Wananchi Wilayani Handeni wametakiwa kuchukua Tahadhari ya Magonjwa ya mlipuko na madhira yanayoweza kujitokeza kwenye kipindi hiki cha mvua.
Tahadhari hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauriya Wilaya ya Handeni Bw. William Makufwe ofisini kwake jana alipokuwa akizungumza na wandishi wa Habari.
Mkurugenzi Mtendaji alisema kuwa mvua zinanyesha kwa mfululizo madimbwi na mabwawa yanajaa maji na wananchi wengi wanatumia maji hayo kwa kunywa bila kuyatibu hali inayoweza kupelekea magonjwa ya mlipuko hasa ukizingtia Halmashauri ya Wilaya ya Handeni inatatizo la upatikanaji wa maji safi.
“ Wananchi wanao wajibu wa kulinda afya zao kwa kuwa makini na maji wanayotumia kwa kunywa na kupikia hasa ya kwenye mabwawa na madimbwi kwani maji hayo mara nyingi huambatana na kubeba uchafu unaopelekwa kwenye vyanzo vyetu vya maji” Alisema Makufwe.
Aidha, alitaka tahadhari hizo kuchukuliwa kwenye maeneo ya shule kwa kuzingatia ubora wa madarsa hasa yale yaliyojengwa kwa udongo kuepuka madhira ya kudondokea wanafunzi, ni muhimu kuchukua tahadhari ya kuwahamisha mapema.
Aliwataka wazazi kuwa makini na watoto wao kwenye kipindi hiki cha mvua, Mito mingi inajaa na watoto huwa wanavuka maranyingine kwenda shule. Watoto waelekezwe maeneo salama ya kupita na kama kuna uhitaji wa watoto kuvushwa basi wazazi/walezi wawe tayari kuwasaidia watoto.
Aliwaasa wanachi waliojenga mabondeni, kwenye mikondo ya maji na sehemu hatarishi Mkurugenzi Mtendaji aliwataka kuchukua tahadhari ama kuhama kabisa kwenye maeneo hayo na kutoa rai kwa wananchi kuacha kujenga nyumba kwenye maeneo hatarishi.
Wakati huohuo aliwataka wakulima kutumia vizuri mvua hizi zinazoendelea kunyesha kwa kulima na kupanda mazao yale yanayokomaa kwa muda mfupi na muda mrefu hasa kwa kuzingatia kipindi cha miaka miwili iliyopita hakukuwa namvua za kutosha.
“Handeni hatuna zao la biashara zaidi ya mazao ya chakula kama mahindi, wananchi wote wa Handeni na ambao mko nje ya Handeni karibuni mpande mikorosho ikiwa ni mtu mmoja mmoja au kikundi, ardhi ya handeni inaruhusu na tupo kwenye kampeni ya kuhamasisha upandaji wa zao la biashara la korosho” Alisema Mkufwe.
Aliongeza kuwa korosho ikilimwa itaongeza na kuimarisha uchumi wa Handeni, lengo likiwa ni kusaidia kuelimisha jamii ya Handeni kwamba yapo mazao zaidi ya Mahindi ambayo yanaweza kuinua uchumi wa Halmashauri yetu.
Kwa upande wa agizo la Mkuu wa Mkoa la kupiga marufuku uuzaji wa mahindi mabichi Mkurugenzi Mtendaji amesema atahakikisha anasimamia kwa kushirikiana na Maafisa watendaji Kata na Vijiji kwani Halmashauri bado haijatambua kama kutakuwepo na mahindi ya ziada baada ya mavuno licha ya mvua ambazo bado zinaendelea kunyesha. Lengo ni kudhibiti upungufu wa chakula unaoweza kujitokeza hapo baadae na hatua za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayekwenda kinyume na tamko hilo.
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa