HANDENI WAFANYA KIKAO KAZI CHA TATHMINI YA MATOKEO YA DARASA LA SABA 2018
Uongozi wa Wilaya ya Handeni umefanya kikao kazi na wadau wa elimu wakiwepo Maafisa elimu Kata, Walimu wakuu, Wakuu wa shule, Maafisa Tarafa na Watendaji Kata lengo likiwa ni kufanya tathmini ya matokeo ya darasa la saba kwa mwaka 2018, Kikao hicho kilifanyika jana katika ukumbi wa CCM Handeni
Akizungumza katika kikao hicho Mgeni rasmi ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh. Godwin Gondwe aliwataka Wakurugenzi kuweka mikakati ya ufundishaji kuinua kiwango cha elimu ili kutoka hatua ya asilimia walizopata mwaka huu hadi kufikia asilimia 90 msimu ujao kwa darasa la saba, kidato cha nne na asilimia 100 kwa darasa la nne na kidato cha pili.
Aliongeza kuwa Idara za Elimu zinatakiwa kufanya ufuatiliaji wa namna ya ufundishaji shuleni na kusikiliza changamoto zinazowakabili Walimu na kuzitatua kwa haraka na kwamba agenda ya kuinua kiwango cha ufaulu iwe ya kudumu katika vikao wanafavyofanya kwa ngazi zote ili wazazi na walezi nao waelewe .
Gondwe aliwataka wadau hao kuimarisha elimu ya kujitegemea kwa shule za Msingi na Sekondari kwani Handeni haina uhaba wa ardhi “Shule ikiwa na ekari chache ni ekari mbili” alisema, hivyo aliwahimiza Shule kulima Mahindi, Mihogo na mazao mengine ili kuwe na chakula cha kutosha kwa Wanafunzi na kuhakikisha pia wadau hao wanasimamia suala la utoro wa Wanafunzi na kusema sheria zipo kwaajili ya kuwasaidia watoto wetu “tushirikiane” alisema.
Pia alitaka Kamati za shule zijengewe uwezo katika vikao vyao vya robo ya kwanza na pili ili zitambue nafasi zao za kuinua maendeleo ya taaluma katika shule zao kwasababu Kamati zipo lakini hazifahamu malengo yao hivyo tuendelee kuzikumbusha wajibu wao ili ziendelee kusimamia maendeleo ya taaluma katika maeneo yao na aliwaagiza walimu kutoa mazoezi ya kutosha , mitihani ya wiki na mwezi pamoja na mitihani ya utimilifu ngazi ya Wilaya kwa darasa la nne na darasa la saba kwa kutumia rasilimali walizonazo.
Aidha Gondwe aliwahimiza wadau hao hasa Watendaji Kata kuhakikisha wanamaliza tatizo la uhaba wa madarasa kutokana na ufaulu kuongezeka ambapo alisema kwa Halmashauri ya Wilaya zinahitajika jumla ya madarasa 49 na kwa Halmashauri ya Mji zinahitajika madarasa 13 hivyo aliwataka mpaka mwezi wa pili mwaka 2019 madarasa hayo yawe yamekamilika na alisema kwa Wilaya ya Handeni hakutakuwa na Wanafunzi watakaobaki nyumbani kwasababu ya kukosa madarasa.
Alihitmisha kwa kuwataka wathibiti bora wa elimu kukagua maendeleo ya shule zetu kwa mujibu wa mwongozo na watoe taarifa mapema kwa viongozi na kuwataka pia Maafisa Elimu Kata kufuatilia ufundishaji na ujifunzaji wa wanafunzi shuleni.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bw. William Makufwe aliwapongeza Wadau wa elimu kwa kuchangia kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu kutoka asilimia 73 mwaka 2017 hadi asilimia 81.6 mwaka huu na kutoka nafasi ya 5 kimkoa mwaka 2017 na kupata nafasi ya 4 mwaka huu.
Mkurugenzi pia alitaja shule kumi zilizofaulisha kwa asilimia mia moja na ikiwepo shule ya msingi Gendagenda, Mgambo, Imani, Kwamwachalima, Lukolongwe, Mkumburu, Kwediloko, Manga, Kwamnele na Kwedibago.
Aidha alikazia suala la ujenzi wa madarasa kwa shule zote zenye upungufu wa madarasa na kwamba Watendaji wanatakiwa kusimamia ujenzi huo na kuhamasisha wananchi kutoa nguvu kazi, pia alitaka zile Kata ambazo hazina Shule za Sekondari wahakikishe na wao wanaanza ujenzi ili kupunguza idadi ya wanafunzi kwenda kwenye Kata zingine hususani Kata ya Kitumbi na Kata ya Misima.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya Bw. Malunda aliwapongeza Walimu kwa kufanya kazi kwa moyo japo wengine wanafanyakazi katika mazingira magumu pia aliwasihi walimu kuwa na mshikamano na umoja na kwamba serikali itashughulikia madai ya walimu lakini walimu pia wahakikishe hayo madai yao wamefanyia kazi.
Naye Afisa elimu Msingi Bw. Gooluck Mwampashe waliwasihi wadau hao kushirikiana kwa pamoja na kuwaelekeza Walimu wakuu na Wakuu wa Shule kuwasimamia walimu ili wafundishe kwa kufuata kanuni, taratibu na sheria.
Pia aliwahimiza wadau hao kuchangia mfuko wa Elimu kama ambazo waliweka viwango kwa kila mdau ambapo alisema kiwango cha kuchangia ni kuanzia shilingi 5000 kwa viongozi na shilingi elfu 4000 kwa walimu.
Katika kikao hicho walimu wakuu wamama walipongezwa kwakuwa wengi wao walifaulisha shule zao kwa kupata asilimia kubwa ikiwepo kufaulisha kwa asilimia mia moja ambapo Mwalimu mkuu wa Shule ya msingi Gendagenda alitolewa mfano kwa kuwa shule ina mazingira magumu na imefaulisha kwa aslimia 100 na alizawadiwa shilingi laki moja kama pongezi na motisha kutoka kwa wadau mbalimbali na Wakuu wa shule wengine waliofaulisha kwa asilimia 100 walipewa elfu kumi kila moja kutoka kwa wadau mbalimbali na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya alisema kuna utaratibu maalumu unaandaliwa ili wapewe zawadi zao rasmi.
Pichani ni Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Bw. William Makufwe akizungumza na wadau wa elimu
Pichani ni Wadau wa Elimu wakiwepo Maafisa elimu Kata, Maafisa Tarafa, Maafisa tendaji Kata,
Wakuu wa Shule na Walimu Wakuu wakisikiliza.
Pichani ni Baadhi ya Walimu wakuu wa Shule zilizofaulisha kwa asilimia 100
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa