Wakala wa barabara mijini na vijijini (TARURA) na Shirika la umeme Tanzania Wilaya ya Handeni walitoa ufafanuzi wa miradi wanayotekeleza Handeni katika baraza lililofanyika leo tarehe 16/05/2019 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni baada mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mh.Mustafa Beleko kuomba ridhaa kwa madiwani ya Tasisi hizo kuwa sehemu ya baraza ili kujenga uelewa wa pamoja juu ya miradi inayofanyika katika maeneo yao ambapo waliridhia na baadaye waheshimiwa hao kuuliza maswali ya kwanini miradi hiyo haikufika katika baadhi ya maeneo ya vijiji vya Kata za Halmashauri ya Wilaya ya Handeni.
Akitoa taarifa, kaimu Meneja wa TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Mhandisi William Lusubilo alisema kwa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni TARURA inasimamia barabara zenye jumla ya kilometa 796.83 na kwa upande wa hali ya barabara hizo amesema kilometa 224.14 ni changarawe ambapo kilometa 186.71 ziko katika hali nzuri na 37.43km ziko katika hali ya kawaida.
Amesema kilomita 572.69 ni barabara za udongo ambapo kati ya hizo 309.04 zipo katika hali nzuri na zinapitika, 125.76km ni za kawaida na 137.89km ziko katika hali mbaya na hakuna barabara ya lami. Bw. William amesema hadi kufikia mwezi machi 2019 utengenezaji na ukarabati wa barabara umefanyika hasa kwa maeneo korofi pamoja na ujenzi wa makavati, Kwa barabara ambazo bado haziko kwenye mtandao wa serikali amewaahidi kuendelea kufuatilia ili ziingizwe na kupewa fedha za matengenezo kwa kuwa fedha zinatolewa kulingana na barabara ambazo ziko kwenye mtandao wa serikali.
Aidha, amewaasa waheshimiwa madiwani kusimamia na kutoa elimu kwa jamii suala la upitishaji wa mifugo katikati ya barabara kwani wamekuwa wakichangia uharibifu wa barabara hizo kwa kiwango kikubwa na kwamba endapo mtu atakamatwa anapitisha mifugo atapigwa faini ya shilingi 5000 kwa kila mfugo.
Naye Meneja wa TANESCO Handeni Bw.Meshack Masanyiwa amesema Halmashauri ya Wilaya ya Handeni imepata umeme wa (REA) katika vijiji 8 ambavyo ni Kwamnele, Madebe, Kwaluguru, Nyasa, Kibaya, Kangata, Kilimamzinga na Kweisasu na wanaendelea kusambaza miundombinu hiyo ili huduma iweze kuwafikia wananchi wote wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni
Meneja huyo pia amesema Serikali imesikia kilio cha wananchi Hivyo imeshusha bei kutoka shilingi 177,000 hadi shilingi 27,000 kuunganishiwa umeme kwa mtu ambaye hahitaji nguzo kwamaana ya wateja ambao wako ndani ya mita 30 kutoka umbali wa nguzo ya umeme.
Pia katika kikao hicho cha Baraza la madiwani ulifanyika uchaguzi wa makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni baada nafasi hiyo kukaa wazi kwa muda wa takribani miezi 6 kufuatia aliyekuwa makamu mwenyekiti kuchaguliwa na kuwa mwenyekiti wa Halmashauri hiyo. Mh. Sharifa Abebe wa Kata ya Kwamgwe kupitia tiketi ya CCM aliibuka kidedea kwa kupata kura zote 26 za ndiyo za wajumbe waliohudhuria baraza hilo.
Mwenyekiti wa Halmashauri Mh.Mustafa Beleko akizungumza na wajumbe wa Baraza.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Handeni Bi. Fatuma Kalovya akisoma agenda za kikao
Kaimu Meneja wa TARURA Mhandisi William Lusubilo akisoma taarifa.
Meneja wa TANESCO Wilaya ya Handeni Bw. Meshack Masanyiwa akizungumza
Wajumbe mbalimbali wa Baraza la Madiwani wakichangia hoja
Wajumbe wakipiga kura.
Afisa uchaguzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bw. Francis Mashalo kushoto na Mh. Muya wakihesabu kura wakihesabu.
Pichani ni Makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Mh.Sharifa Abebe ambaye ameshinda kwa kura zote za wajumbe 26.
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa