Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh. Godwin Gondwe amezindua rasmi zoezi la Utambuzi,Usajili na Ufuatiliaji wa mifugo na kuwataka wafugaji kufuat sheria za kuingia mifugo mipya kwenye maeneo yao ili kubaini idadi halisi ya mifugo kuligana na rasilimali zinazohitajika kwenye uendelezaji wa mifugo.
Akizungumza na wafugaji kwenye uzinduzi wa zoezi hilo Mkuu wa Wilaya amewaeleza kuwa, sheria zimewekwa ili kuwatumikia wananchi na kwamba kwa kuitikia wito wa kupiga chapa ya utambuzi wa mifugo yao ni kuunga mkono Serikali kwa sababu zoezi hilo limelenga zaidi kuwalinda wafugaji.
Aliongeza kuwa kwa kupiga chapa mifugo kutasaidia kwenye suala zima la ulinzi na usalama kwenye Wilaya ya Handeni kwa kutambua mifugo ya kila mtu na kjiji itakayosajiliwa hivyo kuwa na ulinzi mzuri.
Amesema kuwa zoezi hili la utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo lina faida nyingi ikiwemo kudhibiti wizi wa mifugo, kuzuia na kudhibiti kuenea kwa magonjwa ya mifugo kwani hakuna mfugo utakao ruhusiwa kuingia Wilayani Handeni pasipo kupimwa na kuboresha koosafu za mifugo hali itakayopelekea kuwa na begu nzuri za mifugo hatimaye kuongeza fursa ya soko la uhakika kutokana na ubora wa mifugo.
Aidha aliwataka wafugaji na viongozi ngazi ya Vijiji kuwa makini na mifugo inayoingia kwenye maeneo yao kwa kuangalia uwiano wa mifugo waliyonayo na malisho, kwani kwa kukaribisha wafugaji wengine kiholela kutawapelekea wazawa kukosa maeneo ya malisho na kwamba wasiwakaribishe bila kujiridhisha uwepo wa maeneo ya kutosha kwa kupitisha barua ya mwombaji kwa Uongozi wa Vijiji, baraza la ardhi na mikutano mikuu ya wananchi.
“ lazima mtambue na kusimamia sheria Na.12 ya malisho na maliasili ili muweze kulinda rasilimali za wanyama, idadi ya mifugo lazima iwe na uwiano na malisho, kuwa na mifugo mingi mtakosa malisho Handeni na mkienda kuomba Halmashauri nyingine mtakosa”Alisema Mkuu wa Wilaya.
Aliongeza kuwa akitokea mtu yeyote ambaye wananchi hawamfahamu ataingiza mifugo kwenye maeneo yao bila kufuata sheria watoe taarifa haraka iwezekanavyo kwani upigaji chapa ni muhimu na viongozi wapo kuhakikisha wanasimamia haki za wafugaji.
Kwaupande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bw. William Makufwe alisema kuwa kwa kufanya zoezi la upigaji chapa wa mifugo ni kutekeleza agizo la Serikali ambalo liliwataka Halmashauri kusimamia na kuwataka wafugaji kutoa ushirikiano wao ili kufanikisha zoezi hilo kama ilivyokusudiwa.
Mkurugenzi Alisema kuwa mbali na kuitikia agizo la Serikali lakini zoezi hilo litasaidia kupunguza migogoro baina ya wakulima na wafugaji,kuepusha muingiliano wa mifugo baina ya Vijiji na Wilaya na kubainisha kuwa zoezi hilo ni endelevu na hadi kufikia mwezi Desemba Kata 21 na Vijiji vyote 91 viwe vimefikiwa.
“Ng’ombe ambazo zitakuwa hazijapigwa chapa na kuingia kwenye maeneo ambayo hayaruhusiwi watapigwa mnada, naomba tusifike huko, leteni mifugo yenu ipigwe chapa baada ya Desemba mifugo yote ambayo haijapigwa chapa itapigwa faini, sitaki tufike huko” alisema Mkurugenzi
Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Inatarajia kupiga chapa mifugo zaidi ya lakimoja na elfu thelathini(130,000) ambapo uzinduzi umefanyika kwenye Vijiji vya Sua na Mazingara na Ng’ombe zaidi ya 932 wamepigwa chapa.
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa