Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh.Godwin Gondwe jana ametembelea eneo la ujenzi wa kiwanda cha kuchakata mahindi na matunda kinachojengwa katika kijiji cha Michungwani mashariki,Kata ya Segera kuona maendeleo ya ujenzi wa kiwanda hicho.
Mh.Gondwe amewahimiza wawekezaji kuwanufaisha wakulima wa Handeni kwa kununua mazao yanayolimwa katika Wilaya hii kupitia vikundi vya wakulima wadogo wadogo wanaosimamiwa na Wilaya ambao watanufaika na kiwanda moja kwa moja bila kupitia kwa madalali ambao wakati mwingine watakwamisha wakulima hao kupata haki zao kwa wakati au kutopewa stahiki halali.
Pia alimpongeza mwekezaji huyo kwa kuonyesha jitihada za haraka baada ya kupewa ardhi ya kiasi cha ekari kumi bure kwani hakuchukua muda akaanza ujenzi wa kiwanda hicho hivyo alimuahidi kupata ushirikiano wowote anaouhitaji na alimuhakikishia upatikanaji wa malighafi yakutosha kwa kuwa Handeni ina mahindi yakutosha na machungwa yakutosha. Amemueleza mwekezaji huyo kuwa kuna wadau mbalimbali Handeni ambao kwa mwaka huu wameshatoa mbegu mpya ya mazao ya michungwa ya ekari takribani 7000 na kwamba ataendelea kuhamasisha wananchi kupanda hiyo mbegu mpya kwa kushirikiana na maafisa kilimo.
Mwekezaji wa kiwanda hicho Bw.John Charles Kessy amesema kuwa ujenzi wa kiwanda hicho kinachojengwa mpaka kikamilike kitagharimu kiasi cha shilingi bilioni 14 ambapo ndani yake kutakuwa viwanda vinne(4 in one) yaani kiwanda cha kuchakata mahindi,kiwanda cha kuchakata matunda,kiwanda cha kuchakata maharage,ulezi na dengu pamoja na utengenezaji wa chakula cha mifugo. Uchakataji utafanyika kwa awamu mbili, awamu ya kwanza wataanza na kuchakata mahindi utakaoanza rasmi mwezi Januari 2019 na kiwanda kitakuwa na uwezo wa kuchakata tani 120 ya mahindi kwa siku.
Amesema kuwa katika kuchakata matunda wakati wanasubiri aina mpya ya machungwa watatumia aina ya machungwa yaliyopo hivyo ameomba wakulima kuhamasishwa kulima mazao ya mahitaji ya kiwanda kwa wingi, Pia ameomba kufanyika kwa mawasiliano ya kuunganisha wakulima na mabenki ili malipo yafanyike moja kwa moja benki badala ya wakulima kupewa fedha mkononi.
Naye Mkurugenzi wa Halmashuri ya Wilaya ya Handeni Bw.William Makufwe amepongeza jitihada za mwekezaji huyo na kwamba pale atakapohitaji ushirikiano wowote ofisi yake iko tayari na amemuahidi kuhamasisha wakulima wa Handeni kulima mazao kwa wingi ili kuhakikisha malighafi ya kiwanda yanakuwepo ya kutosha hatimye kufikia malengo na ndoto ya Mh.raisi ya uchumi wa viwanda katika nchi yetu.
Mh.Diwani wa Kata ya Segera Bw.Yasini Tamimu kwa niaba ya wananchi amesema kuwa wamepata faraja sana kujengwa kwa kiwanda hiki kwani sehemu kubwa ya wananchi wa Handeni ni wakulima wa mahindi na matunda hivyo kupitia kiwanda hiki tutakuwa na soko la uhakika la mazao yetu na bei pia itakuwa nzuri, Ameishukuru sana serikali kwa kuleta mwekezaji Handeni na ameahidi kuwa watampa ushirikiano mwekezaji huyo.
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa