Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango afanya ziara ya siku mbili mkoni Tanga, akiwa mkoani Tanga atafungua mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Mashirika ya Umma, Taasisi na Makampuni binafsi Tanzania (SHIMMUTA) pamoja na kuzindua kiwanda cha Yogi Polypack cha kutengeneza mifuko kilichopo Tanga.
Akiwashuru kwa mapokezi na kuwasalimia wananchi wa Handeni Mhe. Mpango metoa siku saba kwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa kushirikiana na Wizara ya Madini kuhakikisha wanatatua changamoto inayokwamisha ujenzi wa barabara ya Pangani mpaka Bagamoyo ambayo imekwama kutokana na eneo la jiwe la kuchimba kokoto leseni yake ya uchimbaji kupewa mtu mwingine tofauti na mkandarasi husika.
Pia Makamu wa Rais amewaagiza viongozi wa Mkoa wa Tanga kuhakikisha wanafanya vikao na wafugaji kwa lengo la kuwapa elimu ya sharia na taratibu za nchi ili kuondoa migogoro inayosababishwa na wafugaji kulisha mifugo kwenye mashamba ya wakulima na kuwaasa wakulima kutochukuwa sharia mkononi baina yao na wafugaji.
Makamu wa Rais amewasihi wananchi wa Handeni kutunza mazingira ikiwemo upandaji wa miti kwenye vyanzo vya maji ili kuepuka changamoto za ukame zinazojitokeza hivi sasa.
Aidha Mhe. Mpango amewaasa wazazi na walezi Wilayani Handeni kuhakikisha wanatumia vyema fursa ya elimu inayotolewa bila malipo na Serikali kwa kuwapeleka watoto wao kupata elimu kwa maendeleo ya Handeni na Taifa kwa ujumla.
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa