Mtendaji Kata ya Sindeni Bi. Amina Sakwalu pamoja na Afisa Elimu wa Kata hiyo Mwl. Simon Charles wamepata zawadi ya fedha ya kiasi cha Tsh. 50,000 kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Handeni Bw. Saitoti Z. Stephen kwa kufanya vizuri kwenye zoezi la uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la awali na darasa la kwanza kwa Mwaka wa masomo 2023 ambapo wameandikisha asilimia 120 ya matarajio waliojipangia.
Zawadi na pongezi hizo zimetolewa leo kwenye kikao kazi alichofanya Mkurugenzi Mtendaji kilichowashirikisha Wakuu wa Idara na Vitengo wa Halmashauri pamoja na Watendaji wa Kata na Maafisa Elimu wa Kata zote 21 kwa lengo la kupokea taarifa ya zoezi la uandikishaji kwa wanafunzi wa darasa la Awali na darasa la Kwanza.
Kwenye kikao hiko Mkurugenzi Mtendaji ametoa malekezo kwa Kata zote kuwa mpaka kufikia tarehe 29/12/2022 ziwe zimefikia asilimia mia moja za uandikishaji huo.
Pia Bw. Saitoti Stephen amefuta likizo zote za maafisa hao na walioko likizo warudi mara moja ili washirikiane mpaka zoezi la uandikishaji litakapokamilika na Watendaji ambao hawatafikia asilimia mia moja ya uandikishaji atawapunguzia majukumu ya kazi yao au kuwapangia kazi nyingine.
Aidha ameagiza kwenda kuhamasisha zoezi zima la uandikishaji kwa jamii kwani elimu ni bure na kusisitiza kuwa siku ya kufungua shule masomo yaanze mara moja kwa wanafunzi waliopo na walioandikishwa.
Afisa Elimu ya Msingi Bi. Rehema Nyoka amemshukuru Mkurugenzi kwa kufanya kikao kazi hiko na kuwataka maafisa hao kwenda kushirikiana na viongozi wa vijiji na vitongoiji ili wanafunzi waweze kupatikana kwa wingi kwa ajili ya Mwaka wa masomo 2023.
Mkurugenzi Mtendaji Bw. Saitoti Z.Stephan (katikati) akiongoza kikao hiko.
Afisa Elimu Msingi Bi. Rehema Nyoka(kushoto) akiongea kwenye kikao hiko
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa