RC SHIGELA AWATOA WASIWASI WAKULIMA WA MHOGO TANGA;
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mh.Martin Shigela alifanya kikao cha pamoja na Wadau mbalimbali wa kilimo wa Mkoa wa Tanga wakiwepo waheshimiwa wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala, Wenyeviti wa Halmashauri, Wakurugenzi wa Halmashauri, mashirika ya kiraia, waheshimiwa madiwani, wakulima, Maafisa Tarafa,Taasisi za kifedha na wanunuzi wa mihogo.
Kikao hicho kilifanyika leo katika ukumbi wa Hotel ya Nemdende iliyoko Handeni Tanga baada ya wadau hao kutembelea na kuona baadhi ya mashamba ya mihogo yaliyoko Halmashauri ya Wilaya ya Handeni jana ikiwepo Mgambo JKT na shamba la Bw. Adam Mabewa, lengo la kikao hicho ni kufanya tathmini ya kilimo cha mihogo kwa Mkoa wa Tanga na kuhamisisha wakulima kulima zao hilo wa kwa tija.
Mh. Shigela alisema awali walihamasisha wakulima kulima zao la muhogo kwa lengo la kuondokana na njaa kutokana na uhaba wa mvua hivyo njia pekee ni kulima mazao yanayostamili ukame lakini sasa wakulima wamezalisha kwa wingi mpaka wakapata ziada ya kuuza ambapo uzalishaji huo ukapelekea changamoto ya soko
Aliongeza kuwa Serikali imeipa uzito zao la muhogo ndiyo maana imefungua masoko na nchi ya China ili wakulima waweze kusafirisha muhogo China lakini pia dhamira ya uchumi wa viwanda imewarahisishia wawekezaji kuja kuwekeza viwanda vya kuchakata mihogo na kuongeza thamani ya zao la muhogo. Aidha alisema kwa wazalishaji kujitambua wameona ni vyema kuanzisha chama cha wakulima wa muhogo Tanzania ambacho kitasimamia bei na kutafuta masoko.
Pia aliwataka wajumbe kuwa mabalozi wazuri kufikisha ujumbe kwa wakulima ili kujipanga vizuri namna ya uuzwaji wa zao hilo na kufikiria mfumo mzuri wa kuuza ambapo aliwaagiza maafisa Ushrika kuweka mikakati ya suala zima la namna ya uuzaji wa muhogo.
Alihimitisha kwa kuwashukuru wajumbe kwa kikao kizuri ambacho kimetoka na maazimio mazuri kwa kuwa kumekuwa uhakika wa soko kwa wakulima, watu wamepata uzoefu na maelezo ya kitaalamu kwa kuzalisha kwa tija pamoja na kuvuna kwa wakati akitoa mfano wa mbegu ya Mkuranga ambapo inatakiwa ivunwe kuanzia miezi saba mpaka miezi tisa ili uwe na ubora na wenye soko “ili uzalishe kwa tija lazima ulime kwa tija”. Alisema.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga Mhandisi Zena Said amesema kupitia kikao hiki tumeweza kupata mambo mengi na kurekebisha wakulima wetu nini wafanye kutoka kilimo cha kujikimu kwenda kwenye kilimo cha biashara na kwamba muhogo ni zao ambalo linaweza kuwatoa kiuchumi, Kama viongozi wa Mkoa wa Tanga watalisimamia kuhakikisha zao hilo lina limwa kwa wingi na kwa tija kuanzia ngazi ya familia hadi Mkoa ili kuongeza pato la Mkoa la Taifa hivyo wakulima walime kwa tija ili waweze kupata faida.
Mhandisi Zena amesema palipo na changamoto fursa zinatokea hasa kwa wale ambao hawana machine za kukatakata mihogo watawapa ajira watu ili wakatekate lakini pia kunakuwa viwanda tembezi hasa mashine za kuchakata mihogo.ambazo zitawarahisishia wakulima kuchakatiwa mihogo yao.
Mwenyekiti wa wakulima wa zao la Muhogo Tanzania Bi Mwamtumu Mahiza alishukuru uongozi wa Tanga kwa kuitisha kikao hicho kwani mkutano huo umewaonyesha fursa kubwa ya kiuchumi ambayo Mkoa wa Tanga unahitaji na alisema kuwa umaskini Tanga utaisha endapo wakulima watalima muhogo kwa wingi na kwa kufuata kilimo cha kitaalamu.
Alitoa wito kwa wakulima kuwa waache kulima zao la muhogo kwa mazoea na kuishia kulalamika kuwa muhogo hauna faida badala yake walime kitaalamu ili waweze kupata faida na kujikwamua kiuchumi.
Afisa kilimo Mkoa wa Tanga Bw. Daniel Mgori akisoma ripoti ya uzalishaji wa muhogo ya Mkoa alisema wakulima wanaojihusisha na kilimo cha muhogo ni zaidi ya laki mbili ambao wanazalisha tani million mbili za muhogo mbichi, Alisema awali uzalishaji huo ulikumbutana na changamoto ya soko lakini anashuruku sasa changamoto hiyo imetatuliwa kutokana na wengine kuja kununua na wengine kuanza kujenga kiwanda hivyo anawahimisha wakulima wazalishe kwa wingi kutokana na kupatikana kwa soko la uhakika la zao hilo.
Aidha alitaja Wilaya ambazo zinafanya vizuri katika uzalishaji wa zao la muhogo ambapo alisema Wilaya tatu zinafanya vizuri Handeni ya kwanza katika uzalishaji ikiwa ilizalisha tani takribani millioni mbili Wilaya ya Mkinga tani 224,000 ikfuatiwa na Muheza tani 111,000.
Mkurugenzi wa kampuni ya Kichina inayoitwa Tanzania Agricultural Export Processing Zone Limited(TAEPZ) Dior Feng alisema kampuni inauhitaji wa tani Mil. 2 ya muhogo mkavu uliochakatwa na watanunua kilo ya muhogo mkavu wa shilingi 250 na kwamba ununuzi huo utaanza rasmi tarehe 15/02/2019 ambapo kwa mkoa wa Tanga senta ya kununulia itakuwa Kata Mkata Halmashauri ya Wilaya ya Handeni na kwa wale wa mikoa mingine wataanza kununua tarehe 20 /02/2019 katika kichuo ambacho kipo karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa Dares-salaam, kwa ushauri au kuuliza wapige namba 0657 800008.
Dior alisema kwa kawaida muhogo unatakiwa uvunwe kuanzia miezi 7-9 ili kulinda ubora kiasi cha wanga lakini watu wengi wamepitiliza hivyo kwakuwa wao wanataka kuwainua wakulima watanunua kwa bei hiyo hiyo na kuwasihi msimu ujao wazingatie muda wa kuvuna.
Mkulima wa zao la Muhogo Bw. Adam Mabewa aliwapongeza viongozi wa Mkoa kuanzisha zao hilo kwani ni zao ambalo litawapatia wao faida kubwa endapo watalima kitaalamu kuliko wakilima mahindi, aidha alitoa rai kwa wakulima wenzake kutumia trekta kulima mashamba ili muhogo upate sehemu nzuri ya kupenyeza mizizi na shina kuzaa kilo kuanzia 12-15.
Wadau walipongeza Wilaya ya Handeni kwa kufanya vizuri na kwa pamoja walikubaliana kuunda kauli mbiu ya Mkoa inayosema “ ARDHI YA TANGA NI KARIMU, ONGEZA TIJA KILIMO KINALIPA”.
MWISHO.
Pichani ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mh.Martin Shigela wa pili kulia
akisalimiana na moja ya wakulima alipotembelea shamba la mkulima Adam.
Katibu Tawala Mhandisi Zena Said akizungumza katika cha wadau wa kilimo.
Mwenyekiti wa chama cha wakulima Tanzania Bi Mwantumu Mahiza akitoa rai kwa wakulima wa muhogo.
Viongozi na wadau wakiwa kwenye picha ya pamoja baada kuona shamba la muhogo la Mgambo JKT.
Mkulima Adam Mabewa wa kwanza kushoto akitoa uzoefu kwa kilimo cha muhogo kwa wadau.
Mkurugenzi wa kampuni ya kichina TAEPZ Dior Feng akitoa ufafanuzi wa jambo katika kikao hicho.
Wadau wakifuatilia maongezi katika kikao hicho.
Kamati ya ulinzi na Usalama ikifuatilia maongezi katika kikao hicho.
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa