Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh.Godwin Gondwe amefunga rasmi mafunzo ya jeshi la akiba jana katika viwanja vya Kata Kabuku ndani Wilayani Handeni Mkoani Tanga ambapo mafunzo hayo yalianza mwezi wa 01/08/2019.
Akifunga mafunzo hayo Mh. Gondwe ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo alizitaka Taasisi za Serikali na Makampuni mbalimbali yaliyoko ndani ya Wilaya ya Handeni kuhakikisha wanawaajiri watu waliopitia jeshi la akiba na amesema ni marufuku Taasisi na Makampuni hayo kuajiri watu ambao hawajapitia jeshi la akiba.
Aidha ameipongeza Kampuni ya katani (KWALAGURU ESTATE) kwa kuwachukua jeshi la akiba 54 kati ya 60 waliohitimu jana na kuwataka Maafisa Tarafa kufuatilia makampuni mengine ili wale sita waliobaki waweze kupata ajira na amesema haiwezekani wengine wanapitia mafunzo ya jeshi la akiba lakini wengine ambao hawajapitia mafunzo hayo wanapatiwa ajira katika makampuni na Taasisi za Serikali.
Alihitimisha kwa kuwasihi wananchi kujiunga bima ya matibabu iliyoboreshwa (ICHF) shilingi 30,000 kwa watu 6 ambao watatibiwa mwaka mzima katika Hospitali za Wilaya, Vituo vya afya na Zahanati zote ndani ya Mkoa wa Tanga
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bw. William Makufwe alimuahidi mgeni rasmi kuwaajiri watu waliopitia jeshi la akiba katika Ofisi zote za Halmashauri ya Wilaya ya Handeni. Pia alitumia nafasi hiyo kuwasihi wananchi kujikita katika shughuli za kilimo ikwepo Mihogo na Korosho ili kuondokana na njaa na umaskini.
Meja Donatus Tumaini Mashauri akisoma taarifa amesema kundi la 49 ilianza mafunzo ya awali tarehe 1/08/2019 na kufunguliwa rasmi mwezi wa 9/2019 ambapo walikuwa wanafunzi 71 kati ya hao wakike 14 na wakiume 57 lakini hadi kufikia tarehe ya kuhitimu walibaki 60 ambapo 9 walishindwa mafunzo na 2 walifukuzwa kutokana na utovu wa nidhamu.
Aidha amesema lengo la mafunzo ya jeshi la akiba ni kuwaanda kwaajili kazi ya ulinzi na usalama ya Taifa bila woga, kushiriki katika mapambana na maafa yanapotokea, kushiriki katika gwaride na kushiriki katika ulinzi wa wananchi na mali zao pamoja na mipaka ya nchi.
Wahitimu wa mafunzo ya jeshi la akiba Elizabeth Paskali na Emanueli Masongo wamesema mafunzo yalikuwa magumu kiasi kwamba wengine walishindwa kumaliza lakini wanashuru wao kumaliza salama hivyo wanawaomba viongozi mbalimbali kuwaajiri jeshi la akiba katika Taasisi zao.
Imeandaliwa na;
Paulina John.
Kitengo cha Habari na mawasiliano Handeni DC
Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh.Godwin Gondwe akitoa hotuba kabla ya kufunga mafunzo ya jeshi la akiba
Meja Donatus Tumaini Mashauri akisoma taarifa ya mafunzo ya jeshi la akiba kundi la 49
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bw.William Makufwe akizungumza
Jeshi la akiba wakiwa kwenye gwaride wakimwonyesha mgeni ukakamavu wao
Jeshi la akiba kundi la 49 wakila kiapo
Wananchi walijitokeza kushuhudia ufungaji wa mafunzo ya jeshi la akiba kundi la 49
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa