Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mhe. Godwin Gondwe amefanya kikao kazi na maafisa elimu wa sekondari na msingi, maafisa elimu kata pamoja na wakuu wa shule wa sekondari na msingi zote za Halmashauri ya Handeni lengo ni kupanga malengo ya ufaulu wa wanafunzi mara baada ya kuisha kwa ugonjwa wa Korona na kufanaya tathmini ya namna walivyokuwa wanafundisha wakati wa likizo.
Mara baada ya kufungua kikao hicho Mhe. Godwin Gondwe alimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Handeni kwa kuwajali watumishi hususani kusimamia maslahi ya walimu pia aliwapongeza walimu kwa kufanya kazi kwa ushirikiano na kuiwezesha Halmashauri ya Handeni na kupanda kielimu mwaka hadi mwaka na matokeo ya darasa la saba mwaka 2019 yamepanda hadi kufikia 89% na kuwa Halmashauri ya 3 kati ya 11za kielimu zilizopo mkoa wa Tanga na kusema kuwa umoja wetu ndiyo ushindi wetu.
Kwakuhitimisha Mhe. Godwin Gondwe amewaagiza maafisa elimu wa sekondari na msingi kusimamia nidhamu za walimu na kuwahi kazini na kuhakikisha kuwepo kwa vifaa vya kujikinga na ugonjwa wa Korona kama vile maji tiririka na sabuni.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bw. William Makufwe alimshukuru mkuu wa wilaya kwa kufanya kikao kazi na walimu na kuwapa maelekezo baada ya likizo ya korona.
Bw. William Makufwe amemueleza mkuu wa wilaya ya Handeni kuwa mwaka huu Handeni itakuwa ya kwanza kimkoa kwa matokeo ya mitihani ya Taifa na amewaeleza walimu kuwa malengo ya ufaulu yawe pale pale kwa 100% kwa darasa la nne, darasa la saba na kidato cha pili na 90% kwa kidato cha nne.
Pia amewakumbusha maafisa elimu kusimamia nidhamu za walimu na ruhusa zote za walimu zitatolewa na ofisi ya mkurugenzi ili kudhibiti utoro wa walimu.
Kwakuhitimisha Mkurugenzi Mtendaji wa Handeni amesema kila mmoja awajibike kwa nafasi yake kusimamia na kufuatilia maagizo yote na ametoa lita 20 za mafuta kwa kila afisa elimu kata kwa kata zote za Halmshauri ya Handeni ili kwenda kukagua maagizo kama yanatekelezwa ipasavyo.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mhe. Godwin Gondwe aliyesimama akiongea na walimu wa Halmashauri ya Handeni.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bw. William Makufwe aliyesimama akisisitiza jambo kwenye kikao hicho.
Wakuu wa shule za sekondari na za msingi wakimsikiliza mkuu wa Wilaya ya Handeni.
Baadhi ya wakuu wa shule za sekondari na za msingi wa Halmashauri ya Handeni wakipokea maelekezo kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Handeni
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa