HANDENI IMEPATA MWEKEZAJI MWINGINE WA MIHOGO.
Wilaya ya Handeni imepata mwekezaji mwingine wa zao muhogo ambapo jana walifanya mazungumzo ya awali na Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh.Godwin Gondwe, Mazungumzo hayo yalifanyika Kata ya Mkata katika ukumbi wa Hotel ya KN na baadaye walitembelea shamba la mkulima bora katika Kata ya kitumbi kujionea ubora wa mihogo na ardhi.
Akizungumza katika kikao hicho Mh. Godwin Gondwe alimshukuru mwekezaji huyo kuona Handeni ni eneo muhimu la kuja kuwekeza na kwamba Handeni ni sehemu sahihi yakuja kuwekeza, Pia alimtoa wasiwasi mwekezaji huyo baada ya kutaka kujua ubora wa mihogo, ubora wa ardhi, upatikanaji wa umeme, upatikanaji wa ardhi na maswala ya utozaji kodi alisema Handeni kuna mihogo bora na safi kuliko sehemu yoyote Tanzania kwakuwa Handeni inatumia ardhi ambayo ina mbolea ya asili hivyo ina rutuba yakutosha na kwamba Handeni shina moja ya muhoga inatoa mpaka kilo kumi ukilinganisha na maeneo mengine Tanzania.
Aliongeza kuwa Handeni inalima mihogo kama zao la kimkakati hivyo uzalishaji wake unafaa kwa matumizi ya viwanda kwa hiyo anamkaribisha mwekezaji huyo handeni kujenga kiwanda cha kuchakata mihogo kwani Handeni kuna umeme, barabara zinazofikika kwa urahisi kwakuwa si zaidi ya kilometa kumi kutoka barabara kuu
Mh. Gondwe alisema kuwa Handeni kwa sasa imehamasika kulima muhogo na uzalishaji umekuwa mkubwa hivyo alimwomba ajenge kiwanda Handeni na kwamba endapo mwekezaji huyo atajenga kiwanda Handeni atapewa ardhi ya kujenga kiwanda bure takribani ekari kumi na tano na pia atauziwa mashamba kwa bei nafuu endapo ataamua kulima, Pia alimtaka mwekezaji huyo kutenga muda ili aje kuona maeneo ya kujenga kiwanda pamoja na kukutana na wataalamu wa TRA na TANESCO ili apate ufafanuzi wa kutosha kuhusu masuala ulipaji kodi na umeme.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bw.William Mkufwe amesema kuwa yeye yuko tayari kutoa ushirikiano kwa wawekezaji watakaokuja kuwekeza katika Halmashauri ya Wilaya ya Handeni ili kuweka Tanzania katika uchumi wa kati pia amemshukuru mwekezaji huyo kuja katika Halmashauri yake na kwamba kwasasa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni imezalisha tani takribani milioni 1.3 za mihogo katika ekari 184,338 za wakulima wadogo kwa mwaka huu na tunategemea kuzalisha mara tano kwa mwaka 2018/2019 kwakuwa wakulima wamelima mihogo kwa wingi sana.
Makufwe alisema kwasasa Handeni imepata wawekezaji wanaochakata mihogo lakini bado hawajaweza kukidhi mahitaji ya wakulima hivyo atafurahi mwekezaji akijenga kiwanda Handeni ili wakulima wapate soko la kutosha na kuepukana na adha ya kuharibika kwa zao hilo la muhogo.
Kwa upande Afisa kilimo, Umwagiliaji na Ushirika Bw. Yibarila Chiza alisema Handeni inajumla ya watu 325415 na asilimia 60 ya wakazi ni wazalishaji na pia ina jumla ya hekta 645299 na kati hizo asilimia 53 zinatumika kwa kilimo
Ameongeza kuwa mazingira ya kuwekeza Handeni ni rafiki kwakuwa malighafi zitapatikana na kukidhi mahitaji ya kiwanda kwasababu Kata zote 21 za Handeni zinazalisha mihogo na kwa ekari moja mkulima anapata tani 8-12.
Mwakilishi wa uongozi wa bandari ya Tanga Bw. Moshi Mtambalike naye alitoa ufafanuzi kuwa bandari ya Tanga inatakribani ya miaka 200 sasa na ni bandari kongwe kuliko yote katika ukanda wa Afrika ya mashariki.
Pia amesema bandari ya Tanga haina msongamano mkubwa ukilinganisha na bandari zingine hivyo itakuwa rahisi kusafirisha malighafi kwa urahisi na pia haina umbali mrefu kutoka Handeni ambapo umbali wake ni kilometa 134 kutoka Handeni hivyo pia inafikika kwa urahisi ukilinganisha na bandari zingine.
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa