MAADHIMISHO YA SIKU YA UKIMWI DUNIANI YAFANA HANDENI
Halmashauri ya Wilaya ya Handeni imeadhimisha siku ya UKIMWI duniani ambayo inaadhimishwa kila mwaka tarehe 01/12 ambapo kwa mwaka yana kauli mbiu inayosema “PIMA, JITAMBUE, ISHI”, kwa ngazi ya Halmashauri maadhimisho hayo yalifanyika katika Kata ya Kwamatuku ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh.Godwin Gondwe.
Katika maadhimisho hayo mgeni rasmi Mh.Godwin Gondwe aliwapongeza wananchi kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho hayo lakini pia amewatoa hofu wananchi kuwa serikali itasimamia huduma za kuzuia maambukizi ya virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na alisema kwamba mtu akipata maambukizi siyo kwamba hana haki ya kupata mtoto hivyo aliwasihi wananchi kuwa wale ambao walipata maambukizi kutumia dawa kwani zipo za kutosha na wamama wajawazito kuwahi kliniki mapema ili waweze kupata huduma mapema.
Pia aliwasihi wanaume kupima kwani takwimu zinaonyesha idadi kubwa ya watu wanaopima ni wanawake na alitaka wanaume kutokuwatumia wake zao kama vipimo vyao kujua kama wamepata maambukizi au la maana akina baba hawapimi wanasubiri mama akiwa mjamzito akienda kupima majibu atakayopewa anaamini na yeye atakuwa hivyo hivyo kitu ambacho siyo sahihi “akina baba tusiwafanye akina mama kuwa ndiyo vipimo vyetu vya kujua kama tuna virusi vya UKIMWI au hatuna” alisema.
Aidha Gondwe alisema huduma ya kupima Virusi vya UKIMWI ni endelevu na ni bure hivyo watu waendelee kupima lakini pia alisema Serikali itaendelea kutoa huduma tembezi ya kupima Virusi vya UKIMWI katika Kata zote 33 za Wilaya ya Handeni ili kuhakikisha kwamba wote wanaohitaji kupima wanapata huduma hiyo katika maeneo yao na kwamba mpaka sasa tuna vituo tembezi 11 na tutaongeza vituo vingine vingi zaidi ili kuwasaidia wananchi wote kwa haraka na kwa wakati.
Aliongeza kwa kuwaeleza wananchi kuwa mapambano haya dhidi ya UKIMWI yaambatane na kupiga vita mimba za utotoni na ndoa za utotoni kwani serikali imetoa elimu bila malipo hivyo aliwasihi wazazi kusimamia suala la kuzuia ndoa na mimba za utotoni ili watoto wetu wasome na asijitokeze mtu akawachezea watoto wetu na pia aliwaeleza wazazi kuwalea katika maadili mazuri “wazazi tushirikiane” alisema.
Alihitimisha kwa kuwataka wananchi kutowanyanyapaa wale waliopima na kugundulika na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI na pia wale waliogundulika wasiache kutumia dawa ya kupunguza makali ya Virusi vya UKIMWI maana imekuwa changamoto kama takwimu inavyoonyesha kuwa idadi ya watu walioandikishwa kutumia dawa ni 2023 na walioacha ni 984 hivyo aliwataka wataalamu kufuatilia na kujua sababu ya wale walioacha kutumia dawa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bw. William Makufwe alisema Kata ya Kwamatuku ni moja ya Kata zilizoathirika na maabukizi makubwa ya Virusi vya UKIMWI kama invyoonyesha kwenye takwimu na idadi ya watu 91 ambao wanaishi na maambukizi hayo na alisema kitaifa maambukizi ni yamefika asilimia 5, Kimkoa maambukizi yamefikia asilimia 5.1 na Kiwilaya Handeni maambukizi yamefikia asilimia 2.8 hivyo alisema leo tuko hapa ili kupata taarifa, kutafakari, tujitathmini na kuchukua hatua ya namna ya kukabiliana na changamoto hii.
Kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Makufwe alitaja maeneo ambayo yana maambukizi makubwa kuliko mengine ambayo ni Mkata, Kabuku na Segera ambapo alisema hii ni kutokana na muingiliano wa watu mbalimbali kutoka sehemu mbalimbali kufuatia shughuli za kiuchumi na kijamii na alisema UKIMWI unapoteza maisha ya watu kwani mpaka sasa Handeni imeshapoteza watu 203 kutokana na ugonjwa huu na pia watoto yatima wanaachwa na kukosa malezi yaliyo bora.
Mwakilishi wa wananchi wa Kata ya Kwamatuku Bw. Benson Nyato akisoma taarifa ya Kata alisema lengo la maadhimisho haya ni kuwakumbuka wenzetu waliotangulia mbele ya haki kutokana na ugonjwa wa UKIMWI, kujikumbusha kauli mbiu mbalimbali za kujikinga na ugonjwa wa UKIMWI, kuzuia maambukizi mapya pamoja na kuzuia unyanyapaa kwa walioathirika, Akitoa takwimu za Kata alisema idadi ya watu wanaoishi na Virusi ya UKIMWI ni 97, wanaotumia dawa ni 51, walioacha dawa ni 43 na waliofariki ni 12.
Nyato alibainisha vyanzo vya maambukizi katika Kata ya Kwamatuku ikiwa ni pamoja na wanandoa kutokuwa waaminifu, momonyoko wa maadili kwa watoto kutokana na wazazi kutokufuatilia mienendo ya watoto wao kwani watoto wamekuwa wakijiamulia kufanya wanachotaka na baadhi ya wazazi kuwaozesha watoto mabinti zao wakiwa kwenye umri mdogo.
Mwisho alisema changamoto inayokumba Kata yao ni pamoja na unyanyapaa wa watu waishio na virusi vya UKIMWI, uhaba wa washauri nasihi, elimu duni kwa wananchi kuhusu UKIMWI na uchache wa vituo vya kutolea huduma.
Mwakilishi wa waishio na virusi vya UKIMWI Kata ya Kwamatuku Bw. Faustini Daudi aliwahimiza watu kupima na kujua afya zao na alisema kama mtu yoyote hajapima na kujua afya yake hayuko salama na kwamba ukipima ukajulika unamaambukizi siyo mwisho wa maisha kwakuwa yeye aligundulika mwaka 2005 lakini hadi leo anaishi kutokana na kuzingatia matumizi ya dawa ya kupunguza makali ya virusi vya UKIMWI hivyo aliwasihi walioathirika kutumia dawa ipasavyo. Pia aliomba kutolewa kwa elimu hasa kwa wanaume ili wajitokeze kupima maana wengi wao hawapimi ukilinganisha na wanawake.
Katika maadhimisho hayo pia waliendesha harambee ya kuchangia ujenzi wa madarasa baada ya Mkurugenzi Mtendaji kuibua suala la uhaba wa madasa uliopo kutokana na ufaulu mkubwa wa wanafunzi wa darasa la saba ambapo Mkuu wa Wilaya Mh. Gondwe alichangia mifuko 20 ya simenti na Mkurugenzi alichangia mifuko 15 na wadau mbalimbali walichanga kiasi cha shilingi 177000.
Baadhi ya mabango ya ujumbe wa UKIMWI
Wanafunzi walitumbuiza katika maadhimisho hayo
Mkurugenzi wa Handeni Bw.William Makufwe akizungumza
Kiongozi wa waishio wa virusi ya UKIMWI Bw.Faustini Daudi akihamasisha watu kupima
Mwenyekiti wa kamati ya kudhibiti UKIMWI Mh. Mustafa Beleko akizungumza
Mwakilishi wa Kata ya Kwamatuku katikati Bw. Benson Nyato akisoma taarifa
Mwenyekiti wa CCM Wilaya Bw. Athumani Malunda akitoa nasaha
Wazee nao hawakurudi nyuma kuadhimisha siku ya UKIMWI duniani
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa