Halmashauri ya Wilaya ya Handeni imeungana na wafanyakazi wote duniani kuadhimisha siku ya wafanyakazi ambayo hufanyika kila mwaka ifikapo tarehe 01-05, Kwa mwaka huu siku hiyo imebeba kauli mbiu inayosema “Uunganishaji wa mifuko ya hifadhi ya jamii ulenge kuboresha mafao ya mfanyakazi”, kilele cha maadhimisho hayo yalifanyika jana katika viwanja vya Chanika ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh.Godwin Gondwe.
Katika maadhimisho hayo Katibu wa vyama vya wafanyakazi Ndugu Hamisi Ngomero amesema tunapenda kuikumbusha serikali kupitia maadhimisho haya kuendelea kuboresha maslahi ya watumishi sambamba na maboresho yanayoendelea kufanyika serikalini na katika mifuko ya hifadhi ya jamii na kwamba suala la uhakiki limeshakamilika tangu septemba 2017 hivyo serikali ifungue upandishwaji wa madaraja kwa watumishi wake.
Ameongeza kuwa watumishi wa Handeni wanakumbana na kero ambazo zinarudisha nyuma ari ya utendaji kazi, kero hizo ni madai mbalimbali ya watumishi yaliyokwisha hakikiwa hayajalipwa kama malipo ya uhamisho, masomo, matibabu, kustaafu, likizo, posho ya kujikimu, fedha za kujikimu ajira mpya na stahiki za viongozi na kulazimisha wafanyakazi kulipishwa michango mbalimbali bila hiari yao.
Aidha aliwashukuru waajiri kwa kudumisha mahusiano mazuri baina wafanyakazi, vyama vya wafanyakazi na waajiri, kulipa kwa sehemu madeni ya watumishi, waaijiri kulipa mishahara ya watumishi wao kwa wakati, kuondoa watumishi hewa, kuhimiza mifuko ya hifadhi ya jamii kulipa mafao ya watumishi.
Akizungumza katika maadhimisho hayo Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh. Godwin Gondwe ambaye pia ni mgeni rasmi amesema serikali ya awamu ya tano imehakikisha kuwa wafanyakazi hewa wanaondolewa kwani bila kuondoa wafanayakazi hewa kwanza maana yake watapandishwa vyeo kwa hiyo serikali imeona ni vyema kuhakiki vyeti kabla ya kupandisha madaraja na kwamba serikali imeanza kupandisha madaraja tangu Novemba 2017 baada ya uhakiki huo kukamilika ambapo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni kwa mwaka 2017/2018 itapandisha madaraja wafanyakazi elfu moja mia mbili ishiri na nne (1224), kwa upande wa madeni serikali ilisitisha kulipa ili isiwe inalipa madeni hewa pia ambayo itakuwa hasara kwa serikali kulipa madeni ya watumishi hewa kwa hiyo kwa vile uhakiki umeshakamilika madeni ya watumishi yatalipwa.
Amewataka waajiri kushirikisha kwanza vyama huru vya wafanyakzi kabla ya kuwatoza watumishi michango ya aina yoyote katika ngazi yoyote ile na wafanyakzi waelimishwe kwanza na wao kwa hiari yao ndiyo watatoa hiyo michango na pia amewataka maafisa utumishi kuhakikisha wanasimamia makato ya watumishi yanaenda kwenye mifuko ya hifadhi ya kijamii kwa sababu ni haki yao ya msingi na kuahidi kulisimamia hilo ”nawaahidi nitalisimamia itavyotakiwa” alisema.
Pia aliwapongeza wafanyakazi wote kufanyakazi kwa moyo pamoja na changamoto wanazokutana nazo na amewapongeza waliochaguliwa kuwa wafanyakazi bora kama wawakilishi wa wafanyakazi wote ”lakini nyinyi ni wawakilishi wa wafanyakazi wote maana hamuwezi kuwa wafanyakazi bora wote kwa wakati moja” amesema.
Amehitimisha kwa kuwataka wananchi wote kuwa wavumilivu kutokana na tatizo la mda mrefu la maji Handeni kwani limepata ufumbuzi, amesema waheshimiwa Mbunge wanalifanyia kazi na baada ya wiki mbili tutakuja kutangaza tena kwa wananchi akiwepo na mkandarasi na kwamba makubaliano yatafanyika mbele ya wananchi ili mkandarasi huyo akianza kazi amalize kwa wakati unaotakiwa na pia kazi ifanyike kutokana na thamani ya fedha iliyotolewa amesema ”hilo tunalifanyia kazi pamoja na wabunge na viongozi wote”
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa