Naibu Waziri wa maji Mh.Jumaa Aweso amewachukulia hatua wakandarasi wa mabwawa ya Manga na Mkata yaliyoko katika Kata ya Mkata Halmashauri ya Wilaya Handeni kwa kuwaweka mbaroni jana, hii ni baada ya kutembelea mabwawa hayo kuona mwenendo wa ujenzi na wakandarasi hao kutokuonekana eneo la Bwawa la Manga kwa kujitetea kuwa wanaendelea na kazi ya ujenzi wa Bwawa la Mkata.
Akizungumza na wananchi wa Kata ya Mkata baada ya kutembelea mabwawa hayo amewaeleza kuwa yeye kama waziri wa maji hatakuwa kikwazo kwa wananchi kupata maji safi, salama na yakutosheleza na kwamba dhamana aliyopewa na Mh. Raisi ya kuwa naibu waziri wa maji ni ya kutetea wananchi wanyonge kupata maji safi, salama na ya kutoshelea na pia anatambua kuwa utekelezaji wa miradi ya maji inategemeana na upatikanaji wa fedha lakini maeneo mbalimbali fedha inapelekwa na watu wanatumia vibaya halafu hakuna hatua zinazochukuliwa na wananchi wanapata tabu hasa akina mama.
Aliongeza kuwa yeye ametembelea mabwawa hayo lakini hakuona kazi iliyofanyika ambayo itawafanya wananchi kupata maji na watu wanaendelea kuumia na kuteseka, Amesema haiwezekani viongozi wanakuja mara kwa mara hadi raisi katoa agizo, utekelezaji usiwepo na sisi bado tunaendelea kubembelezana, mkandarasi anaitwa eneo la mradi anakaidi na kudharau hivyo aliagiza Mkuu wa Polisi kuwaweka wakandarasi hao ndani ambao ni Mkurugenzi wa mradi wa kampuni ya Tansino Logistics,Mtaalamu msahuri (Don Consults) na mhandisi wa ujenzi. Amesema kuwaweka ndani wakandarasi hao siyo suluhisho kwani wananchi wa Mkata wanahitaji maji wala siyo maneno na siyo kwamba fedha hazipo ila watu wanafanya ujanja ujanja hivyo amewaahidi wananchi kulisimamia hilo na amewaagiza watu wa mamlaka ya maji Chalinze na Tanga kukutana na kumpa mrejesho wa namna gani wananchi wa Mkata wanapata maji safi kwa haraka ” haiwezekani fedha zikae kwenye benki na watu hawana maji, hawatatuelewa”alisema.
Baada ya kutembelea mabwawa hayo na kutoa maagizo pia aliongea na wananchi wa Kata ya Kang’ata na kuwaahidi kupata maji safi, salama nay a kutosheleza na kwamba Handeni tayari wamepewa kibali cha kuchimba visima kumi na kwa upande wa Kang’ata amewaongeza kisima kimoja katika idadi ya visiwa waliyopewa, Amemshauri mhandisi wa maji wa Halmashauri kutumia wakala wa uchimbaji wa serikali ili wakapochimba maji sehemu wakakosa wanarudia tena kuchimba na pia hao wakala waangalie namna ya kutatua matatizo ya maji na kwamba kutokana na changamoto ya maji serikali imetenga kiasi shilingi Bilioni 1.374 ili kutatua tatizo la maji.
Kwa upande ujenzi wa tanki la maji lililoko Kata ya Malezi Halmashauri ya mji wa Handeni Mh.Naibu Waziri amempa wiki nne mkandarasi kukamilisha mradi huo baada ya mkandarasi huyo kumweleza changamoto zilizokwamisha mradi huo kukamilika kwa wakati.
Alihitimisha kwa kuwataka wataalam kufanya kazi kwa bidii ili wananchi wapate huduma wanayopaswa kupata na kwmba wahandisi wa maji wa Halmashauri na Mkoa washirikiane kuhakikisha fedha za miradi ya maji inatumika ipasavyo na kwa wakati na pia kuhakikissha miradi inatekelezaka kwa wakati.
Naye Mbunge wa Handeni vijijini Mh.Mboni Mhita amesema kuwa changamoto ya maji Handeni limekuwa la muda mrefu hivyo anaimani na ujio wa Mh.Naibu Waziri katika kutatua changamoto hiyo kwani akisema anatenda na kwamba baada yakutembelea mabwawa na kujionea hali halisi anaamini maamuzi mazito yatatolewa na pia watu wanaokwamisha upatikanaji wa maji Handeni wataondolewa kwenye mtandao wa maji ili wananchi wapate maji kwa haraka, Aliongeza kuwa hata kwa upande wa mradi wa HTM kuna tatizo hivyo ujio wake utatoa ufumbuzi wa namna ya kuharakisha upatikanaji wa maji Handeni.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh.Godwin Gondwe amemshukuru Mh. Naibu waziri wa maji kwa kuja kuona hali halisi ya maji Handeni mwenyewe hivyo anaamini tatizo la maji Handeni linakwisha, Amemuahidi kusimamia fedha itakayoletwa inakwenda kufanya kazi iliyokusudiwa kwani atathibiti mianya ya ubadhirifu wa fedha hizo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bw. William Makufwe amemweleza Mh.Naibu Waziri kuwa baada ya kuona mabwawa hakujengwa kwa viwango vinavyotakiwa tulichukua hatua ya kuandika barua Wizarani ili kupata mbinu mbadala ya kutumia chanzo cha Chalinze (CHALIWASA) ili wananchi wa Mkata wapate maji hivyo anaamini ujio wake utatatua tatizo la maji Mkata na Handeni kwa ujumla.
MWISHO.
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa