WANAWAKE WATAKIWA KUBADILI FIKRA KIUCHUMI BADALA YA KUWAZA KUNUNUA MADERA.
Halmashauri ya Wilaya ya Handeni imeadhimisha siku ya Wanawake Duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 8/3 lengo likiwa ni kuwakumbusha wanawake kujikwamua kiuchumi na kujua haki zao za kisheria katika jamii. Kwa mwaka 2019 Halmashauri iliadhimisha siku hiyo katika Kata ya Kitumbi ikiwa na kauli mbiu inayosema “Badili fikra kufikia usawa wa kijinsia kwa maendeleo endelevu”.
Maadhimisho hayo pia yaliambatana na ugawaji wa mikopo yenye jumla ya kiasi cha shilingi Milioni 15.2 kwa vikundi vitatu vya wanawake na kikundi kimoja cha vijana.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Mh. Mustapha Beleko ambapo alisema ili mwanamke ajikwamue kiuchumi lazima atue ndoo ya maji hivyo amewahakikishia wananchi kuwa tatizo la maji lililotokana kukatwa kwa maji limeatatuliwa hivyo kuanzia leo usiku maji yataanza kutoka. Kwa upande wa Mkata alisema chazo cha Chalinze kimeanza kufanyiwa kazi na mkandarasi amepewa muda hivyo wakati wowote maji yatafika Mkata, pia alielekeza pongezi kwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya Mh. Athumani Malunda kwa kuwa bega kwa bega kufuatilia suala la upatikanaji wa maji Handeni.
Mh. Beleko alitoa rai kwa waliochuchukua mkopo kutumia mkopo huo kuzalisha kwani lengo la Mh. Raisi ni kuwainua kiuchumi wananchi na mkopo huo unatolewa bila riba na kwamba ili kikundi kipate mkopo mwingine lazima kirejeshe mkopo huo kwa wakati na pia itakuwa rahisi vikundi vingine kupata mkopo huo..
Aliwasihi wazazi kutokuwabagua watoto katika suala la kuwapa haki ya elimu kwamba kila mtoto lazima apate elimu hasa mtoto wa kike kwani wengi huwapeleka watoto wa kiume na kuwaacha wa kike.
Alihitimisha kwa kuwataka wananchi kujiepusha na maambukizi mapya ya UKIMWI kwakuwa kiwango cha maambukizi kimeongezeka kutoka asilimia 2.7 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 4 mwaka 2018 hivyo wapeane elimu kwamba UKIMWI bado upo na waache kujiliwaza kwamba dawa za kufubaza zipo, “gharama za kununua dawa hizi ni kubwa na tunairudisha nyuma nchi kimaendeleo”alisema.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Mkoa wa Tanga Dr. Aisha Kigoda aliwataka wanawake kutojiweka nyuma katika shughuli za uzalishaji mali bila kuogopa changamoto na pia wasisite kufuatilia haki zao za kisheria na kwamba hakuna mafanikio bila kujishughulisha.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Handeni Mh. Athumani Malunda aliwataka wanawake kutafuta fursa za kujiendeleza kiuchumi ili kuepuka unyanyasaji wa kijinsia na waache kufikiria kununua nguo badala ya kufanya kitu cha maana ambacho kitamkwamua kiuchumi hasa kujiwekeza kwenye umiliki wa ardhi.
Pia aliwasihi wazazi kuzingatia maadili ya watoto ili kujenga kizazi kijacho chenye maadili la sivyo watapoteza kizazi kijacho chenye maadili hasa suala la mavazi na lugha staha.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bw. Simon Mdaki aliwapongeza wananchi wa Kitumbi kwa kuanzisha ujenzi wa Shule ya Sekondari na kuwasihi kuhakikisha hakuna mtoto anayebaki nyumbani hasa watoto wa kike na pia aliwasihi kujitokeza kuchangia nguvu kazi katika ujenzi wa zahanati ili kupata huduma ya afya iliyokaribu kwa akina mama hasa kupeleka watoto kliniki.
Na kwa uchaguzi ujao alisema Mdaki wanawake wagombee nafasi mbalimbali ili iwe rahisi kusimamia haki za mwanamke katika jamii na kwamba wasikae nyuma wajiamini.
Bw. Mdaki aliwataka wananchi kujikinga na kipindupindu na kwamba viashiria vimeonekana hivyo wamama wachukue tahadhari kwani wana nafasi kubwa katika kuelimisha jamii na kuzuia kuenea kwa kipindupindu katika familia zao kwa kuwa wao wameshika Nyanja zote za usafi katika familia
Afisa Maendeleo ya jamii Bi. Amina Waziri akisoma majina ya vikundi vya wanawake na vijana wanaopewa mikopo alisema ili kikundi kipewe mkopo lazima kiwe na vigezo ikiwepo usajili wa Halamashauri na uwepo wa akunti benki, kujishughulisha na uzalishaji wa viwanda vidogo, shughuli endelevu iliyokwisha anzishwa na kwa upande wa vijana alisema kikundi lazima kiwe na watu wasiozidi umri wa miaka 18- 34.
Aidha, alisema kuna vikundi viwili vinavyotarajiwa kupewa mkopo wa mashine za kuchakata mihogo vyenye thamani ya shilingi milioni 17 kila moja ikiwepo kikundi cha wanawake cha jipemoyo kilichopo Kata ya Kitumbi na kwamba mchakato wa awali umeshafanyika ikiwepo sehemu ya kuweka mashine hizo ambapo tayari serikali ya Kijiji cha Kitumbi kimewapa ekari mbili bure kwaajili ya kujenga miundo mbinu ya kuweka mashine hizo.
Mwakilishi wa wanawake Bi.Clementina Nyoni akisoma risala alisema wanawake wapewe mikopo yenye riba nafuu ili wajikwamue kiuchumi pia aliomba viongozi wa serikali kusimamia sheria ili watoto wate katika jamii wapate elimu kwani watoto wa kike wamekuwa wakiachwa nyuma katika suala la elimu.
Katika maadhimisho hayoTaasisi na mashirika mbalimbali zilitoa salamu za siku ya wanawake wakiwepo MNB,shirika linaloshughulika na shughuli mbalimbali za maendeleo katika jamii( TANZACARE), Shirika linaloshughulisha na afya ya jamii(DSW), wasaidizi wa kisheria(NALIDO) na TAKUKURU ambapo mwakilishi wake Bw.Mwamkamba aliwataka wanawake kutoa taarifa katika vyombo vya kisheria pale mtu anapotaka rushwa hasa ya ngono ambayo inamrudisha mwanamke nyuma kimaendeleo, pia vikundi mbalimbali vya wanawake vilileta bidhaa zao.
Mgeni rasmi Mh. Beleko mwenye tisheti ya bluu kulia akikagua bidhaa zilizoletwa katika maadhimisho ya wanawake
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Handeni Mh. Athumani Malunda akitoa nasaha
Mwenyekiti wa umoja wa wanawake Mkoa wa Tanga Dr. Aisha Kigoda akitoa neno
Kaimu Mkurugenzi Bw. Mdaki akizungumza katika maadhimisho hayo
Afisa maendeleo ya jamii Bi. Amina Waziri akisoma taarifa
Burudani mbalimbali zikiendelea katika maadhimisho hayo
Mgeni rasmi Mh.Beleko wa kushoto akiwapa vyeti viongozi wa vikundi waliopewa mkopo
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa