Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni umekabidhi matrekta manne (4) kwa vikundi vya uzalishaji na kuvitaka vikundi hivyo kutumia matrekta hayo kwa lengo la kuchochea kasi ya maendeleo ya kilimo kwenye maeneo yao.
Akikabidhi matrekta hayo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Mh. Ramadhani Diliwa amewaeleza vikundi kuwa Halmashauri imeamua kuwapa matrekta hayo kama mtaji kutokana na utayari wa vikundi vyenyewe kwani vikundi vipo vingi ambavyo vingeweza kupewa na hivyo watambue wanao wajibu wa kuyatunza na yasiwe chanzo cha migogoro.
Amesema kuwa Halmashauri inatekeleza ilani ya chama cha mapinduzi ya kuhudumia wananchi, matrekta yaliyotolewa wangeweza kutoa hata kwa mtu mmoja mmoja lakini yametolewa kwa vikundi ili kuchochea maendeleo na kurahisisha utunzaji wa mradi huo.
“kasaidianeni matrekta haya yakachochee na kuboresha kilimo, kuongeza uzalishaji na tija asitokee mtu mmoja kati yenu akawa ni chanzo cha mafarakano, Halmashauri haitavumilia tutawapokonya na kuwapa wahitaji wengine” alisema
Ameongeza kuwa matrekta yote matengenezo yake yapo chini ya Suma JKT hivyo iwapo kutatokea hitilafu yoyote wasitumie mafundi wa mitaani kuyatengeneza badala yake yafikishwe kwa walengwa wa matengenezo, na kuwataka wasitumie mradi huo kwa lengo la kujinufaisha mtu binafsi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni William Makufwe amesema kuwa matrekta yamekabidhiwa kwa vikundi kwa kuamini vitarahisisha katika utunzaji na kuvitaka vikundi hivyo kutumia matrekta hayo kama iivyokusudiwa kwa kuzingatia muda wa kufanya kazi na kuyapumzisha ili yaweze kudumu.
Aidha ameongeza kuwa matrekta yote mbali ya kuwa mali ya vikundi lakini yapo kwenye Vijiji hivyo ni wajibu wao kutoa taarifa ya usimamizi wa matrekta hayo kwenye uongozi wa Vijiji ikiwa ni pamoja na kuwasilisha mapato ghafi (10%ya mapato) kwenye miradi ya maendeleo ya Vijiji vyao na mwisho wa siku kuongeza uzalishaji utakaopelekea wananchi kuishi kwa amani na utulivu.
“Matrekta haya ni mradi kama ilivyo miradi mingine , naomba yasiwe chanzo cha migogoro,kuwepo na uaminifu na uwazi katika kuendesha mradi, hii ni mali ya kikundi sio ya mtu binafsi na taarifa zote ziwekwe kwenye maandishi ikiwa ni pamoja na kuziwasilisha kila baada ya miezi mitatu.” Alisema Mkurugenzi.
Halmashauri iliingia makubaliano na vikundi vya wakulima kuchangia 20% kwa aajili ya matengenezo ya matrekta ambapo Halmashauri imetumia zaidi ya Tsh.36,218,000/= kwa ajili ya kununua vipuri mbalimbali katika kuyakarabati matrekta kwa lengo la kuhamasisha matumizi ya zana bora za kilimo.
Vikundi vilivyokabidhiwa leo matrekta ni pamoja na Kikundi cha Amani Vicoba Misima, umoja wa marafiki Mkata, kikundi cha wakulima Mandera na kikundi cha maziwa Kwamsisi Saccos. Vikundi vyote vimeshukuru kupokea Matrekta hayo na kuahidi kuyatunza vizuri.
Mwenyekiti wa Halmashauri Mh Ramadhani Diliwa akikabidhi mkata kwa moja ya kikundi cha wakulima.
Mkurugenzi Mtendaji mwenye shati nyeupe akipata maelezo machache kutoka kwa mwendeshaji wa trekta aliyeshika usukani.
Mwenyekiti wa Halmashauri Mh. Ramadhani Diliwa akifanya majaribio kwenye moja ya Trekta kabla ya kukabidhi kwa wanavikundi.
Menyekiti wa Halmashauri Mh.Ramadhani Diliwa akifuatiwa na Mkurugenzi Mtendaji William Makufwe wakizungumza wanavikundi.
Baadhi ya Matrekta yaliyotolewa na Uongozi wa Halmashauri.
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa