Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh. Godwin Gondwe amempa siku 90 mwekezaji anayejulikana kama Hiragro LTD kufikisha hati ya kumiliki ardhi lenye ukubwa wa ekari1000 na kumpiga marufuku kufanya shughuli zozote mpaka atakapokamilisha taratibu za umiliki halali wa ardhi,kinyume na hapo ardhi itarudishwa kwa wanakijiji kwa kushindwa kuendeleza eneo hilo kama walivyokubaliana.
Kauli hiyo ameitoa leo alipokuwa kwenye kikao baina ya wanakijiji wa Kijiji cha Mkomba kilichopo Kata ya Kwachaga Wilayani Handeni na wawekezaji wa Hiragro LTD ambao waliuziwa eneo hilo mwaka 2013, baada ya wawekezaji kukiuka makubaliano na kuanza kukata miti kwa kuvuna mbao,magogo na kuchoma mikaa kinyume cha makaubaliano.
Mkuu wa Wilaya ameeleza kuwa ndani ya siku 90 kama hatafikisha hati miliki kwenye ofisi ya Mkurugenzi , ardhi hiyo itafanyiwa utaratibu kurudishwa kwa Mkurugenizi Mtendaji ili wapangie mpango bora wa matumizi ya ardhi kwa manufaa ya Kata na Kijiji kwa ujumla.
Mkuu wa Wilaya aliwaeleza wanakijiji na viongozi kuwa walifanya makosa kuuza ardhi yenye ukubwa wa ekari 1000 kinyume cha taratibu, hivyo katika kumdai mwekezaji huyo anayedaiwa kuingia kwenye mashamba na makazi ya wanakijiji wanapaswa kufuata taratibu ili kuweza kupata haki zao kwa utaratibu.
Ameongeza kuwa mwekezaji ili afanye kazi ni lazima awe na hati miliki ya eneo na kwamba Serikali na wananchi kwa ujumla wanahitaji mwekezaji lakini, mwekezaji huyo anapaswa kuwa na faida kwa Serikali na jamii inayomzunguka. Mwekezaji akiwa mzuri hata wananchi watanufaika.
Aidha amewataka wanakijiji kuacha kufanya shughuli kwenye eneo hilo mpaka hapo suluhisho litakapopatikana, wanakijiji wameelezwa kulinda eneo hilo na kuhakikisha hakuna shughuli inayoendelea katika eneo hilo na kwa yeyote atakayekwenda kinyume na taratibu hizo Serikali itachukua hatua.
“Walinzi wa mali zenu ni ninyi wenyewe, kila mmoja awe mlinzi kuhakikisha kuwa eneo hilo halifanyishiwi shughuli tena mpaka suluhu itakapopatikana , mkibaini mtu anakwenda kinyume na utaratibu huu mtoe taarifa na Kamada wa polisi Wilaya atachukua hatua stahiki” amesema Gondwe.
Kwa upande mwingine Mkurugenzi Mtendaji Bw. William Makufwe amesema kuwa mwekezaji ahakikishe anapata hati na kuiwasilisha kwenye ofisi yake kinyume na hapo utaratibu wa kisheria utafuatwa ili kumpokonya ardhi hiyo kwa kupeleka pendekezo la kumyangaya ardhi hiyo kwenye baraza la madiwani kwa sababu atakuwa hana hati.
Aidha ameongeza kuwa hata akifanikiwa kuipata hati halali Halmashauri haitaweza kumvumilia mtu awe na ekari1000 lazima zitapunguzwe ili ekari nyingine ziweze kufanya shughuli za maendeleo kwenye Halmashauri na Kijiji husika.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni akizungumza na wanakijiji na mwekezaji.
Mkurugenzi Mtendaji akizungumza na wanakijiji na mwekezaji
Baadhi ya wataalamu na wanakijiji
wanakijiji wakisikiliza kwa makini.
Mwenyekiti mstaafu wa Kjiji cha Mkomba akijibu utaratibu alioufuata katika kumuuzia mwekezaji ardhi.
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa