Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mh.Martine Shigella amepongeza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni ukiongozwa na Mkuu wa Wilaya na Mwenyekiti wa Halmashauri kwa kutekeleza vyema agizo la kilimo cha zao la muhogo miongoni mwa wananchi wa Handeni.
Pongezi hizo zimetolewa jana alipofanya ziara ya kutembelea mashamba ya wakulima wa zao la Muhogo Kata ya Kwamsisi Halmashauri ya Wilaya ya Handeni na kusema kuwa ,2016 ilitokea hali ya upungufu wa mvua hivyo wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi walielekezwa kuanza mchakato wa kuhakikisha Mkoa wa Tanga unanusuriwa na kuondolewa kwenye aibu ya upungufu wa chakula.
Alisema kuwa zao la muhogo linahimili ukame, ni zao la biashara na chakula pia, hivyo amefurahi kuona wananchi wameitikia wito kutokana na kupewa mbegu hizo bure mara baada ya viongozi kutekeleza agizo la kwenda kununua Mkuranga na kuzigawa kwa wananchi ili waweze kupata hamasa ya kulima.
Aliongeza kuwa dhamira ya Serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha wananchi wananhudumiwa na kuondokana kwa upungufu wa chakula na kuwatafutia masoko ya mazao wanayozalisha, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa viwanda.
Mkuu wa Mkoa alisema kuwa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Handeni kuzungumza na JKT Mgambo kwaajili ya kupata shamba la ekari 200 ili kuzalisha mbegu za mihogo zitakazowasaidia wananchi wa Handeni na tayari Milioni 10 zimepatikana na zitakabidhiwa kwa Mkuu wa Wilaya kwa utekelazaji.
“ Serikali ya Tanzania imeingia makubaliano na nchi ya China ili kuwauzia muhogo ,Kwamsisi mmeonesha dhamira ya dhati kwa kulima kwa wingi zao la muhogo hadi sasa mna zaidi ya ekari 16 elfu na ustawi ni mzuri, suala la kiwanda cha kuchakata mihogo nalibeba naenda kuwashawishi viongozi ngazi za juu waje waone mnachofanya , muendelee kufanya kazi na kuitikia wito ili kwenda sawa na kauli mbiu ya HAPA KAZI TU.” Alisema Mkuu wa Mkoa.
Aidha alimpongeza Afisa kilimo wa Kata ya Kwamsisi Bw. Selemani Ikosi kwa kufanya kazi nzuri na kuwataka Maafisa kilimo kuacha kukaa ofisini kwani muda huo umekwisha na badala yake waende shambani kuhudumia wananchi.
“Naagiza Maafisa Kilimo wote Mkoa wa Tanga muda wa kukaa ofisini umekwisha , nendeni shambani mkahudumie wananchi na hiyo iwe ndio mwelekeo na dira ya utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Mh. Rais na Waziri Mkuu ” Alisema Mkuu wa Mkoa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh. Godwin Gondwe aliwahamasisha wananchi kujiandaa vyema na kilimo cha muhogo katika msimu huu wa kilimo unaokuja ili kuweza kuinua hali zao kiuchumi zaidi.
Ziara ya mkuu wa Mkoa wa Tanga iliambatana na mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Kwamsisi kwa kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wa Kata hiyo na kutembelea shamba la SASAMUA.
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa