Halmashauri ya Wilaya ya Handeni imefungua duka/stoo ya kuhifadhia dawa ili kukabiliana na changamoto ya upungufu na ukosefu wa dawa kwa wakati kwenye Hospitali ya Wilaya ya Handeni.
Uwepo wa duka hilo umekuja kufuatia changamoto zilizokuwa zinaikabili Hospitali pamoja na Vituo vya Afya ya upungufu na ukosekanaji wa dawa na wakati mwingine kutokupata dawa kwa wakati pindi wanapoagiza Bohari Kuu ya Dawa (MSD).
Akizunguma Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni BW. William Makufwe wakati wa ziara na madiwani kwenye Duka/ Stoo hiyo alisema kuwa, tumeamua kukabiliana na changamoto ya upungufu na malalamiko ya wananchi ya ukosefu wa dawa kwa muda mrefu kwenye Hospitali yetu na vituo vya afya kwa kufungua Duka/Stoo ambayo itakuwa na dawa za aina mbalimbali ili kuboresha huduma.
Aliongeza kuwa vituo vyote vya afya kwasasa vitakuwa vinachukua dawa kwenye duka/stoo ya Hospitali ya Wilaya pindi dawa zinapohitajika badala ya kuagiza moja kwa moja MSD.
kuagiza dawa MSD kulikuwa kunachelewesha upatikanaji wa dawa kwa wakati na hivyo kusababisha upungufu wa dawa ambao ulikuwa unasababisha malalamiko ya muda murefu kutoka kwa wananchi.
“ukiona unapata maelezo yasiyoeleweka kuhusiana na upatikanaji wa dawa kwenye maeneo yote yanayotoa huduma za afya piga simu kwangu moja kwa moja namimi nitashughulikia” alisema Makufwe.
Aidha, aliwaomba waheshimiwa madiwani kuendelea kuhamasisha kaya kuendelea kujiunga na mfuko wa afya wa jamii (CHF) ambao kwa kiasi kikubwa umesaidia upatikanaji wa fedha za kununulia dawa, ambapo kwa kuongeza idadi ya kaya wanaojiunga na CHF kutasaidia kuwepo kwa dawa maratatu zaidi ya zilizopo.
Aliwaomba pia kusimamia dawa zinazopelekwa kwenye vituo vyao vya afya ili kuepuka dawa kuhujumiwa na kuibwa.
Mfamasia wa Hospitali ya Wilaya ya Handeni Mustafa Lutavi alisema kuwa kabla ya kufunguliwa kwa duka hilo hospitali ilikuwa inachangamoto kubwa ya ukosefu wa dawa za kutosha hali iliyopelekea malalamiko ya mara kwa mara kwa wananchi wanaopata huduma kwenye hospitali hiyo na vituo vya afya.
Alieleza kuwa CHF imepanga kuboresha huduma zake ambapo badala ya wananchama kupata huduma kwenye vituo vilivyopo Wilayani, waanze kupata huduma ngazi ya Mkoa.
Mbunge wa Handeni Vijijini Mh. Mboni Mhita na waheshimiwa madiwani walimpongeza Mkurugenzi na timu yake nzima kwa ujumla kwa jitihada walizozionesha katika kukabiliana na changamoto hiyo na kwamba wao kama viongozi wenye dhamana kwa wananchi wataendelea kuhamasisha wananchi kujiunga na mfuko wa afya wa jamii CHF ili kuendelea kuboresha huduma za Afya, huku akiahidi kuendelea kufuatilia uapatikanaji wa watumishi wa idara ya afya kupunguza changamoto ya upungufu wa watumishi.
Baadhi ya Waheshimiwa Madiwani wakiwa kwenye duka la dawa.
Baadhi ya Dawa
Waheshimiwa madiwani wakiwa kwenye picha ya pamoja nje ya Duka/Stoo ya Dawa.
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa