Maadhimisho ya juma la elimu kitaifa yatakayofanyika Handeni kwa siku tano kuanzia tarehe 27-31/05/2019 yamefunguliwa rasmi leo katika viwanja vya shule ya msingi Chanika-Handeni na mgeni rasmi ambaye ni mkuu wa Mkoa wa Tanga Mh. Martin Shigela. Maadhimisho hayo yenye kauli mbiu ELIMU BORA NI HAKI YANGU yamefadhiliwa na mtandao elimu Tanzania unaojumuisha mashirika ya kiraia takribani 180 inayojulikana kwa jina la (Ten Met), tarehe 28 -30/05 wadau wa elimu watatembelea shule mbalimbali kuona mafanikio ya shule hizo na changamoto mbalimbali zinazokabili maendeleo ya elimu Handeni na tarehe 31 maadhimisho hayo yatafungwa rasmi.
Akifungua maadhimisho hayo mgeni rasmi Mh. Martin Shigela amesema lengo la maadhimisho haya ni kufanya tathmini ya elimu tulikotoka, tulipo na tunakoenda hasa katika suala kuboresha mazingira ya wanafunzi kusoma na walimu kufundisha kwa weledi.
Amesema lengo lingine ni kuhamasisha wadau ili kuunga mkono jitihada za Mh.Raisi ya kutoa elimu bila malipo kwa kushiriki kikamilifu pale wanapoweza kuchangia hasa kujenga miundo mbinu muhimu kwakuwa elimu bila malipo imefanya idadi ya wanafunzi kuongezeka.
Pia amesisistiza suala la upatikanaji wa chakula shuleni ambapo alisema wanafunzi wakipatiwa chakula kiwango cha ufaulu utaongezeka na kuwasishi wadau hao kuchangia chakula kwa wanafunzi ili waweze kusoma wakiwa hawana njaa “kupatikana kwa chakula imekuwa ni kipaumbele chetu ili kuhakikisha watoto wanasoma wakiwa hawana njaa” alisema.
Aidha, amesema Mkoa wa Tanga kupitia kikao cha wadau wa elimu wamekubaliana kutokomeza ziro kwa kuhakikisha ufaulu unakuwa kuanzia daraja la kwanza hadi la tatu pekee na amesema anaishukuru serikali imeleta walimu na kwamba jitihada zinafanyika ya kuleta vifaa kwa ajili ya maabara ili kuboresha zaidi mazingira ya wanafunzi kufanya vizuri zaidi.
Alitihitimisha kwa kushukuru mtandao wa elimu Tanzania (Ten Met) kwa kufanya maadhimisho hayo na kuwasihi kuendelea kuonyesha ushirikiano huo ili kuhakikisha elimu inasonga mbele, kwa wale wazazi ambao wanakwamisha watoto wasiende shule hasa watoto wa kike Shigela amesema sharia itachukua mkondo wake.
Katibu Tawala Mkoa wa Tanga Mhandisi Zena Said amesema maadhimisho ya juma la elimu kitaifa Handeni haikufanyika kimakosa ni kutokana na juhudi zinazofanyika hasa kuongezeka kwa ufaulu mwaka hadi mwaka. Akitoa taulo kwa watoto wa kike Mhandisi Zena amesema taulo hizo zitasaidia watoto wa kike kujiamini wakiwa kwenye siku zao na ameishukuru shirika la Dorcas kwa kuwasaidia mabinti hao kwani itasaidia kupunguza utoro wa rejareja kwa watoto hao wa kike.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh. Godwin Gondwe akitoa ufafanuzi wa namna ufaulu ulivyoongezeka alisema matokeo mazuri yametokana na Wakurugenzi kuweka makubaliano na Maafisa elimu hadi ngazi ya shule kuhakikisha wastani uliowekwa unafikiwa, pia kuwaweka walimu washauri ili wanafunzi waweze kupeleka matatizo yao yanayorudisha taaluma zao nyuma na kutatuliwa kwa wakati.
Mh.Gondwe amesema pia Handeni tumeanzisha kampeni ya binti shujaa inayolenga mtoto wa kike kujiamini ili kufikia malengo na ndoto zake alizojiwekea kupitia elimu bila malipo na asije akatokea mtu akakatisha ndoto zake hizo kwa kumrubuni na kwamba wasichana hao wakiwa kwenye siku zao wasijisikie vibaya ni hali ya kawaida, Gondwe amesema kupitia shirika la Dorcas wasichana hao waligawia taulo za kike ambazo zinaendana na mazingira yoyote kwa kuwa Taulo hizo ni za vitambaa na zinaweza kutumika mwaka mzima kwa paketi moja ambayo ina taulo nne kitu ambacho kitasaidia kupunguza utoro wa rejareja.
Mwenyekiti wa mtandao wa elimu Tanzania (Ten Met) Bw.Clemence Manganga amesema mtandao wa elimu Tanzania ni mtandao wa kitaifa unaojihusisha na uhamasishaji wa masuala ya utoaji elimu bora hapa nchini. Maadhimisho hayo hufanyika kila mwaka katika eneo husika kwa kuzingatia vigezo maalumu kama ufaulu mzuri, elimu jumuishi wa Wilaya husika na uwepo wa changamoto mbalimbali zinazokabili maendeleo ya elimu.
Pia amesema maadhimisho yamefanyika katika Wilaya ya Handeni kwa lengo la kuhamasisha jamii kuungana na serikali katika suala la utoaji elimu bora kwa watoto kwa kuchangia maendeleo ya elimu kwa kuwa elimu bila malipo haimaanishi jamii kutokuchangia chochote.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bw. William Makufwe amesema ushirikiano kati ya wazazi na viongozi umesaidia kuongeza ufaulu pamoja na vikao vya tathimini ya maendeleo ya elimu kwa kila ngazi ya uongozi wa Halmashauri hasa suala la utoro wa wanafunzi. Motisha kwa walimu kupitia vikao vya mara kwa mara pia imesaidia kuwakumbusha walimu kufanya kazi kwa weledi kwa kufuata kanuni, taratibu na sharia kitu kilichopelekea ufaulu kuongezeka kutoka asilimia 65 mwaka 2016 hadi kufikia 82% mwaka 2018.
Naye mwanafuni Mohamedi Jumanne amesema wanaiomba serikali kuendelea kuboresha miundombinu ili waweze kusoma katika mazingira mazuri na kupata wataalamu watakaofikisha Tanzania katika uchumi wa kati.
MWISHO
Mgeni rasmi Mh.Martini Shigela akitoa neno wakati wa kufungua maadhimisho ya juma la elimu kitaifa
Katibu Tawala Mkoa wa Tanga Mhandisi Zena Said mwenye ushungi mweusi katika akiwa kwenye picha ya pamoja na wanafunzi wa kike baada ya kuwagawia taulo za kike.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh.Godwin Gondwe akifafanua jambo
Mwenyekiti wa Ten Met Bw. Clemence Maganga akizungumza
Mkurugenzi Mtendaji wa Handeni DC Bw. William Makufwe wa kwanza kushoto akisikiliza jambo kutoka kwa msemaji wa banda mojawapo la maonyesho
Mgeni rasmi Mh.Martin Shigela akitembelea mabanda ya maonyesho
wadau malimbali walitembelea na kujionea mabanda ya maonyesho
Burudani mbalimbali kutoka kwa wanafunzi ziliwepo za kimila
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa