Katika kuhakikisha Miradi ya maendeleo inatekelezwa kama ilivyokusudiwa, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya Fedha, Uchumi na Mipango ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Mhe. Mussa Ibrahimu Mwanyumbu ameongoza kamati hiyo iliyoambatana na wataalam kutoka Halmashauri kufanya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Handeni kwa kipindi cha robo ya kwanza kuanzi Julai,2021 hadi Septemba,2021 kwa mwaka wa fedha 2021/2022 kwa lengo la kujiridhisha na utekelezaji wa Miradi hiyo.
Miradi ya Maendeleo iliyokaguliwa katika zira hiyo ni pamoja na mradi wa ujenzi wa jengo la Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Ujenzi na ukarabati wa madarasa shule ya Msingi Amani, Kiundi cha wanawake cha utengenezaji wa Chaki (WALONDI) kilichopo kata ya Kwachaga na mradi wa ujenzi wa kituo cha Afya Sindeni.
Wakati wa ziara hiyo Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Mwanyumbu amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bw. Saitoti Stephen pamoja na wataalam wake kwa kusimamia kikamilifu miradi hiyo kwani utekelezaji wake unaendelea kutekelezwa kama ilivyokusudiwa.
Aidha kamati hiyo ya Fedha Uchumi na Mipango imeishauri Halmashauri kusimamia miradi yote inayotekelezwa kwenye Halmashauri ikamilike kwa wakati kulingana na muda uliopangwa ili wananchi wa Handeni wapate huduma za afya kwenye vituo hivyo vya kutolea huduma za afya.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bi. Rachel Mbelwa aliieleza kamati hiyo ya Fedha, Uchumi na Mipango kuwa ujenzi wa majengo matano ya Hospitali ya Halmashauri zikiwepo majengo ya Maabara, chumba cha kutolea dawa, wodi ya wanawake, wodi ya wanaume pamoja na jengo la chanjo yapo katika hatua za ukamilishaji wa kuweka mifumo ya maji na umeme, ufitishaji wa milango pamoja na rangi sawa na 85% ya utekelezaji wa mradi, Pia amesema ujenzi huo unatumia njia ya mfumo wa (force account).
Pia Bi. Rachel Mbelwa amesema Halmashauri ya Wilaya ya Handeni ilitoa kiasi cha fedha Tsh.25,000,000,000 na bati 141 kwa ajili ya ujenzi wa chumba 1 cha darasa na ofisi 2 za walimu pamoja na ukarabati wa madarasa katika shule ya msingi Amani iliyopo Kata ya Mazingara kutokana na janga la Moto uliounguza vyumba vya madarasa vya shule hiyo na jamii walichangia kiasi cha shilingi milioni moja (1,000,000).
Kaimu Mkurugenzi Bi. Rachel Mbwela alieleza kuwa kwa kipindi cha mwezi septemba, 2021, Halmashauri ya Wilaya ya Handeni kupitia fedha za mapato ya ndani pia ilito kiasi cha Tsh.9,000,000.00 kwa ajili ya kukikopesha kikundi cha wanawake cha kutengeneza Chaki (WALONDI) ambapo Kikundi kimeweza kununua mashine moja mpya ya kutengenezea chaki yenye thamani ya Tsh.3,500,000.00 na kiasi kingine kimetumika kununua vitendea kazi na malighafi zinazotumika katika shughuli za utengenezaji wa chaki.
Naye Afisa Mipango, Takwimu na ufuatiliaji wa Halamshauri ya Wilaya ya Handeni Bi. Amina Said ameishukuru kamati ya Fedha, Uchumi na Mipango kufanya ziara ili kujionea miradi inayotekelezwa kwenye Halmashauri na amesema wamepokea ushauri wa kamati kwa utekelezaji.
Mhe. Mussa Ibrahimu Mwanyumbu, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya Fedha, Uchumi na Mipango ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, mbele akiongoza kamati hiyo kukagua miradi.
Kamati ya Fedha, Uchumi na Mipango Ikikagua miradi.
Wajumbe wakimsikiliza Kaimu Mkurugenzi.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bi. Rachel Mbelwa(aliyevaa kilemba cheusi) akitoa ufafanuzi mbele ya kamati ya Fedha, Uchumi na Mipango.
Afisa Mipango, Takwimu na ufuatiliaji wa Halamshauri ya Wilaya ya Handeni Bi. Amina Said, aliyevaa gauni nyekundu akiongea na Kiundi cha wanawake cha utengenezaji wa Chaki (WALONDI.
Mhandishi Mbazi Mfinanga kulia akitoa maelekezo ya ujenzi mbele ya kamati ya Fedha, Uchumi na Mipango ilipotembelea ujenzi wa hospitali ya Wilaya.
Mashine ya kutengeneza chaki.
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa