Maadhimisho ya siku ya kudhibiti UKIMWI hufanyika kila mwaka ifikapo tarehe 01/12 ambapo kwa mwaka 2019 Halmashauri ya Wilaya ya Handeni iliadhimisha siku hiyo Kata Kwasunga katika viwanja vya shule ya msingi Kwasunga, Maadhimisho hayo yalikuwa na kauli mbiu isemayo “JAMII NI CHAHU YA MABADILIKO-TUUNGANE KUPUNGUZA MAAMBUKIZI YA VVU”.
Akizungumza katika maadhimisho hayo Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bi. Fatuma Kalovya ambaye alikuwa mgeni rasmi alisema lengo la maadhimisho ya siku ya UKIMWI ni kufanya tathmini ya hali na mwelekeo wa udhibiti wa UKIMWI Kitaiafa na kimataifa na Serikali kila mwaka inatoa sera, miongozo, maelekezo mbalimbali na kauli mbiu ili kudhibiti maambukizi mapya na kutokomeza kabisa gonjwa hili la UKIMWI.
Aliongeza kuwa maambikizi ya UKIMWI katika Halmashauri ya Wilaya ya Handeni kwa mwaka 2019 yameongezeka kutoka asilimia 2.8 hadi kufika asilimia 4.0 hivyo alitoa wito kwa wananchi na wadau mbalimbali kushirikiana kwa pamoja ili kutokomeza gonjwa hatari la UKIMWI kwamba kila moja kwa nafasi yake apambane kuhakikisha ugonjwa huu unakwisha kabisa katika Halmashauri ya Handeni.
Bi Kalovya amewasihi wanaume kwenda kupima bila kutegemea majibu kutoka kwa wake zao wanapokwenda kliniki badala yake wapime wote na pia wale waliokwisha pata maambukizi wasiache kutumia dawa maana baadhi yao wamekuwa wakiacha kutumia dawa za kupunguza makali ya virusi vya UKIMWI.
Alihitimisha kwa kuwataka wazazi kuwapeleka watoto shule na amesema kwa wale ambao hawakufanikiwa kuendelea na elimu ya Sekondari wawapeleke kwenye vyuo vya ufundi na kwamba wananchi washirikiane pia kupamabana na mimba na ndoa za utotoni.
Akisoma taarifa ya UKIMWI Kaimu Afisa maendeleo ya jamii Bi. Joyce Daudi amesema upimaji kwa mwaka 2019 umejumuisha ule wa ushawishi kutoka kwa watoa huduma vituoni, hiari, kutoka katika familia zenye wateja na kuwatemebelea wateja manyumbani ambapo jumla ya wateja waliopima ni 45289 kati yao wanaume 20,283 na kati yao waliopata maambukizi ni 290 sawa na asilimia 1.43, wanawake waliopima ni 2,5006 waliopatikana na maambukizi ni 444 sawa na asilimia 1.785 na uwiano mkubwa wa maambukizi uko kwa wanawake wenye umri kati ya miaka 25-49 sawa na asilimia 3.6 na wanaume wa miaka 25-49 katika uwiano wa asilimia 2.40.
Aidha amesema wateja walio katika dawa ni 2,639 sawa na ongezeko la wateja wapya 370. Wateja 58 wamefariki katika kipindi cha januari hadi Oktoba 2019 wakati wateja 307 hawajulikani walipo kutokana na kutokuonekana katika vituo vya huduma na kwamba mikakati ya kuongeza vituo vya kutolea huduma kutoka 6 hadi 10 katika Zahanati za Komsala, Sindeni, Mnzundu na Kwachaga itafanyika pamoja na kutoa dawa mpya ya DTG yenye kufubaza virusi vya UKIMWI kwa kasi zaidi kwa washio na virusi vya UKIMWI ifikapo 2020.
Diwani wa Kata ya Kwasunga Mwingwa H. Ramadhani kwa niaba ya wananchi ameishukuru Halmashauri kwa kufanya maadhimisho hayo katika Kata ya Kwasunga kwani wananchi wamekumbushwa kujihadhari na maambukizi mapya na wale waliokwisha pata maambukizi kutokuacha dawa.
Katika maadhimisho hayo upimaji ulifanyika ambapo jumla ya watu 37 walipima kati ya hao wanaume 31 na wananwake 6 na wote hawakuwa na maambukizi ya virusi vya UKIMWI.
Imeandaliwa na;
Paulina John
Kitengo cha Habari na mawasiliano Handeni DC.
Mgeni rasmi Bi.Fatuma Kalovya akitoa hotuba katika maadhimisho ya siku ya UKIMWI
Kaimu Afisa maendeleo ya jamii Bi. Joyce Daudi akisoma taarifa.
Mratibu wa kudhibiti UKIMWI Bi. Amina Waziri akitoa neno la nasaha.
Diwani wa Kata ya Kwasunga Mh.Mwingwa Ramadhani akitoa neno la shukrani
Wanafunzi wakibeba Mabango yenye jumbe mbalimbali ya kupambana na UKIMWI
Maandamano ya kuelekea uwanja wa maadhimisho
Burudani mbalimbali zilikuwepo
Wananchi walijitokeza kwa wingi katika maadhimisho hayo
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa