Elimu ya kulinda mazao ya misitu imefanyika Halmashauri ya Wilaya ya Handeni kupitia programu ya kuendeleza mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu (FORVAC) iliyoendendeshwa na Idara ya Misitu na maliasili ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni.
Utambulisho huo wa mradi ulifanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni mwishoni mwa wiki iliyopita kwa Kamati ya ulinzi na usalama, waheshimiwa madiwani, wakuu wa Idara, Maafisa Tarafa na Watendaji Kata.
Akitoa maelezo ya mradi, Mratibu wa progaramu Bw. Petro Masolwa alisema lengo la mradi ni kuongeza faida za kiuchumi, kijamii na kimazingira kutokana na usimamizi endelevu wa rasilimali za misitu pamoja na kuongeza ushiriki wa sekta binafsi kwenye sekta ya misitu.
Amesema programu imefanywa kwa ufadhili wa serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na serikali ya Finland ambapo kwa Tanzania mikoa iliyopata ufadhili huo ni Lindi, Tanga, Dodoma na Ruvuma na kwa Mkoa wa Tanga utanufaisha Wilaya ya Handeni katika maeneo ya Mazingara, Kwedikabu, Kwamsundi, Kitumbi na Gole na Wilaya ya Kilindi.
Aidha, amesema programu itawajengea uwezo serikali za vijiji na kamati za maliasili, Halmashauri, Wizara na wadau mbalimbali kwenye usimamizi shirikishi wa rasilimali za misitu pia progrmu itwezesha kuingizwa kwa mafunzo/elimu ya uendelezaji wa mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu na masoko katika mitaala ya vyuo husika.
Pia amesema programu itawezesha uboreshaji wa huduma za ugani na mawasiliano katika sekta ya misitu na kuanzisha ufuatiliaji na usimamizi wa taarifa sambamba na uboreshaji wa sera na sheria za misitu, utawala na biashara ya mazao mbao zilizovunwa kwenye misitu iliyohalalishwa kuvunwa.
Alihitimisha kwa kuwataka wadau kusimamia misitu hiyo ili kuleta matokeo chanya yatakayoendeleza ufadhili kwasababu Wilaya ambazo zitafanya vizuri ndizo zitakazoongezewa ufadhili na zile ambazo zitafanya vibaya hazitaletewa ufadhili huo hata kama zilikuwepo kwenye programu.
Kwa upande wake Afisa misitu Bw. Elinihaki Mdee akijibu maswali ya wadau kuhusu uharibifu wa misitu na mipaka ya kazi kati ya misitu inayosimamiwa na vijiji na misitu inayosimamiwa na Wakala wa misitu alisema maafisa misitu wa Halmashauri na Wakala wa misitu wanashirikiana kusimamia misitu yote iliyoko ndani ya Wilaya tofauti ni katika mipaka ya kiutawala kuwa msitu fulani ni wa serikali kuu na mwingine ni wa Halmashauri au wa kijiji. Kwa upande wa uharibifu wa misitu alisema hakuna namna yoyote yakuvuna msitu bila mpango wa uvunaji wa rasilimali ya misitu iliyopo hivyo uvunaji unafanyika kulingana na kiasi kitakachostahili kuvunwa kwa mwaka na mtu akifanya zaidi ya kiasi hicho basi ni kiume cha sheria.
Bw. Mdee alitoa wito kwa wadau kushirikiana katika kusimamia misitu bila kutegemea maafisa misitu pekee kwasababu wananchi ndiyo ambao wapo katika maeneo ya misitu hivyo taarifa zitolewe pale ambapo kuna uharibifu au uvamizi ili kuchukua hatua kwa wakati.
MWISHO.
Mratibu wa programu Bw. Petro Masolwa akitoa mafunzo.
Afisa misitu Bw.Elinihaki Mdee akijibu maswali ya wadau
Wadau wakifuatilia mafunzo.
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa