Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mh. Martin Shigela alitembelea mgodi wa kusini gateway Indusrial Park uliyoko katika kijiji cha Kwedikabu, Kata ya Kwamsisi Wilaya ya Handeni jana tarehe 28-04-2019 kujionea maendeleo ya mgodi huo na kutoa maelekezo kwa wachimbaji hao.
Mh.Shigela aliwapongeza wachimbaji hao kwa kazi nzuri wanayofanya lakini aliwaeleza wachimbaji hao kufuata kanuni, taratibu na sharia za uchimbaji wa madini ya Tanzania. Pia aliwataka wachimbaji hao kuwashirikisha wataalamu na maofisa wote wa serikali ambao wanatajwa kwa mujibu wa sharia ya madini kuwepo wakati wa uchenjuaji wa madini na kwamba wakae eneo la mgodi ili waweze kujua kiasi na aina ya madini yatakayopatikana katika migodi.
Aidha Mh.Shigela amesema tarehe 18-05-2019 kutakuwa na uzinduzi wa soko la madini ya Mkoa wa Tanga ambayo itafanyika katika Wilaya ya Handeni ukihusisha wachimbaji wote wa madini wa Mkoa wa Tanga, wanunuzi wa madini, wauzaji, Mamlaka ya Mapato Tanzania,Taasisi na fedha, Taasisi za Umma na wananchi kwa ujumla ili kutoa elimu ya pamoja juu ya taratibu za uendeshaji wa soko la madini.
Amesema tutatoa maeneo ya uuzwaji wa madini kwa Mkoa wa Tanga na yeyote atakayeuza nje ya maeneo yaliyotengwa na utaratibu uliotolewa atakuwa sehemu ya uhujumu uchumi na sehemu ya kuturudisha nyuma jambo ambalo hatutalikubali. Rai yake kwa wachimbaji wa madini ni kwamba wahakikishe wanalipa kodi na wananchi wa maeneo ya migodi wanufaike lakini pia amewaasa wananchi kuzalisha kwa wingi ili huduma yoyote itakayohitajika ndani migodi iweze kupatikana na mzunguko wa fedha utakaopatikana ulete tija kwa wananchi wa Mkoa wa Tanga.
Baada ya kutembelea mgodi huo Mkuu wa Mkoa alitembelea jingo la kituo cha Afya Kwamsisi kilichojengwa na shirika lisilo la kiserikali linaloitwa World vision ambalo halijaanza kufanya kazi kutokana na kutokukamilika kwa baadhi majengo na kuagiza zahanati ya Kwamsisi kuhamishiwa hapo ili majengo yaliyopo yasije yakaharibika wakati wanaendelea na ukamilishaji wa majengo mengine ili iwe na hadhi ya kituo cha Afya.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh.Godwin Gondwe alisema serikali itahakikisha mazingira mazuri kwa wawekezaji Handeni na kushirikiana kwa karibu wanapokutana na changamoto ili kuzitatua mapema hasa suala la migogoro ya ardhi na mwisho wa siku kufikia malengo ya Mh. Raisi ya Tanzania ya viwanda
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bw. William Makufwe amesema ili kuhakikisha mwekezaji huyo anakuwa na mazingira mazuri kijiji tayari kimepimwa na kupangiwa matumizi kitu kitakachosaidia kuepusha migogoro, pia amesema kupitia mwekezaji huyo Halmashauri itapata 0.3% ya ushuru wa madini na hii itasaidia kuongeza mapato ya ndani ya Halmashauri.
Naye Mkurugenzi wa mgodi wa Kusini Gateway Industrial Park Bw. Abdulahi Abdalah Mohamedi alisema mgodi huo umetoa ajira kwa wananchi wa Handeni zaidi ya 30 na wameshasajiliwa kwa sasa na kwa hatua zinazofuata wataajiri wafanyakazi 54 tena.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mh.Martin Shigela wa kwanza kushoto akisikiliza jambo kutoka kwa Mkurugenzi mgod wa kusini gateway.
Ukaguzi wa mitambo ukiendelea katika mgodi wa Kusini gateway Industrial Park.
Mganga mkuu Dkt. Credianus Mgimba wa pili kulia akiongoza msafara wa Mkuu wa Mkoa katika ukaguzi wa jengo la kituo cha Afya Kwamsisi.
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa