Mashindano ya UCHUMI CUP Wilayani Handeni yamemalizika jana katika viwanja vya Kigoda na timu ya Vibaoni FC ikiibuka na ushindi wa magoli 3 kwa 0 dhidi ya Kurugenzi FC, mashindano yaliyoasisiwa na Mkuu wa Wilaya ya Handeni yenye kauli mbiu ya “Kipaji changu Mtaji wangu”
Akizungumza kwenye fainali hizo Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh. Godwin Gondwe alisema kuwa mbali na kupeana taarifa mbali mbali za fursa zilizopo Handeni UCHUMI CUP imelenga kuinua vipaji na uchumi wa vijana , na kuwapongeza washindi na timu zote zilizoshiriki mashindano hayo kuanzia ngazi ya Tarafa hadi kufikia kwenye fainali.
Mh. Gondwe alisema kuwa msimu wa kilimo umezinduliwa rasmi kwenye fainali hizo kwani vijana wamepata uelewa na kuwahamsisha kulima mazao mbalimbali kama vile mahindi, korosho, mihogo na katani huku akiwataka vijana kuwa na walau na ekari ya Muhogo hususani katika kipindi hiki ambapo zao la muhogo linastawi vizuri.
“Ardhi ya Handeni inarutuba na mazao mengi yanastawi vizuri, vijana mtumie fursa hii kujikuza kiuchumi kwa kulima mazao mbalimbali , uzuri zao la muhogo linastawi sana”Alisema Mh. Gondwe
Aliongeza kuwa Ilani ya Chama inatekelezwa kwani michezo ni moja ya Ilani hivyo Uchumi Cup inatekeleza fursa aliyotolewa na Rais wa Jamuhuriu ya Muungano wa Tanzania Mh.John Pombe Magufuli kwa kusapoti viongozi wa Mkoa wa Tanga na kuahidi kufanyika kwa michezo kila mara muda utakapopatikana.
Aidha amepongeza timu ya mpira wa miguu kupanda daraja na kuingia kucheza ligi kuu msimu ujao Coastal Union kwa kuwakilisha vyema Mkoa wa Tanga na kusema Uchumi Cup ipo tayari kuwasapoti na kuwapa nafasi ya kuwachangia katika shughuli mbalimbali ikiwemo kambi pindi itakapohitajika.
Alisema kuwa vipaji vya mpira wa pete na miguu vimeonekana na vijana wameonesha uwezo wao, sasa imetengenezwa timu itakayokuwa inawakilisha Wilaya ya Handeni na itatafutiwa timu zilizoingia ligi kuu ya Tanzania zije kucheza na Handeni kwa lengo la kupata msingi mzuri utakaowezesha timu ya Handeni kusonga mbele.
Katika Mashindano ya Uchumi Cup mshindi wa kwanza Vibaoni Fc ametoka na zawadi za Jezi seti moja,TSh.300,000/=, kikombe cha dhahabu , mipira 3 na medali huku wafungaji wakiwa ni Hassani Ngilo aliyefunga magoli 2 na Shabani Mswagala bao 1. Mshindi wa Pili Kurugenzi FC amepata mipira 2, seti ya jezi na Tsh.200,000/=, huku mshindi wa tatu Mtazamo FC akitoka na kitita cha Tsh.100,000/=, medali za shaba na jezi. Na mshindi wa nne aliyepata mpira 1 ametoka Umoja FC kutoka Segera huku washindi wote ngazi ya Tarafa wakipewa zawadi ya jezi seti 1.
Kwaupande wa mpira wa pete mshindi wa kwanza ni Wanawake live waliowatoa kivesa Sekondari kwa bao 44 kwa 14, wamepata zawadi ya medali, jezi, kikombe cha dhahabu, mipira 3 na fedha kiasi cha Tsh.300,000/= huku mchezaji bora akiwa ni Nusura Almasi aliyefunga magoli 140 tangu mashindano kuanza. Mshindi wa Pili ni Kivesa Sekondari wamepata mipira 2, jezi na fedha kiasi cha Tsh.200,000/=. Mshindi wa tatu Kabuku Quens walipata mipira 2 na Tsh.100,000/=.
Mashindano hayo ya fainali yalimalizika salama huku yakishirikisha Wilaya nzima , wananchi walihamsika ambapo viongozi mbalimbali wa ngazi ya Wilaya na Mkoa walishiriki huku mchezaji bora wa mpira wa miguu , Nguruko Machele kutoka Kurugenzi FC akipata zawadi ya kombe.
Shamra shamra za wachezaji wa mpira wa pete kabuku quens
Kaptaini wa timu ya Kurugenzi FC iliyoshika nafasi ya pili akikabidhiwa zawadi za mipira na Mbunge wa jimbo la Handeni Mji Mh. Omary Kigoda jana.
Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Tanga Bi. Aisha Kigoda akikabidhi zawadi kwa mwwalimu wa timu ya mpira wa Pete Kivesa sekondary kwa kuwa washindi wa pili.
Mchuano kati ya Wanawake live na Kivesa Sekondari ukiendelea.
Kurugenzi FC wakipambana na Vibaoni FC
Mwenyekiti wa CHANETA Wilaya Bi.Amina Kigoda akikabidhi zawadi kwa Mfungaji bora wa mpira wa pete Nusura Almasi, katikati ni mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh.Godwin Gondwe.
Mwenyekiti wa chama cha mpira wa miguu Wilaya Bw.Essau Ngadala akikabidhi zawadi ya kombe la dhahabu kwa mchezaji bora wa mpira wa miguu Nguruko Machele kutokea Kurugenzi FC
Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Mji Bw Thomas Mzinga akikabidhi zawadi kwa washindi wa Uchumi Cup, kaptaini wa vibaoni akipokea.
Mkurugenzi Halmashuri ya Wiaya ya Handeni Bw.William Makufwe akikabidhi Kombe la dhahabu kwa washindi wa mpira wa pete wanawake live, pembeni ni Mkuu wa Wilaya Mh. Godwin Gondwe.
Viongozi wakifatilia kwa makini mechi jana kwenye viwanja vya kigoda.
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa