Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni wametakiwa kuchukua hatua stahiki ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya ukimwi kwani UKIMWI upo na maambukizi bado yapo.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Hamlamashuri ya wilaya ya Handeni William Makufwe ambaye ndiye mgeni rasmi kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya, kwenye maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani yenye kauli mbiu ya “ Changia mfuko wa udhamini wa ukimwi,okoa maisha, Tanzania bila ukimwi inawezekana”.
Makufwe alisema maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani yanatoa nafasi kwa wananchi na jamii kujitathmini, kujipima na kujitafakari katika kujua tabia na mienendo katika kujikinga na janga zima la ukimwi.
Aliongeza Kuwa UKIMWI ni tatizo kubwa ulimwenguni hususani kwa nchi zinazoendelea, na kwamba Handeni kama maeneo mengine ya Tanzania wanakila sababu ya kutafakari na kutathmini kuhusu athari za ukimwi na namna ya kupambana na maambukizi mapya.
Makufwe amesema Serikali inajitahidi kupambana na janga la Ukimwi kwakua athari zake ni kubwa ikiwemo kuongezeka kwa watoto yatima,kupoteza nguvu kazi hatimaye kuongezeka kwa umasikini ngazi ya familia hadi taifa hivyo ni muhimu kuchukua hatua stahiki kujikinga na maambukizi mapya.
Aidha ametoa wito kwa wananchi kujitokeza katika upimaji wa afya zao mara kwa mara, kupinga ndoa za utotoni, kufanya kazi kwa bidii kuepuka vishawishi na kuhakikisha wazazi na walezi wanawalea watoto na vijana wao katika maadili yaliyomema yatakayowasaidia kujiepusha na maambukizi ya Ukimwi.
Kwa upande wake Makamu mwenyekiti wa Halmashauri na Mwenyekiti wa Kamati ya Ukiwmi Mh. Abdallah Pendeza amesema ukimwi upo na maambukizi yanaongezeka ni vyema kwa kutumia maadhimisho haya hatua ikachukuliwa.
Alizitaka kamati za ukimwi ngazi ya Kata na Vijiji kuhakikisha zinafanya kazi ya kuelimisha wananchi kuacha ngono zembe na visababishi vingine vinavyosababisha maambukizi ya virusi vya Ukimwi.
Maadhimisho ya Ukimwi Halmashauri ya Wilaya ya Handeni yamefanyika katika shule ya Msingi Magamba kata ya kwaluguru na kushiriki kwa vikundi mbalimbali vya burudani.
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya Handeni . Haki zote zimehifadhiwa