Maadhimisho ya juma la elimu Mkoa wa Tanga yamefanyika katika Wilaya Handeni tarehe 26-27/04/2019 ambapo siku ya kwanza wadau wa elimu kutoka Wilaya zote za MKoa walitembelea miradi ya elimu ya Wilaya ya Handeni ikiwepo ujenzi wa madarasa, mabweni, Maabara ya sayansi na shamba la shule lenye ekari zaidi ya 20 na baadaye walitembelea mabanda ya maonyesho ya taaluma na kugawa wa zawadi kwa shule zilizofanya vizuri kitaaluma kwa mwaka 2018. Siku ya pili kilifanyika kikao cha tathmini ya maendeleo ya elimu ya Mkoa katika ukumbi wa Makuti uliopo Wilayani hapo.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa miradi ya maendeleo ya elimu Mkuu wa Mkoa wa Tanga ambaye pia alikuwa mgeni rasmi wa maadhimisho hayo Mh. Martin Shigela aliwapongeza viongozi wa Wilaya ya Handeni na wananchi kwa jitihada wanazofanya kuhakikisha maendeleo ya elimu yanasonga mbele na kuahidi kuunga mkono juhudi hizo lakini pia alichangia mifuko ya simenti zaidi ya 300 na matanki ya kuvuna maji.
Wakati huo huo Mh. Shigela aliwaagiza Meneja wa TANESCO na TARURA kutengeneza miundo mbinu ya barabara na umeme katika shule za sekondari Kisaza ambayo inatarajiwa kuanzishwa kidato tano na sita na shule ya sekondari Kitumbi ambayo ni mpya iliyojengwa na wadau wa elimu ili kuwa na mazingira rafiki kwa wanafunzi kusoma hasa shule ya sekondari Kisaza ambayo ni ya bweni.
Mh. Shigela alipotembela shamba la shule ya Sekondari ya Komnyang’anyo lenye ekari zaidi ya 20 iliyopandwa mihogo, mahindi na korosho aliagiza kila Halmashauri kuiga mfano huo ili kuondokana na uhaba wa chakula shuleni kwani upatikanaji wa chakula una uhusiano mkubwa katika ufaulu wa wanafunzi.
Katika kikao cha tatmini ya maendeleo ya elimu ya Mkoa Mh.Shigela alitaka kila ngazi ya uongozi katika kila Halmashauri kufanya tatmini ya elimu kila mara ili kujua changamoto za maendeleo ya elimu mapema na kuzitatua kwa wakati ikiwepo suala la upatikanaji na chakula shuleni, utoro wa wanafunzi, suala la mimba kwa wanafunzi na maendeleo ya taaluma na michezo.
Aidha, Mh. Shigela aliwasihi viongozi wa ngazi ya Halmashauri, Kata na Vijiji kuwa na utamaduni wa kutoa motisha kwa walimu pale wanapoajiriwa katika maeneo yao ili waweze kupenda mazingira ya kazi na kupunguza tatizo la walimu kuhama. Alitoa agizo kwa kila Halmashauri kusimamia suala makambi kwa madarasa ya mitihani ili kuinua kiwango cha ufaulu.
Katibu Tawala Mkoa wa Tanga Mhandisi Zena Said amesema Halmashauri ziwe makini katika utoaji wa takwimu kwani wamekuwa wakikana takwimu kuwa siyo zao hivyo tatmini ya kina ifanyike, wajiridhishe na kusainiwa na Mkurugenzi ndipo ipelekwe ngazi ya mkoa.
Mhandisi Zena alipongeza Halmashauri kuboresha utoaji wa zawadi kwa shule zilizofanya vizuri na kuwasihi kuendelea kutoa hiyo hamasa lakini pia alipongeza suala la wadau wa elimu kuongegezeka katika tatmini ya elimu mwaka huu.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh. Godwin Gondwe alieleza jinsi ambavyo upatikananji wa chakula shuleni ulivyochangia ufaulu wa wanafunzi ambapo alisema mwaka 2016 ufaulu wa darasa la saba kwa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni ulikuwa asilimia 62 lakini walivyoanza kuhimiza utoaji wa chakula shuleni mwaka 2017 ufaulu ukaongezeka na kufikia 73% na mwaka 2018 ukafika 81.6% lakini pia alisema utoro wa rejareja wa wanafunzi ulipungua kwa kiwango kikubwa.
MWISHO.
Pichani ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mh.Martin Shigela akishindilia udongo alipotembela na kuona
ujenzi wa bweni la shule ya Sekondari Kisaza Wilayani Handeni.
Katibu Tawala Mkoa wa Tanga Mhandisi Zena Said
akizungumza katika kikao cha tathmini ya elimu Mkoa wa Tanga.
Mkuu wa Wilaya Handeni Mh.Godwin Gondwe wa tatu kushoto akifafanua jambo kwa Mkuu wa Mkoa.
Wadau wa Elimu wakifuatilia tathmini ya elimu ya Mkoa wa Tanga.
Wadau wa Elimu wakisikiliza jambo kutoka kwa msimamizi wa mradi wa ujenzi Shule ya Sekondari Kisaza
Bw. Mbazi Mfinanga wa kwanza kushoto.
Mwanafunzi aliyefanya vizuri kitaifa kutoka shule ya Tanga ufundi katika mahindano ya ubunifu akipokea zawadi kutoka kwa mgeni rasmi.
Pichani ni Wanafunzi,Shule na Kata zilizofanya vizuri mitihani ya mwaka 2018 zikikabidhiwa zawadi.
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa