Madiwani na Watendaji wa kata wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni mkoani Tanga,wameshauriwa kuhakikisha wanasimamia vizuri miradi ya maendeleo hususani inayofadhiliwa na mashirika yasiyo ya kiserikali iliyopo kwenye maeneo yao ili iweze kujengwa kwa kiwango kinachohitajika.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Hamlamashuri ya wilaya ya Handeni William Makufwe kwenye kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika Oktoba 16 na kueleza kuwa kuna umuhimu wa viongozi wa Kata kuwa karibu na wafadhili wanaojenga miradi kwenye maeneo yao kwani wao ndio wasimamizi.
Makufwe alisema ofisi ya Mkurugenzi inakuwa na imani kwamba Madiwani na Watendaji wa Kata ndio wasimamizi wakuu wa miradi iliyopo kwenye kata zao hivyo ikitokea miradi haina kiwango ina maana viongozi ngazi ya Kata hawakutimiza wajibu wao.
Aliongeza Kuwa ni kweli Serikali inahitaji kufadhiliwa lakini sio kwa kujengewa miradi ambayo ipo chini ya kiwango hali inayopelekea kuharibika Kwa muda mfupi na kutokufikia malengo yaliyokusudiwa.
" Waheshimiwa mnaopata miradi hii ya ufadhili hakikisheni inaleta tija kwa kusimamia hususani wanaopewa tenda ya kujenga kuepuka madhara yanayoweza kuepukika kwa kuisimamia tu" alisema Makufwe.
Kwaupande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Handeni,Ramadhan Diliwa alisema kuwa kuna baadhi ya miradi ni kweli mapungufu yapo na yamesababishwa na kutokuwepo uangalizi wa karibu na kusisitiza Madiwani kusimamia vyema miradi kwa manufaa ya wananchi wao.
Alitolea mfano eneo la Kata ya Kabuku mjini kuwa kuna madarasa yaliojengwa na wafadhili miaka iliyopita lakini ipo chini ya kiwango hali iliyopelekea wanafunzi kutolewa ndani ya madarasa hayo na kutafutiwa mengine kutokana na kuwa hatarishi kwao.
Aidha Sharifa Abebe diwani kata ya Kwamgwe alisema ni kweli awali hali kama hiyo ilikuwa ikitokea ila kwasasa wanasimamia vizuri miradi iliyopo kwenye maeneo yao ambapo kwake ipo miradi inayofadhiliwa na inajegwa katika ubora unaohitajika kutokana na usimamizi uliopo Kwa kushirikiana na watendaji ngazi ya Kata.
Meza kuu
Diwani wa Kata ya Kwamgwe Mh.Sharifa Abebe akizungumza na wataalamu na madiwani kwenye kikao cha baraza.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni William Makufwe akitioa ushauri kwenye kikao cha Baraza.
wataalamu na Madiwani wakiwa kwenye kikao cha baraza ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya.
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa