuja kuwekeza Handeni na kwamba Handeni inawakaribisha wawekezaji kuja kuwekeza katika sekta mbalimbali kwani Handeni inamikakati ya kuhakikisha kwamba wawekezaji wakifika kwenye Wilaya yetu na wamevutiwa na uwekezaji wowote tunawapa ushirikiano unaostahili kwa kuwa nia yetu ni kutengeneza viwanda vingi kadiri inavyowezekana ili kufikia nia na ndoto ya Mh.raisi wetu ya kutengeneza viwanda vyenye thamani ya mahitaji yetu tuliyonayo
Kwa upande wake kaimu Afisa madini mkazi wa Wilaya ya Handeni Bw.Naiman Abdiel Samana aliwaeleza wawekezaji hao kuwa Handeni ina aina mbalimbali ya madini yakiwepo madini ya viwandani, madini ya ujenzi na madini ya vito ambayo yanapatikana katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Handeni, Pia kwa upande wa madini ya Dolomite Handeni ina jumla ya hekta 302.69 yakiwepo maeneo ya Kwedikwazu,Chanika Kofi na Mumbwi na maeneo hayo yanafikika kwa urahisi na kwamba wao wakotayari kuwaelekeza wawekezaji namna ya kupata leseni ya utafiti na leseni ya uchimbaji wa madini.
Naye mkazi wa kijiji cha Chanika Kofi BW.Hassani Mkombozi amesema kuwa amefarijika kuona ujio wa wawekezaji kwani wanahandeni watanufaika kupitia wawekezaji hao kwa kupata ajira zitakazoinua hali ya uchumi ya watu wa Handeni.
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa