Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mh. Martin Shilega alitembelea Wilaya ya Handeni jana tarehe 10-01-2019 lengo likiwa ni kuona mwenendo wa ugawaji wa vitambulisho vya wajasiriamali na kusikiliza kero mbalimbali za wananchi ambapo alipata muda wa kuwagawia wajasiriamali zaidi ya mia moja katika miji midogo ya Segera, Kabuku na Mkata.
Akizungumza na wananchi Mh.Shigela aliwataka wajasiriamali ambao hawapo kwenye mfumo rasmi wa walipa kodi kujitokeza kwa wingi kupata vitambulisho hivyo ili kuepukana na usumbufu wa ushuru wanaotozwa kila mara kitu kinachowapelekea kutoa zaidi ya laki moja kwa mwaka badala yake wachukue vitambulisho vinavyowagarimu shilingi elfu ishirini kwa mwaka mzima.
Pia aliwapongeza wajasiriamali kwa kujitokeza kwa wingi kuchukua vitambulisho hivyo ikiwa ni kuunga mkono rai na dhamira ya Mh. Raisi ya kuhakikisha kila mjasiriamali mdogo kuwa na kitambulisho chake na kuwahakikishia watakaokosa kwa awamu hii kupata awamu ijayo na kwamba viongozi wa Wilaya wahakikishe wanawatambua na kuwaainisha wajasiriamali ambao bado hawajapata vitambulisho ili kuweka utaratibu wa wajasiriamali hao kupata vitambulisho vya wajasiriamali.
Aidha Mh. Shigela aliwataka viongozi wa Wilaya kutowatoza ushuru wowote wajasiriamali ambao wamepatiwa vitambulisho na alisema mjasiriamali hatakiwi kulipa fedha zaidi ya hiyo ya kitambulisho ambayo ni kiasi cha shilingi elfu ishirini kwa mwaka mzima “Hatutarajii kuona michango wala ushuru wala tozo wala kusukumwasukumwa”alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh. Godwin Gondwe alimshukuru Mkuu wa Mkoa na timu yake kuja kuweka msukumo kwa wajasiriamali wa Handeni na alisema kwamba Handeni inatakribani asilimia tisini ya ugawaji wa vitambulisho, hivyo ndani ya siku mbili watakuwa wamekamilisha kugawa vitambulisho vyote elfu nne kwa Halmashauri ya Wilaya na Mji na kuwaorodhesha wale waliokosa ili waandaliwe utaratibu wa kupata.
Aliongeza kuwa wafanyabiashara wadogo wadogo wameitikia vizuri na kwamba anamshukuru Mh.Raisi kwa kuwaomboa wajasiriamali wadogo kwakuwa wakitoa elfu ishiri wanaepukana na kero za ushuru mbalimbali.
Naye Mkurugenzi Mtandaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bw. William Makufwe alisema Halmashauri ya Wilaya ya Handeni tulipewa vitambulisho elfu mbili na wameuza vitambulisho 1,677 hivyo aliahidi ndani ya siku mbili vilivyobaki vitakuwa vimeisha kutokana na mwitikio mkubwa wa wajasiriamali wanaohitaji vitambulisho.
Pia alieleza kwa masikitiko makubwa ajali ya gari la Halmashauri ambayo ilipata ajali wakati wa kwenda kugawa vitambulisho na kusababisha watumishi wanne kuumia pamoja na kupelekea upotevu wa vitambulisho 80.
Moja wa wajasiriamali Bi Saida Adamu alisema wao kama wajasiriamali wadogo wamefurahi sana na pia wanamshukuru Mh.Raisi kwa kuwatambua wajasiriamali wadogo na kuanzisha utaratibu ambao utawasaidia wao kufanya biashara yao kwa kodi nafuu kwani wamekuwa wakitozwa ushuru kila mara.
Mkuu wa wa Mkoa wa Tanga Mh. Martin Shigela wa kwanza kushoto akigawa vitambulisho kwa wajasiriamali
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa