Serikali ya Wilaya ya Handeni imesema haitakuwa tayari kwa mwananchi au mzazi/mlezi atakayekuwa kikwazo kwa kukosesha haki za msingi za mtoto na wakati yupo katika nafasi ya kupata haki hizo hasa katika kipindi hiki ambacho haki zao zinatambulika ulimwenguni kote.
Hayo yamezungumzwa na Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh. Godwin Gondwe walipokuwa wanatoa msaada kwenye kituo cha kulelea watoto wenye mahitaji maalumu na ulemavu kilichopo Kwamkono Wilayani Handeni.na Taasisi ya kifedha ya DTB jana.
Mkuu wa Wilaya amesema kuwa mtoto kukosa haki ya kupata elimu,kutumikishwa katika umri mdogo, kuficha watoto walemavu kwa namna yoyote ile Serikali ya awamu ya 5 itachukua sheria, taratibu na kanuni kuhakikisha mtoto huyo anapata haki zote za msingi.
“ kitendo cha kumsababishia mtoto kukosa haki zake za msingi kunasababisha maumivu na kuzima ndoto za mtoto huyo, sisi kama Serikali ya Handeni hatutaweza kumvumilia mtu wa namna hiyo kwani atakuwa hana tofauti na wale watu waliowatesa na kuwauwa watoto huko Afrika Kusini. Tutahakikisha sheria, taratibu na kanuni zinachukuliwa kwa mhalifu huyo” alisema Gondwe.
Ametoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha fedha za TASAF wanazozipokea wanawanunuliwa watoto mahitaji ya shule na kuwapeleka shule, Elimu bure wazazi wote kupeleka watoto wote wenye umri wa kuanza shule mapema kwani hakuna malipo.
“wazazi/walezi naomba tushirikiane ili tuweze kuwafikisha watoto kwenye ndoto zao na kuwapatia haki zao za msingi” alisema Gondwe.
Aidha ametoa rai kwenye ujenzi wa majengo ya umma yanayojengwa kuhakikisha wanaweka miundombinu rafiki kwa walemavu ili kuwasaidia kwani ulemavu wao sio kikwazo cha kushindwa kupata haki zao za msingi.
Mwisho amewataka wadau mbalimbali kushirikiana na Serikali ili kwa umoja waweze kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili watoto katika kuzifikia ndoto zao.
Kwa upande mwingine Afisa Uhusiano na masoko wa taasisi ya kifedha ya Diamond Trust Bank (DTB) Bw. Silvester Bahati amesema kuwa walipata mwaliko kutoka kwa Mkuu wa Wilaya na wakaona watumie fursa hiyo kwani katika kipindi hiki cha Ramadhani na maadhimisho ya mtoto wa Afrika wamekuwa wakitembelea vituo mbalimbali vilivyopo kwenye matawi yao kote Tanzania ili kurejesha kiasi kidogo cha faida waliyoipata kwa jamii hususani kusaidia wenye uhitaji .
Aliongeza kuwa wameungana kuadhimisha siku ya mtoto wa Afrika na kituo cha Kwamkono kuonesha kuwa wao kama Taasisi wanaunga mkono jitihada za kuboresha mwenendo mzima wa maisha na makazi kwa watoto wa Afrika.
“upo karibu na jamii, hatuwezi kujiendesha bila kiuwa na jamii nyuma yetu, tunaitegemea jamii na jamii inatutegemea” alisema Silvester.
Kituo cha Kwamkono kinamilikiwa na Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Tanga kina watoto zaidi ya 50 ambapo kilianzishwa mwaka 1963 na waanzilishi walikuwa masista wa passion for Christ kwa lengo la kushughulikia watoto walioathirika na ugonjwa wa polio na mwaka 1973 kubadilishwa kuwa kituo cha kulelea watoto wenye mahitaji maalumu wanaoweza kufundishika.
Kituo kinajiendesha kwa miradi midogo midogo ya kulima mbogamboga, mradi wa maji unaosaidia kituo na jamii inayozunguka,vibanda vya kupangisha (fremu) na wahisani mbalimbali.
Diamond Trust Bank imetoa msaada wa vyakula na mahitaji mbalimbali ya shule kwa watoto vyenye thamani ya milioni moja.
Baadhi ya Watoto waliopo kwenye Kituo cha Kwamkono.
Picha ya pamoja mara baada ya makabidhiano ya Zawadi.
watoto wakishangilia kupewa zawadi na Diamond Trust Bank.
Mkuu wa Wilaya Mh. Godwin Gondwe akimsaidia kuendesha kiti mmoja wa walemavu wanaotumia kiti kutembelea.
Afisa Masoko na Uhusiano Bw. Silvester Bahati wa DTB kushoto akikbidhi zawadi kwa mkuu wa kituo hicho.
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa