Akizungumza kwenye makabidhiano ya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Handeni Ndugu Siriel Mchembe amewashukuru viongozi wa Kitaifa, Mkoa na Wilaya pamoja na wananchi wa Handeni walivyoshirikiana katika kuijenga Wilaya ya Handeni na kufanikiwa kufika hapo ilipo tangu yeye alipoteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kumwamini katika kipindi chote alichokuwa katika nafasi ya ukuu wa Wilaya ya Handeni.
Akitaja baadhi ya Miradi na miundombinu ambayo imefanikiwa katika kipindi chake ni pamoja na kusimamia upatikanaji wa maji kwenye Wilaya ya Handeni,ujenzi wa barabara,ujenzi wa vituo vya Afya,ujenzi wa madarasa pamoja na utekelezaji wa ilani ya dira ya kitaifa ya Maendeleo.
Pia Ndg. Mchembe ametumia nafasi hiyo kuwaaga madiwani, watumishi pamoja na wananchi wote wa Handeni na kuwaomba kumpa ushirikiano mkubwa Mkuu wa Wilaya mpya ili awaletee maendeleo wananchi wa Handeni.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mhe. Albert Msando amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassani kwa kuendelea kumwamini na kumteuwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Handeni na kuahidi kutoa ushirikiano kwa viongozi wote wa Wilaya ya Handeni na wananchi kwa ujumla ili waweze kufikia malengo ya Kitaifa katika ujenzi Taifa.
Mhe. Msando amesema kuwa anataka kupitia mikataba yote ya miradi ya 2023 ifike ofisini ili kuona imeanza lini na inaisha lini,lengo ni kujua thamani ya pesa kwenye miradi inayotekelezwa kwenye Wilaya ya Handeni.
Mkuu wa Wilaya anachukizwa na watu wanaoeleta mazoea kwenye kazi na anakerwa sana na tabia za kuchunguzana na kuripotiana vibaya kwenye kazi na kusema kuwa wenye kazi hiyo wapo.Yeye anapendezwa na wanaofanya kazi kwa weledi pia amesema kuwa mifumo ikafanye kazi kila mtu kwa nafasi yake awajibike kuanzia kwenye kitongoji hadi ngazi ya Halmashauri na kero za wananchi zote zitatuliwe.
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa