Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Mhe. Mussa Mwanyumbu na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Bw. Saitoti Zelothe Stephen wamefanya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye kila Kata na kisha kufanya vikao na Kamati za Maendeleo za Kata (KAMAKA) kwa kila Kata kwa kata zote 21 za Halmashauri ya Handeni. Wakati wa ziara hiyo viongozi hao wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia Halmashauri ya Wilaya ya Handeni fedha kwa ajili ya ujenzi wa Miundombinu mbalimbalimbali ambayo itasaidia wananchi wa Handeni.
Mhe. Mwanyumbu na Bw. Saitoti.wameshatembea kata 5 kati ya kata 21, Kata hizo ni pamoja na Kitumbi, Mkata, Komkonga, Kabuku na Kabuku Ndani.
Mhe. Mwanyumbu amesema lengo la kufanya ziara hiyo ni kuangalia maendeleo ya miradi kwenye kila Kata na kusikiliza changamoto na kero mbalimbali zinazowakabili Kamati za Maendeleo za Kata na kuzipatia ufumbuzi ili kufanya kazi kwa ufanisi.
Mhe. Mussa Mwanyumbu amezipongeza kamati zote zilizosimamia ujenzi wa Madarasa ambapo jumla ya kiasi cha Shilingi bilioni mbili na milioni miambili kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya vyumba vya madarasa 72 kwa shule za Sekondari na madarasa 19 ya shule shikizi 7 za Msingi kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19.
Baada ya kusikiliza kero mbalimbali za Kamati za Maendeleo za Kata Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Handeni Bw. Saitoti Zelothe Stephen alitatua baadhi ya kero papohapo na kuchukuwa changamoto nyingine kwenda kuzifanyia kazi ikiwepo suala la malimbikizo ya mishahara ya watumishi na migogoro ya ardhi..
Aidha Bw. Saitoti ametoa maelekezo kwa Kamati za Maendeleo za Kata zote 21 za Halmashauri ya Wilaya ya Handeni kuwa Kamati zote za Maendeleo ya Kata zikae kila mwezi na zitoe tarifa za miradi kwa jamii na kutatua changamoto za wananchi, Kila Kata na kijiji visome taarifa za mapato na matumizi ya ofisi zao pia amepiga marufuku viongozi wa kata au vijiji kuuza ardhi bila kufuata sheria na taratibu za uuzaji wa ardhi.
Mkurugenzi Mtendaji alihitimisha kwa kusema kuwa kila mtu kwa nafasi yake asimamie ukusanyaji wa mapato na wasiruhusu bidhaa kutoka kwenye Kijiji au Kata bila kulipia ushuru wa Halmashauri kwa kufanya hivyo mapato ya Halmashauri yataongezeka na kutoa ushauri kuwa miradi ya ujenzi inayotekelezwa na serikali ya kijiji ikamilishwe isiishie kwenye lenta na kusubiri Serikali kuja kuimalizia ambapo itachukuwa muda mrefu husani madarasa.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Handeni Mhe. Mussa Mwanyumbu (aliyevaa shati la pink) akiwa na Mkurugenzi Mtendaji Saitoti Zelothe Stephen (aliyeva Suti) wakikagua boma la darasa la Shule ya Msingi Msilwa.
Madarasa Matano ya Shule ya Sekondari Kwaludege.
Wakikagua jengo la choo kwenye eneo ambalo wanatarajia kujenge stendi ya manasi Kabuku
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa