Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.John Pombe Magufuli amewataka wakandarasi wajenzi na washauri waliojenga mabwawa ya Manga,Mkata na Kwandungwa chini ya kiwango kuwepo kwenye site ndani ya wiki 2 kuanzia leo ili kujenga mabwawa hayo kwa kiwango cha fedha ambacho tayari wamechukua cha Tsh. Bilion 2.8 au kwenda jela kuelezea namna gani watarejesha fedha hizo za watanzania .
Amri hiyo meitoa leo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Handeni eneo la viwanja vya Mbwembwele Handeni Mjini akitokea Tanga kwenye uwekaji wa jiwe la Msingi wa Bomba la mafuta Linalounganisha Tanzania na Uganda.
Rais Magufuli amesema kuwa haiwezekani kiasi kukubwa cha fedha kama hicho kulipwa bila kuwepo kwa maji yanayowafikia wananchi.Amewataka wakandarasi kuwepo eneo la site na kujenga upya mabwawa kwa kutumia fedha zao hadi itakapofikia hatua ya certificate (cheti) ya kulipwa na Serikali Bilioni 1.2 ndipo watakapolipwa na kwamba fedha za watanzania haziendi bure na haiwezekani wananchi wa Handeni kusubiri maji kwa miaka 5 wakati fedha zao tayari zimetumika.
Aidha amewaeleza wananchi kuwa atahakikisha tatizo la maji Handeni linatatuliwa kwasababu kuna miradi mitatu ambayo inatarajiwa kuleta matokeo chanya ikiwemo mradi wa Bilion 2.6 unaomalizikia utakao unganisha maji maeneo ya Manga, Mkata na Handeni, mradi wa zaidi ya Bilion 200 maji yatatolewa Pangani na Mabwawa hivyo kumaliza tatizo la maji .
Amewataka wakandarasi waliopo na wajao kufanya kazi kwa weledi na wakati ili kufikia malengo kwa wakati uliopangwa na kwamba hatakuwa tayari kuwashikilia wakandarasi watakaokwamisha upatikanaji wa maji ya uhakika Handeni.
“Wakandarasi mliopo na mtakaokuja mkitaka kugombana na mimi chezeni na miradi hii maji ya Handeni” amesema Rais Dk. John Magufuli.
Kwa upande mwingine amewataka wananchi wa Handeni kuwa wavumilivu na kushirikiana vyema na watumishi wa Afya kwa sababu wanafanya kazi kubwa ya kuwahudumia wagonjwa kulinganisha na idadi ndogo ya watumishi iliyopo, amewaeleza kuwa ajira zilisitishwa kwa muda kutokana na zoezi la uhakiki hivyo hivi punde watumishi wa Afya wataongezeka kwani ajira zimekwisha anza kutolewa. Aidha amewataka wananchi kujiunga na mifuko ya bima ya afya ili kuboresha huduma za afya na kuhakikisha wanapata huduma kwa wakati pindi wanapohitaji kuhudumiwa.
Sambamba na hilo Rais amepiga marufuku wafugaji kulisha mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima na kuwataka viongozi ngazi ya Mkoa na Wilaya kuhakikisha wanasimamia katika kutatua changamoto za wakulima na wafugaji kabla matatizo hayajakuwa makubwa na kugeuka kero, amewataka wakulima na wafugaji kuishi kwa amani kwasababu wanategemeana kwa kiasi kikubwa.
Amewaagiza TAKUKURU kusimamia ili kubaini viongozi wanaopokea rushwa hususani kwa wafugaji ambao wanapesa kwalengo la kupindisha kero za wakulima na wafugaji hali inayopelekea kudumu kwa migogoro ambayo ingeweza kutatuliwa kwa wakati.
Amewataka wananfunzi kuhakikisha wanasoma kwa bidii na kutumia vyema fursa ya elimu bure ili kujiandaa kuwa viongozi wa baadae na kuwaeleza kwamba changamoto ya upungufu ya walimu inakwenda kutatuliwa hivi karibuni kwani ajira zimekwisha tangazwa na zilichelewa kupisha uhakiki wa watumishi waliokuwa wananufaika kinyume cha utaratibu.Amewahakikishia wanafunzi kuwa Serikali imeweka kipaumbele kwenye elimu hususani kwa watoto wa kike.
Mwisho amepongeza wananchi wa Handeni kwa namna wanavyojishughulisha na shughuli za kiuchumi hususani kilimo na ufugaji ambazo ni tija kwa maendeleo yaTaifa letu na kuwataka kuendelea na motisha ya kufanya kazi kwa juhudi huku wakiendelea kulinda amani na umoja uliopo ili kuendeleza Taifa. Rais pia ameahidi kumalizia barabara inayounganisha Dumila na Handeni yenye utrefu wa KM 50 kwa kiwango cha lami ili kurahisisha shughuli za kiuchumi na usafirishaji .
Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Joseph Pombe Magufuli amuzungumza na wannchi wa Handeni alipokuwa akimalizia ziara yake akitokea Tanga Mjini.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Magufuli akizungumza na wananchi wa Handeni kwenye viwanja vya kwambwembwele
Mbunge wa Handeni Vijijini Mh. Mboni Mhita akizungumza na wananchi wa Kwachaga.
Mh. Rais John Magufuli akizungumza na wananchi wa Mkata
Baadhi ya Wananchi wa Kata ya Kwachaga
Viongozi mbalimbali wakimsikiliza Mh. Rais Magufuli eneo la Manga mpakani mwa Mkoa wa Tanga na Chalinze.
Mh. Rais Magufuli akisalimiana na wanafunzi wa Maganga sekondari kwa kuwahimiza kusoma kwa juhudi.
Mwanafunzi wa Manga Sekondari akifurahia ahadi ya Mh.Rais ya kutatua changamoto ya upungufu wa walimu hususani walimu wa sayansi.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mh. Martin Shigella akimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutembelea mkoa wa Tanga.
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa