Shirika la kiraia linaloitwa DORCAS limekabidhi mradi wa matenki mawili ya yakuvuna maji kwa Halmashauri jana katika shule mbili za msingi ambazo ni Kweditilibe na Zavuza za Kata ya Kiva,Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga, lengo likiwa ni kuwasaidia wanafunzi kupata maji kutokana na uhaba wa maji uliopo katika maeneo hayo.
Wakati wa kupokea mradi huo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bi.Fatuma Kalovya aliipongeza na kuishukuru shirika hilo kwa kutoa ufadhili huo ambao utatumiwa na vizazi vya sasa na vya baadaye lakini kuwahakikishia pia ufuatiliaji wa karibu wa matumizi mazuri ya mradi.
Bi Kalovya aliwaagiza viongozi wote wa vijiji na wa shule kuhakikisha wanasimamia na kutunza miundo mbinu hiyo ya maji waliyojengewa ili iweze kudumu kwa muda mrefu na wanafunzi kuendelea kunufaika.
Sambamba na hilo Kalovya amewataka viongozi wa shule hizo kuongeza gata za kupeleka maji kwenye tenki kuzuia upotevu wa maji wakati wa mvua, pia matenki kupata maji mengi yatakayotumika kwa muda mrefu kitu kitakachowafanya wanafunzi hao kupata muda wa kutosha wa kusoma badala ya kufuata maji sehemu zingine ambazo ziko mbali na shule.
Pia alitumia nafasi hiyo kuwaasa wananchi kuweka mazingira katika hali ya usafi na kuweka takataka zote katika madebe ya uchafu kuepuka magonjwa ya mlipuko kwani pamoja na shirika hilo kujenga matenki ya kuvuna maji pia limegawa madebe ya kuweka takataka.
Msimamizi wa mradi huo Bi Augusta Keiya alisema lengo hasa la mradi ni kuhakikisha pia usafi binafsi wa mtoto wa kike na hedhi salama na alisema kwa Wilaya nzima mradi umelenga kuwafikia wanafunzi elfu nne mia mbili (4200) katika shule 25 pamoja na wasichana 800 ambao hawapo shuleni. Kwa mwaka 2019 alisema watajenga matenki 6 ambapo kati ya hizo matenki matatu tayari yameshajengwa.
Keiya alisema ujenzi wa matenki hayo yenye ujazo wa lita 23000 kila moja ulianza 21/01/2019 ambapo mpaka kukamilika kila tenki liligharimu kiasi cha shilingi milioni 16.6. Ujenzi huo pia ulihusisha mafundi wa mtaani ambao walifundishwa namna ya kujenga matenki yanayotumia waya meshi na simenti pekee bila kutumia matofali au mawe kutoka shirika la SHIPO na kuwasihi mafundi hao waliofundishwa kutoa elimu hiyo kwa mafundi wengine ili wananchi waweze kupata mafundi wakutosha kwa gharama nafuu lakini pia kuongeza ajira katika jamii.
Walimu waliosoma risala akiwepo Mwl.Adamu Saidi wa shule ya msingi Kweditilibe na Mwl.Christina Mpanda wa shule msingi Zavuza walielekeza shukrani zao kwa shirika hilo kwani pamoja faida ya maji watakayopata pia walisema shirika limekuwa karibu na wanafunzi hasa wa kike kwa kutoa elimu ya usafi binafsi na hedhi salama.
Mtoto Abdalah Mokiwa kwa niaba ya wanafunzi ameishukuru sana shirika la DORCAS na SHIPO kwa kuwajengea matenki hayo kwakuwa walikuwa wanapata shida sana kupata maji ya kupikia na yakutumia chooni na alisema sasa hivi hawatakuwa na tatizo la maji kama zamani na kuahidi pia kutunza matenki hayo.
Imetolewa na kitengo cha habari
Halmashauri ya Wialaya ya Handeni.
03/04/2019
Kaimu Mkurugenzi Bi.Fatuma Kalovya akifungua maji baada ya kukabidhiwa mradi.
Fundi sanifu wa Halmashauri Bw.Omary Kipigo upande wa akikagua mradi
Mwonekano wa matenki ya lita 23000 kila moja yaliyojengwa na shirika la DORCAS.
Msimamizi wa mradi Bi.Augusta Keiya akitoa ufafanuzi wa mradi.
Maofisa mbalimbali wa shirika la DORCAS
Wanafunzi wa shule ya Kweditilibe wakichota maji katika tenki waliyojengewa na shirika hilo
Picha ya pamoja baada ya kukabidhi mradi
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa