Wawezeshaji wa Mpango wa (TASAF) wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni watafanyiwa mafunzo ya siku tano ambapo watafanyiwa mafunzo ya nadharia na vitendo kuhusu utaratibu wa uundaji wa vikundi vya kuweka akiba kwa walengwa wa mpango wa kunusuru Kaya maskini awamu ya tatu.
Mafunzo hayo yalifunguliwa jana tarehe 09-04-2018 na Mgeni rasmi Bw.Willam Makufwe ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni katika ukumbi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC). Mgeni rasmi aliwashukuru viongozi wa TASAF Makao makuu kwa kuleta programu hiyo katika Halmashauri ya Wilaya ya Handeni kwani watanusuru Kaya maskini kutoka katika hali waliyonayo kwenda hatua nyingine kiuchumi kwa sababu jamii ikipata elimu ya kuweka akiba itajihusisha na ujasiriamali ikiwemo kilimo,ufugaji na biashara mbalimbali itakayowaingizia kipato.Pia aliwataka wawezeshaji wa kunusuru Kaya Maskini kutumia utaalamu wao ili kuhakikisha wanaelimisha jamii na mwisho wa siku zoezi linafanikiwa kwa kiwango kinachotakiwa.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa TASAF makao makuu ambaye pia ni Afisa Mawasiliano TASAF Makao makuu Bw. Estom Sanga Wakati wa ufunguzi huo aliwaeleza wawezeshwaji kuwa programu hii ya kukuza uchumi wa Kaya maskini inahusu utekelezaji wa shughuli mbalimbali ambazo zitasaidia ukuaji wa uchumi wa Kaya. Shughuli hizo zinahusu uhamasishaji wa walengwa kuunda vikundi vya kuweka akiba ambazo zitatumika na walengwa kama mitaji ya kuanzisha au kupanua shughuli zao za kiuchumi.Aidha, walengwa wanatarajia kupata ujuzi utakaowasaidia kutekeleza miradi au biashara zao kwa faida na endelevu hivyo kuongeza kipato chao na pia kupunguza umaskini.
Aliongeza kuwa uanzishaji wa program hii utalazimu kuwa na wawezeshaji wengi wenye ujuzi wa kuwaelezea walengwa jinsi shughuli za program hii zitakavyofanyika katika nyakati tofauti na utaratibu wa uendeshaji wa mafunzo utakuwa jumuishi ili kuwezesha walengwa kuwa na shughuli zenye tija hivyo njia ya ushirikishaji zitatumika katika ngazi ya jamii kwani lengo ni kuiwezesha Kaya kumudu mahitaji yake na kupata ziada ili kujikwamua kiuchumi na hivyo kuwatoa walengwa kwenye umaskini.
Pia alisema utekelezaji wa mpango wa kunusuru Kaya maskini unaendelea vizuri kwani hadi sasa unafanyika katika Vijiji, Mitaa na Shehia 9809 kwenye maeneo 161 ya Mamlaka za utekelezaji ikihusisha Tanzania Bara na Visiwani(Unguja,Pemba na Zanzibar). Idadi ya Kaya maskini zilizotambuliwa ni 1,369,649 na Kaya zilizoandikishwa kwenye mpango na zinazolipwa ni 1,106,071 na utekelezaji wa miradi ya kutoa ajira za muda imeanza katika Halmasahuri 44 hivyo mafunzo haya ni sehemu ya mkakati endelevu wa kuondokana na umaskini kwa kuwezesha Kaya hizo hizo za walengwa kuweka akiba na kufanya shughuli za kiuchumi
Aidha,aliongeza kuwa utekelezaji wa programu ya kukuza uchumi wa Kaya ulishaanza kutekelezwa katika Mamlaka nane za maeneo ya utekelezaji ambazo ni Chamwino, Bagamoyo, Kibaha, Mtwara MC, Lindi MC,Unguja na Pemba na jumla ya vikundi 5182 vimeundwa na mafunzo ya awali ya vikundi hivyo yanaendelea, Walengwa wameonyesha ari kubwa ya kuanza kuweka akiba. Changamoto iliyopo ni jinsi ya kuvifuatilia vikundi na kuvipa taaluma ya uendelevu ambayo inatarajiwa kufanywa na ninyi wakufunzi na ndiyo sababu tunapenda wakufunzi watoke ngazi ya Kata ili kurahisisha ufuatiliaji kwani bila kufanya hivyo ukuaji wa vikundi utakuwa ni changamoto.
Kwa upande wa mratibu wa TASAF wa halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bi Amina Luhizo alisema kuwa program hii itasadia kuweka Kaya maskini kwenye uchumi wa kati kutokana na kuwa vikundi vikiundwa na vikaweka akiba vitapata fedha za ziada ambazo zitawasaidia kufanya shughuli mbalimbali za ujasiriamali zitakazowaongezea kipato.
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa